Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ushetu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote, nimshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kibali hiki cha kuweza kusimama ndani ya Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendelea pia kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa namna alivyoweza kufufua ushirika hapa nchini na kuimarisha vyama vya ushirika. Pia, ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na viongozi wote wa Wizara ya Kilimo. Kwa kweli, Mheshimiwa Waziri ni kiongozi wa mfano, amefanya vyema, lakini bado hujasahau maono ya mtangulizi wake. Yeye ni kiongozi wa kipekee sana. Ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri amefanya kazi kubwa. Sisi tumwahidi, Waheshimiwa Wabunge na Wajumbe wa Kamati, tutaendelea kumpa ushirikiano mkubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mrajisi wa Vyama vya Ushirika, Dkt. Benson Ndiege na Tume yote ya Ushirika, wamefanya kazi kubwa sana kipindi hiki. Wamefufua vyama, wamepeleka fedha nyingi, lakini pia, wamenunua magari karibu mikoa yote na warajisi wote wana magari, kwa ajili ya kuwafikia wakulima. Kwa kweli mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni; ninaendelea kutoa pongezi kubwa sana kwa Benki yetu ya Kilimo (TADB).
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Fedha iliahidi kupeleka fedha zaidi ya shilingi bilioni 100 kila mwaka, kwa ajili ya kuongeza mtaji. Kwa Mwaka 2025 ilipeleka zaidi ya shilingi bilioni 365 moja kwa moja, kwa ajili ya mikopo. Kati ya fedha hizo shilingi bilioni 77.4 fedha hizi zilipelekwa kwenye vyama vya ushirika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakwambia vyama vilivyokuwa vimekufa ikiwemo KAP, CCU, Mbogwe, pamoja na maeneo ya Simiyu ni vyama vilivyokuwa vimekatiwa tamaa, leo vinafanya kazi vizuri. Vimepeleka ushindani mkubwa, leo bei inabadilika na baadhi ya vyama vinalipa malipo ya pili. Ninamwomba Mheshimiwa Waziri, aendelee kupeleka fedha kwenye Benki ya Kilimo, itakuwa mkombozi mkuu wa wakulima, itaendelea kupeleka fedha na kukuza maeneo mengine ya viwanda na kuwakopesha wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapongeza sana Watumishi wa Benki hiyo wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu, ndugu yangu Frank Nyabundege, wamefanya kazi kubwa sana, wameleta mapinduzi makubwa mno katika vyama vya ushirika. Ni kweli, maono ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan hawa wanayatekeleza kwa vitendo, ninawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vipo vyama vingine vya ushirika vinafanya vizuri sana katika kipindi cha Mheshimiwa Rais. Angalia pia, maeneo ya korosho kuna Chama cha Ushirika kinaitwa TANECU, kimejenga kiwanda na kinaendelea kujenga viwanda vingine tisa. Tuna MAMCU, leo wana magari makubwa nane, tuna KNCU wamejenga business centre kubwa. Haya yote ni maono ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ana haki ya kupongezwa mama wa watu, hana maneno, hana makeke, lakini ni Mheshimiwa Rais anayefanya kazi kwa vitendo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, amewainua wakulima, maono ya Mwalimu Nyerere aliyoyasema kwamba, wakulima waundiwe benki yao. Leo tuna benki ya ushirika na imepelekewa mtaji zaidi ya shilingi bilioni 58 inaenda kuwahudumia wakulima na imefungua matawi maeneo mbalimbali hapa nchini, ikiwemo Tabora, kwa kutumia wakulima wa tumbaku. Kwa hiyo, ninaendelea kuomba vyama vya ushirika viendelee kuangaliwa kwa macho ya karibu, vinafanya kazi vizuri kwa sababu, ndiyo vipo karibu na watu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna changamoto kubwa kwenye suala la mbolea, ninaomba na hili wali-note tuendelee kuongeza na ujenzi wa viwanda hapa nchini. Mbolea tunayoitegemea ni inayotoka kwenye nchi za wenzetu, material ya kutengeneza mbolea ni yanayotoka kwenye nchi ambazo leo zinapigana vita; mfano, sasa hivi bei inaweza ikapanda kuliko hata mwaka jana kwa sababu ya vita. Serikali iweke bajeti nzuri ya kujenga viwanda vya mbolea viongezeke, hasa NPK, Urea, KANI na mbolea nyingine ambazo zinapatikana kwa wingi, ambazo wakulima wanazitumia, itatusaidia sana kupunguza gharama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba Mheshimiwa Waziri, tuna changamoto kubwa sana kwenye bei ya tumbaku na yeye mwenyewe ni shahidi. Matrix three ilitengenezwa mwaka huu ambayo ni wastani wa dola 1.95 na bei ya mbolea ambayo imeenda kwa wakulima ilitumia matrix ya mwaka jana ambayo ilikuwa na dola 2.1, ambapo mfuko mmoja wa NPK unapelekwa mpaka kwenye AMCOS dola 56.22.