Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia. Ninaomba nimtangulize Mwenyezi Mungu katika mchango wangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na pongezi nyingi kwa Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Chongolo; Naibu Waziri; Katibu Mkuu, Mr. Mweli; Naibu Makatibu Wakuu; na viongozi wote waliopo katika Wizara ya Kilimo kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya katika Wizara yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya 90% ya wananchi wa Kilolo ni wakulima, wanategemea kilimo. Hivyo niiombe Serikali sasa hizi Wizara ziweze kusomana. Niiombe Serikali kuhakikisha kwamba Wizara zetu zinasomana ili barabara zote za kiuchumi na za kilimo ziweze kupitika wakati wote, ili pembejeo ziweze kufika kwa wakati kwa wananchi, lakini vilevile, mazao yaweze kufika sokoni kwa wakati ili uchumi wetu uweze kukua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba vilevile nichangie zao la chai. Ninaungana na Mheshimiwa Mwenyekiti wetu wa Kamati ya Kilimo kuhusiana na zao la chai. Kwanza ninapongeza Serikali, ilikuwa na nia nzuri kabisa hii Awamu ya Sita kuhakikisha kwamba, wanafufua viwanda vya chai, lakini bahati mbaya sana Kilolo na sisi tumepata mwekezaji, ambaye hawezi kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya miaka 30 wakulima wa zao la chai wa Kilolo walikuwa wanasubiri kwa hamu kuona sasa wanapata mkombozi wapate mwekezaji, ambaye atawasaidia, lakini bahati mbaya yule mwekezaji wa Kichina tuliyempata ni changamoto kubwa sana. Wananchi wanalia, wanasema yule mwekezaji anataka auziwe chai yao iliyochumwa kwa sindano, wakati wananchi wanachuma chai yote kwa hiyo, hawana pa kupeleka, hawana soko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunategemea kwamba, soko la wakulima wa chai ni kiwanda. Mheshimiwa Waziri kwa hiyo, nakuomba, kwanza uje uwatembelee Wananchi wa Kilolo uone wewe mwenyewe jinsi yule mwekezaji anavyowatesa wananchi wa Kilolo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba, ipo AMCOS ambayo ina uwezo na kuna wakulima wana uwezo kuliko huyu mwekezaji ambaye yupo. Tushukuru sana ushirika unawezesha hivi vyama viweze kuendesha viwanda vyetu. Kwa hiyo, ninaomba aje Kilolo na tunaomba kiwanda cha chai ili wananchi wa Kilolo wapate soko; walikuwa wanataka hata kuondoa kabisa, ili waweze kulima kilimo kingine kwa sababu, ukiangalia waliolima parachichi wameshazungusha mara tatu, mara nne. Waliolima miti wameweza kuvuna mara tatu, mara nne, lakini wao miaka zaidi ya 30, hakuna walichopata. Kwa hiyo, ninamwomba Waziri, Mwenyekiti wetu ameongea sana, zao la chai sasa liweze kupata suluhu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua Waziri pia, amekulia katika hili zao la chai. Kwa hiyo, tunajua atakuwa suluhisho kuhakikisha sasa hili zao linawasaidia wakulima, linaleta ajira na linaleta uchumi mkubwa katika hii nchi. Atakapokuwa anahitimisha hoja hebu sema neno moja, kwa ajili ya Kilolo waweze kupona. Tupate kiwanda kitakachowasaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba vilevile nizungumze kuhusiana na ushirika kwa kweli, yapo mambo mazuri. Benki ya Ushirika pia, itawasaidia sana wakulima wetu, tunaomba iwezeshwe, wakulima wengi waende kwenye hivi vyama, waweze kukopa kwa kiasi kikubwa, ili kilimo chetu kiwe na tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapongeza vilevile tumeona wamezindua, “Linda Ushirika Chagua Uadilifu.” Ninaamini kabisa vyama vyetu vingi vilikuwa vinakufa kwa sababu, kulikuwa kuna ubadhirifu mkubwa. Kwa hiyo, kutokana na hii kampeni yao tunategemea sasa vyama vingi vitafanya vizuri na vitawezeshwa, ili viweze kufanya vizuri katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaungana na wote kwamba, Tume ya Umwagiliaji ipewe pesa ya kutosha, ili miradi ya umwagiliaji ile iliyoanzishwa ikamilike iweze kuleta tija, tunaomba sana. Katika Kamati yetu tumezungumzia sana, miradi mingi imeanzishwa haikamiliki kwa hiyo, gharama ya hii miradi inakuwa kubwa sana kama haikamiliki kwa wakati. Tuombe sana Tume ya Uwekezaji ikamilishe miradi yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Kilolo tumepata mradi wa shilingi bilioni 4.4 katika Kata ya Ruaha Mbuyuni, tunashukuru sana, lakini pia, tuna mradi wa shilingi bilioni 23.9. Hii miradi tuna imani sasa inakwenda kukamilika, leteni pesa ikamilike, ili wananchi wa Kilolo na sisi tuweze kutumia miradi hii kuhakikisha kwamba, kilimo chetu kinakuwa na tija. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie vilevile kuhusu zao la parachichi. Kwa kweli, ninapongeza sana zao hili sasa hivi ni la mkakati kupitia COPRA, mtendaji wake dada Irene tunamshukuru sana, ameweza kufanya vizuri sana. Sasa hivi kutakuwa kuna miche ya ruzuku kwa Mikoa ya Iringa, Mbeya, Njombe na Songwe, kwa hiyo, tunaomba sasa hii ruzuku igawiwe vizuri na ikiwezekana hata katika shule zetu sasa hivi wajifunze kuwa na hili zao liweze kuwasaidia, ili wanapokua pia, waendelee kujua kwamba, ukitaka mali utaipata shambani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tushukuru pia kwamba, sasa hivi tutakuwa na collection center katika kata mbili katika Wilaya yetu ya Kilolo. Tunawashukuru sana COPRA, endeleeni hivyo tuhakikishe kwamba, zao hili pia linachangia uchumi wa kutosha (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba viwanda vyetu vya mbolea viwezeshwe, ili mbolea tutegemee viwanda vya ndani, sasa hivi kuwe na mpango maalum kabisa wa kupunguza gharama ya ruzuku. Tukiwa na viwanda vyetu, tukiviwezesha, tuna uhakika kabisa bei ya mbolea itashuka, kuliko kutegemea viwanda vya nje ambavyo kama kutakuwa kuna vita wananchi wanapata shida, bei inakuwa gharama kubwa, wananchi wanashindwa kujitegemea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba vilevile kuwepo na mpango mkakati wa kulipa madeni ya kampuni hizi za mbolea, karibu shilingi bilioni 398 zinadaiwa. Ninajua wakiwezeshwa, wakilipwa, basi tutapata mbolea kwa wakati. Kumekuwa kuna changamoto kubwa sana, mbolea haipatikani kwa wakati, wakulima wanapata shida sana wakati wa kupanda. Kwa hiyo, ninaomba Serikali ihakikishe kwamba, mbolea inapatikana kwa wakati katika maeneo ya wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante kwa mchango wako. Kengele ya pili.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ninaomba Wizara ya Kilimo wapatiwe pesa kwa wakati, ili miradi iweze kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)