Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Deodatus Philip Mwanyika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Njombe Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia kwenye bajeti hii ya Wizara ya Kilimo. Awali ya yote ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri sana aliyoitoa hapa inayotupa matumaini makubwa kwenye kilimo. Kwa kweli Wizara hii imefanya kazi kubwa na inafanya kazi kubwa kuendeleza kilimo. Mambo yanayofanyika ni mengi na tunawapongeza sana kwa kazi nzuri wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kuna maeneo machache ambayo niliona niyazungumze, ambayo mengi tumeyaongelea kwenye Kamati, lakini nime-pick machache ambayo ni muhimu kwangu na kwa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia uzalishaji wa mazao ya asili ya biashara, Wizara inafanya vizuri sana kwa ujumla, hasa kwenye uzalishaji. Masuala ya bei yana complications zake na bei zinapanda na kushuka, lakini kiuzalishaji, mazao mengi yanafanya vizuri sana. Ukienda kwenye korosho, inafanya vizuri sana kiuzalishaji, kahawa, mkonge unafanya vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaposema vizuri, ni malengo waliyojiwekea ukilinganisha na walipofikia. Kwa kiasi kikubwa, haya mazao kama korosho yapo 80%, kahawa 90%, mkonge 90%, pamba 60%, tumbaku wako 95%, hata sukari wako 70%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake ni kwamba kwa ujumla, amesema kwenye ripoti yake, mpango ulikuwa ni kuzalisha tani milioni 2.2 kwa ujumla kwa mazao hayo yote, lakini wameweza kufikia tani milioni 1.5. Kwa hiyo, progress ni nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kuna baadhi ya mazao ambayo kwa kweli ni tatizo kubwa sana. Zao ambalo linaongoza na lenye changamoto kubwa kwenye Wizara hii ni zao la chai. Zao la chai, tunavyoongelea sasa, uzalishaji wake umeendelea kuporomoka siku hadi siku. Malengo yalikuwa ni kuzalisha angalau tani 30,000, lakini mpaka Februari walikuwa tani 9,000 na ilikuwa inaonyesha wapo tani 10,000. Hali hii siyo nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwa karibu sana, utagundua kinachosababisha zao la chai kuporomoka, sababu kubwa ni viwanda kutozalisha, na viwanda kufungwa. Kuna viwanda nane ambavyo vimefungwa. Kama kiwanda kinazalisha chini ya asilimia tano ni sawa na kama kimefungwa, lakini kuna vile ambavyo vimefungwa kabisa havifunguliwi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda ukaangalia viwanda vilivyofungwa, mfano Rungwe kuna viwanda kama vitatu vimefungwa. Ukija Njombe kuna viwanda vitatu vimefungwa, na Mufindi kuna viwanda viwili vimefungwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda ukaangalia zaidi vimefungwa kwa sababu gani? Cha kwanza utagundua kwamba vimefungwa kwa sababu kuna mwekezaji ambaye au hana uwezo ama hana nia ya kuendeleza zao la chai. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaongea nikiwa nimeongozwa na data za uzalishaji wa viwanda hivyo. Ukiangalia hivi viwanda nilivyovitaja, vyote kwa pamoja, kimoja kinazalisha tani 8,000, kimoja 6,000, kimoja 2,000. Kuna uzalishaji wa viwanda vinne au vitano vya mwekezaji mmoja ambaye ni DL Group, hawa peke yao wana uwezo wa kuzalisha tani 17,800.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa masikitiko sana, uzalishaji wao sasa hivi ni tani 320, chini ya asilimia tatu. Sasa hili siyo jambo la kufumbia macho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Watanzania tuna jambo letu. jambo letu ni Dira. Dira inatuambia kwamba 2025 kwenda 2050, tunataka private sector ichangie 70% kwenye hiyo dola trilioni moja ambayo tunatakiwa tuwe nayo au tuizalishe na pato la mtu liwe dola 7,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwendo huu ambao tunakwenda kwenye viwanda, nchi yetu lazima iwe tayari kufanya maamuzi magumu. Nilikuwa ninatafuta neno zuri, “maamuzi magumu.” Katika maamuzi magumu ni pamoja na kufanya evaluation ya aina ya uwekezaji ambao