Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Kabla sijaanza nikumbushie jimboni kidogo, kuna scheme ya umwagiliaji Mheshimiwa Waziri anaijua ya Balili, ilipata madhara ya mvua, sasa hivi imeharibika tunahitaji pesa ya dharura pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nisisitize, mchangiaji aliyepita amezungumzia miradi ya umwagiliaji ya kimkakati. Kama kweli tunataka tupige hatua kwenye kilimo, ile miradi 26 ambayo imezungumzwa kenye taarifa ya Kamati lazima tuifanye ya kimkakati kama ambavyo tumefanya Bwawa la Mwalimu Nyerere, kama ambavyo tumefanya SGR na maeneo mengine ya kimkakati, ndiyo tutatoka hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifanya hivyo, tutakuwa na uhakika wa kutenga pesa za kutosha katika miradi ya umwagiliaji. Lazima iwe miradi ya kimkakati ili tuondokane na kilimo cha kutegemea mvua. Hilo Mheshimiwa Waziri lazima alichukue, ili ile ndoto ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kufanya kilimo, kiwe kilimo cha biashara na siyo watu waone kilimo ni mateso, waone kilimo ni starehe, kilimo pesa, kilimo mali, lazima tuwekeze katika kilimo cha umwagiliaji kwenye miradi ile 26 ya kimkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nizungumzie zao la parachichi. Tunazungumza kila siku kwamba parachichi ni green gold. Parachichi duniani huko inahitajika kweli kweli na soko lake lipo wazi. Zao la parachichi halina msimu. Parachichi ukienda India, parachichi moja ya Hass unanunua kwa shilingi 10,000 au 15,000. Mheshimiwa Waziri anajua, bandari yetu haina miundombinu rafiki ya kusafirisha mazao ya mbogamboga na parachichi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama zao hili linailetea pesa za kigeni nchi yetu, kwa nini hatuwezi kutengeneza miundombinu katika bandari yetu? Leo hii wakulima wa parachichi wanatumia zaidi ya dola 6,500 kwenda kusafirisha kwa kulipia gari la kwenda kupeleka bandarini. Wanaenda Mombasa kwa sababu Bandari ya Mombasa kuna miundombinu mizuri kwa ajili ya kuwezesha wakulima kusafirisha matunda pamoja na mboga mboga. Tungekuwa tuna miundombinu yetu kwenye Bandari yetu ya Dar es Salaam, wakulima wangetumia dola 2,000 tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa nini tusione kwamba ni wakati muafaka wa bandari yetu yenyewe iweze kujitosheleza, siyo tena wakulima wetu wa hapa wanaenda Bandari ya Tanga, kiuchumi haijakaa sawa. Yaani sisi tunaenda kunufaisha nchi nyingine wakati tuna uwezo wa kutengeneza miundombinu yetu katika bandari yetu na wakulima wetu tukawaondolea mzigo mkubwa wa pesa kwa ajili ya lile gari la kusafirisha kwenda kupeleka parachichi bandarini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, Mheshimiwa Waziri anajua kwamba maeneo ambayo kuna mashamba ya parachichi, barabara zake ni mbovu. Zao la parachichi linahitaji uangalizi wa hali ya juu. Leo hii mkulima unaweza ukavuna parachichi let say tani tano au kumi, barabara ikiwa mbovu mpaka uende kwenye park house, unaweza ukaambiwa tani mbili zote, tani tatu zote ni parachichi ya kiwango cha pili. Unaambiwa reject ingawa sisi wakulima wa parachichi hatutaki suala la reject.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa lazima Mheshimiwa Waziri, Wizara yake na Wizara ya Miundombinu kupitia kule TARURA kuhakikisha maeneo yote yenye mashamba ya kimkakati ya parachichi, barabara zinapitika muda wote, ili wakulima wa parachichi wawe na uhakika wakitoa zao kwenda kupeleka kwenye park house, basi tunda liwe na ubora. Likisafirishwa, lisafirishwe kwa kiwango kikubwa, mkulima apate pesa ya kutosha na Serikali ipate mapato. Hilo ni jambo la msingi sana na Mheshimiwa Waziri anayajua mashamba ya parachichi, kote barabara hazipitiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaenda kwenye msimu wa mwezi Agosti, ukienda kule Mgala, Kifanya na maeneo mengine Mafinga, barabara hazipitiki wakulima wa parachichi wanalalamika. Watashindwa kuvuna, wakishindwa kuvuna matunda yataoza. Parachichi ni green gold, wanaiacha gold inaoza shambani, kwa sababu miundombinu haipitiki? Hapana, lazima tuwe tuna mkakati wa kutosha. Mheshimiwa Waziri anajua dawa za kuulia wadudu za parachichi ni very expensive, wakulima wetu wengi hawawezi kumudu. Ni wakati muafaka sasa wa kupata ruzuku kwa ajili ya dawa za parachichi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutoe elimu kwa wakulima wetu wadogo, kwa sababu usipowapa ruzuku wanashindwa kuwahi kupuliza dawa kwa wakati. Hawezi kupata mazao ya kutosha yenye ubora. Utakuta anakuwa na maparachichi ambayo hayana standards ambazo zinatakiwa kwenye soko huko duniani, lakini tukiwapa ruzuku wakulima wa parachichi, wakalima vizuri na tukatoa elimu ya kutosha kwa wakulima wadogo wadogo, ninaamini kabisa parachichi yetu itaenda mbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niwaambie kwa Afrika, Tanzania parachichi yetu ni bora sana sana na ndiyo maana kuna hila za kiuchumi ya nchi jirani hapo, kutaka kuonesha parachichi letu ni baya lakini tuna parachichi bora na linatoka Njombe, lazima kama Watanzania tupige…

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa Elibariki Kingu.