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiweka tozo za benki admin storage ambazo ziko pale mkulima anaenda kukatwa dola 63.89 wakati bei ni dola 1.95. Ni wakati wakulima hawataweza kulipa madeni yao, wakulima hawataweza kumaliza madeni benki. Ninamwomba Waziri, aliyepeleka mbolea ni TFC ni Kampuni ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba Mheshimiwa Waziri, wakae wapitie upya bei za pembejeo, wakae wapitie upya bei ya miji, wakae wapitie upya bei ya magunia na wakae wapitie upya bei za dawa. Mahali ambapo tunaweza kupunguza gharama, wapunguze waweze kuuza, wapate faida, warudi tena shambani. Inawezekana kweli walioweka hizi bei wakapata faida kubwa mwaka huu, lakini wakulima wasiende tena shambani msimu unaokuja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba Waziri suala la bei ya tumbaku na mbolea waliangalie vizuri. Mwaka jana wakati Bunge halijavunjwa, nilishauri, ikiwezekana tuanzishe Mfuko wa Kinga ya Mazao, utatusaidia sana unapofika mtikisiko wa bei. Tuna mazao ya kimkakati, ninampa mfano tu, korosho tumezalisha tani 618,000 lakini pia, tumbaku tumezalisha tani 220,000. Ukienda kwenye pamba, zaidi ya tani 290,000 ukiziweka hizi ukaamua kutengeneza mfuko wa bei ya pembejeo, kinga ya mazao, tunaweza tukatoka hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakupa mfano wa mwisho, korosho peke yake sisi tunaogopa kuweka tozo, lakini taasisi za wenzetu, ma-supplier wenzetu, wanaweka tozo na wanatengeneza faida, lakini sisi tunaona kwamba, tukiweka tozo zinawaangusha wakulima. Kwenye korosho ukiweka shilingi 50 tu, tunakusanya shilingi bilioni 30 kwa mwaka mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye tumbaku ukiweka shilingi 50 unakusanya shilingi bilioni 33, lakini pia, kwenye pamba ukiweka shilingi 50 unakusanya shilingi bilioni 14, kwa mwaka tunapata shilingi 79,180,000,000 tayari hizi fedha tunazipeleka kwenye Benki ya Ushirika, zinakaa pale kusubiri mtikisiko wa bei zetu, zinakaa pale kusubiri mtikisiko wa biashara yetu ya mazao kwa miaka miwili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukisema tutunze, ndani ya miaka mitano tutakuwa na zaidi ya shilingi bilioni 395. Hapa Mheshimiwa Waziri ana uwezo wa kuchukua baadhi ya fedha, anajenga kiwanda cha mbolea, atajenga kwenye Kanda ya Juu Kusini, atajenga Kanda ya Magharibi, atajenga Kanda ya Kati; tutaongeza thamani zao letu la pamba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kwenye tumbaku tuna changamoto ya cotton twine, tuna jute twine ni shida, kuna hessian cloth ni shida. Tunazipata wapi leo nchi za wenzetu kuna vita?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tungekuwa tumekusanya hizi fedha kwa mwaka mmoja, tuna uwezo wa kujenga kiwanda chetu cha kuongeza thamani, pamba tunayo tayari. Kuna vyama ambavyo vinazalisha na kununua pamba tunapeleka kwenye malighafi yetu, tunaongeza malighafi, tunatengeneza faida. Kwa hiyo, ninaomba Wizara wakae, wataalam wapo wanatosha, tena wamebobea, akina Mweli Katibu Mkuu, ninamwamini sana. Watengeneze utaratibu mzuri tuweze kupata fedha, ili tuweze kuhakikisha kwamba, tunaongeza thamani mazao yetu, lakini pia, kuna zao Mheshimiwa analisahau sana na leo hapa nimesoma bajeti yake hajaliandika. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante. Muda wako umekwisha.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakuomba dakika moja tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la maembe. Zao la maembe umeliacha, maembe kwa mwaka tunazalisha tani 400,000 mpaka 500,000 na 30% mpaka 40% yanapotea kwa sababu ya kukosa soko. Hebu ninaomba hili zao waliingize kwenye Mfumo wa Ushirika, liwahudumie wakulima wanaolanguliwa kwa bei ndogo, wanakosa faida. Uzalishaji kwa mwaka…
MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru na ninaunga mkono hoja. (Makofi)