tunao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu inavutia wawekezaji, lakini tunapovutia wawekezaji kuna baadhi ya wawekezaji hawatufai. Ninalisema hili kwa sababu nimeongea ndani ya Bunge hili kwa miaka mitano pamoja na wenzangu kuhusiana na zao la chai kwenye maeneo ya Mufindi, Njombe mpaka Rungwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli ni kwamba tuna mwekezaji ambaye alipewa viwanda kwa nia njema na Serikali kupitia benki, lakini uwezo wake umeonesha kwamba ni mdogo kuendesha hivyo viwanda. Kama tunataka kufikia lengo letu la private sector kuwa ndiyo engine ya kutusaidia kule mbele ni lazima tuwe tayari kufanya maamuzi sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2021 mwezi Machi, Mheshimiwa Majaliwa Majaliwa akiwa Waziri Mkuu alitembelea Njombe, akakaa na wadau wa chai na yaliyojitokeza yalikuwa wazi kwamba, mwekezaji huyu tunayemwongelea ambaye ni DL Group kutoka nchi ya mbele ya Mlima wa Kilimanjaro. Mwekezaji huyu ilionekana wazi na haya siyo maneno yangu ni maneno ya Mheshimiwa Waziri Mkuu wa wakati ule kwamba, anatuhujumu. Ni mhujumu uchumi hapa nchini, kwa sababu hawezi kuendesha viwanda, wafanyakazi wengi kule wamepunguzwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, …

MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa Edwin Swalle.

TAARIFA

MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ninataka nimpe taarifa Mheshimiwa Deo Philip Mwanyika anayechangia vizuri sana kuhusu zao la chai. Amerejea hotuba ya Waziri Mkuu Mstaafu, Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa ya tarehe 9 Machi, 2021 Njombe na mimi nilikuwepo. Waziri Mkuu alisema mwekezaji anayemiliki viwanda hivi vya Kibena, Lupembe na Luponde inaonekana kama anafanya sabotaging kwenye zao la chai hapa nchini. Hivyo ndiyo taarifa ambayo nilitaka nimwongezee Mheshimiwa Deo Mwanyika. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Deo Mwanyika, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipokea taarifa hiyo. Ninamshukuru sana mdogo wangu Wakili Enosy Swalle. Matokeo ya jambo hili ni kwamba mapato ya Taifa, ya Serikali na halmashauri yameporomoka kwenye maeneo hayo yote, ajira zimepotea, fedha za kigeni tulizozitegemea hazipo tena, migomo ya wafanyakazi ni jambo la kawaida inaendelea, ilianza Mufindi baadaye imehamia Njombe, lakini pensheni za wafanyakazi hazilipwi na huyu mtu. Sisi tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutambua nia nzuri ya kumwita mwekezaji, aliruhusu Wizara ifanye utaratibu wa kutafuta fedha angalau kumsaidia mwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, alipewa shilingi 10,000,000,000 siku za karibuni, mwaka jana. Pamoja na kupewa shilingi 10,000,000,000 hali bado ni mbaya, hakuna mwanga. Hizi fedha siyo fedha za kutoka huko anakotoka, hizi ni fedha za nchi yetu, za Benki yetu hapa ya CRDB. Kwa hiyo, niseme kwamba aina ya huu uwekezaji ni lazima tukubaliane. Ndiyo mambo aliyosema Profesa Kitila lets try to do business unusual, let’s do business unusual. Tunataka wawekezaji ni kweli na sisi hatutaki kupeleka meseji mbaya kwa wawekezaji, lakini mwekezaji anayeturudisha nyuma, mwekezaji ambaye anarudisha umaskini kwa wananchi! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, chai ni zao ambalo linaongeza ajira kwa watu wa kawaida. Chai ni zao ambalo watu wanauza, wanapata hela ya kwenda kulipa ada. Chai ni zao ambalo wanalipa hela ya matibabu. Leo hii watu hawawezi kufanya hayo mambo kwa sababu mwekezaji amefunga viwanda, hata chai yake anashindwa kuhudumia. Hawezi kuweka mbolea, hawezi kubadilisha mashine, hawezi kununua spare, hata umeme anashindwa kulipa. Hivi huyu mwekezaji wa aina hiyo, kwa nini Serikali isifanye maamuzi magumu ya kutatufa njia ya kuachana naye? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wazo letu na wazo langu. Ni wakati sasa wa kutafuta wawekezaji wengine wa uhakika maana wapo. Wapo na tuombe sana benki ya CRDB itusaidie kwenye hilo, kwa sababu wao wame-finance, siamini kama wanaona mwanga kwenye jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huhitaji kuwa financial guru kujua kwamba this is a failure business, huhitaji, unaona namba zinajionesha wazi kabisa. Ukizalisha kwa uzalishaji huu na migomo inayoendelea deni la pensheni peke yake la wafanyakazi ni shilingi bilioni 4.7. Hata hivyo, analipa mishahara kwa kusuasua na hapeleki hata hizo pensheni bado kwa wafanyakazi. Kwa hiyo, hatuwezi kuendelea na hii hali, we have to make a decision.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, nina matumaini makubwa kwamba analifahamu na nina uhakika sana kwamba Waziri wetu ana uwezo wa kutusukuma tukafika mahali pazuri kwenye jambo hili. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, sisi tuna matumaini makubwa naye, tunakutegemea sana kwenye jambo la chai. Bahati nzuri na yeye ni mkulima wa chai, ninayoyasema haya na yeye anayapitia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilipenda niongelee chai kwa uzito huo na niombe sana Serikali ifanye maamuzi. Wakati ninamshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia kwa kusababisha hawa wamepata pesa, lakini hizo pesa hawazitumii kama inavyotakiwa. Hata hivyo, wanafanya vizuri kwenye mazao mengi na zao la parachichi pamoja na mbogamboga, Wizara hii imelisimamia vizuri sana na linafanya vizuri sana. Tumeona hapa linakwenda vizuri, production iko above the target wanaongelea 108%. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe sana bado kuna changamoto. Zao la parachichi ni very delicate, lakini linaweza lika-transform uchumi wa nchi hii. Unaposema ni green gold, it’s real means green gold. Lina uwezo mkubwa wa ku-transform uchumi wa nchi hii na kubadilisha maisha ya wananchi wa kawaida. Niwaombe sana, kuna changamoto ndogondogo pale na ninawapongeza sana watu wa COPRA wamekuwa mstari wa mbele kushirikiana na wakulima kutatua changamoto, kwa hiyo, tuwatie moyo waendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwenye chai tuwaambie watu wa Bodi ya Chai wapo, kazi yao ni kusimamia zao hili. Tunapiga kelele miaka yote hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Waziri akiweza aanze na kubadilisha hiyo bodi. Hatuwezi kuwa na bodi ambayo hatuoni mwanga kwa miaka mitano. Ni vema tukatafuta watu wenye uwezo na walio na commitment ya kubadilisha zao la chai ambalo lina watu wa kawaida wengi sana wanaolitegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu umwagiliaji. Tumesema hapa kwamba kwa kweli fedha zinakwenda kidogo kidogo na sisi tuombe, ukiangalia statistics za success kwa maeneo ambayo yameshapata umwagiliaji. Niwaombe Wabunge pamoja na kwamba tuna matatizo kwenye umwagiliaji, lakini tukumbuke kwamba umwagiliaji ndiyo utakaotutoa nchi hii. Kwa statistics za haraka haraka, kwa kiasi ambacho tume-invest kwenye umwagiliaji kwa maeneo yale mpaka muda huu, tumeongeza eneo la umwagiliaji mpaka kufika hekta 800,000 kutoka hekta 400,000 mwaka 2015, lakini lengo letu ni kufika hekta milioni 1.5.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tija imeanza kusikika, mpunga, mahindi na vitunguu zote kwa pamoja zimeongeza uzalishaji kwa tani kwa kila hekta. Ukiangalia mpunga tulikuwa 1.5 tons per hectare, tupo five mpaka seven. Mahindi tulikuwa 1.5 tons per hectare tupo 3.7 mpaka 5.0. Nyanya tulikuwa 5.0 tons per hectare tupo 18 tons per hectare kwa sababu ya umwagiliaji. Vitunguu vilikuwa 13 tons tuko 26 tons per hectare. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sana bado tuna matumaini makubwa kwamba ni vizuri fedha zikatolewa. Tuombe kuna miradi mikubwa ambayo tunaweza kusema ni game changer. Miradi hii ni miradi ambayo itatusaidia sana na miradi hii, kwa vile ceiling yetu ya Wizara ni ndogo, tukiendelea kuiweka kwenye hiyo hatutaweza kufanikiwa, tuiweke kama miradi ya kimkakati ili tupate financing kutoka Serikalini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)