TAARIFA

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mchango wa kizalendo sana unaotolewa na Mheshimiwa Bulaya, ninaomba nimpe taarifa kwamba, pamoja na kwamba anawaombea wakulima waweze kupewa ruzuku ya viuatilifu, lakini kwa sababu duniani maparachichi yanabidi yatumie mbolea ya organic ni wakati muafaka kwa Serikali kuingiza mbolea ya organic katika ruzuku ili wakulima wa Tanzania wapate access ya masoko duniani. Ninaomba kutoa taarifa. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ester Bulaya, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipokea taarifa ya Mbunge bingwa kabisa. Kwa hiyo, kwenye parachichi Mheshimiwa Waziri amenielewa. Nimesoma hotuba yake amesema kabisa mbegu ni usalama wa nchi na amezungumzia mbegu ni chakula. Tuna Taasisi ya Serikali ya ASA, ninaomba waiwezeshe, inahitaji hekta 60,000 ili waweze kumaliza changamoto ya mbegu ili tusitegemee watu wanaoagiza mbegu nje. Amezungumza vizuri kabisa mbegu yetu ya ASA inastahimili ukame, mazingira yetu sisi Watanzania kuliko mbegu za nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii wana ardhi hekta 17,000 na kwenye hiyo hekta 3,000 tu ndiyo ina miundombinu ya umwagiliaji. Hivi tukiwawezesha hawa wakahakikisha wanalima kwa msimu mara mbili kwa mwaka, hatutakuwa na shida ya mbegu, yaani tutakuwa tuna mbegu zetu wenyewe. Watu waliotumia mbegu za ASA leo hii hawataki kutumia mbegu nyingine na mbegu zao ni bei rahisi, shilingi 7,000 tofauti na watu wengine ambao wanaleta mbegu zingine ambazo siyo nzuri zaidi ya 15,000. Kwa nini tusiiwezeshe taasisi yetu ya Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine Mheshimiwa Waziri tunaomba wawalipe wakulima ambao wameingia mikataba, wanalima mbegu. Hivi tunavyozungumza wanadai zaidi ya shilingi 3,000,000,000. Mkulima anakopa benki, anatakiwa ajiandae vizuri kwenda kwenye msimu mpya mpaka sasa hivi wanadai shilingi 3,000,000,000. Tunaenda kuvuna, tunaanza mwezi Juni mwishoni, Julai, mpaka kuhakikisha mbegu zimechakatwa, tunaenda mwezi Septemba, mpaka Oktoba, anatakiwa ajiandae, lakini hajalipwa bado! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawezaje kuhakikisha tuna mbegu zetu wenyewe tunazozizalisha nchini, kama huyu mkulima nyinyi mnampa shamba, hela ya kwake na bado wanachelewa kumlipa atawezaje kuwaletea mbegu? Tumeshasema sisi wenyewe tuna uwezo wa kuzalisha mbegu bora. Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Waziri wa Fedha yupo hapa, wakulima wanadai, mbegu ni usalama wa nchi, tuna taasisi yetu wenyewe, kwa nini tusiiwezeshe tukawa na uhakika. Mbegu ni chakula, chakula ndiyo usalama wa nchi. Why tutegemee nje wakati tuna taasisi yetu ina mbegu ambazo zinaendana na mazingira yetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine Mheshimiwa Waziri ni kuhusiana na ushirika. Nimeambiwa wana mizani ya kidijiti, wametumia zaidi ya shilingi 15,000,000,000 kuinunua; zaidi ya mizani 4,000 na wameisambaza, ila kuna fitina kwa watu kule, viongozi wa ushirika kule hawataki, kwa sababu hii inadhibiti kuwaibia wakulima. Ninaomba washikilie hapo hapo, wakatoe elimu, mizani hii itumike na wawaondoe vishoka kwenye vyama vya ushirika wanaowadhulumu wakulima huku. Kuna wizi mkubwa sana na ndiyo hiyo yote inaondoa sifa ya vyama vya ushirika kuonekana vibaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ile mizani wameijaribu imefanya vizuri, wale viongozi hawawezi ku-temper nayo, tunaomba wawaelimishe wakulima itumike ili mkulima asiibiwe…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, la msisitizo hilo nililokwambia Waziri la pamba jimboni kwangu, aliangalie kwanza, tunahitaji mabomba 1,200 kwa ajili ya kunyunyuzia wadudu kwenye wakulima wa pamba. Ahsante sana. (Makofi)