Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Gairo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuwa mmoja wa wachangiaji. Kwa vile dakika ni chache nitaongea kidogo tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kusema tu kwamba, moja ya Wizara ambazo zinategemewa kwenye nchi hii ni kilimo. Kilimo ndiyo kila kitu kwa wananchi wa Tanzania, Wafanyabiashara wa Tanzania na kwa Viongozi wa Tanzania. Ndiyo maana hata ukiangalia mzunguko wetu wa pesa, hasa dola, inakuwa stable wakati watu wanauza korosho, wanauza pamba, wanauza tumbaku, wanauza mazao, utakuta kila kitu kinakaa vizuri. Kama kilimo kisipokuwa vizuri, basi wajue ni matatizo makubwa sana kwenye nchi. Kwa hiyo, nchi hii inategemea sana wakulima wadogo na siyo wakulima wakubwa. Wakulima wadogo wanategemewa sana kuliko kitu cha aina yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namna ya uwezeshaji kwa hawa wakulima wetu tunamwomba sana Mheshimiwa Waziri wetu wa sasa hivi ahakikishe kwamba, uwezeshaji kwa wakulima wadogo unakua mkubwa na ahadi kwa wakulima wadogo zinakuwepo. Ninatoa mfano, tumetoka kwenye uchaguzi mwaka jana, sisi Wabunge ambao tulikuwa humu, kwa mfano kama Gairo, kuna mabwawa ambayo niliahidiwa, Bwawa la Kibedya, Bwawa la Gairo, Bwawa la Chanjale, Visima, Kisitwi, Msingisi, Chiwe, aah no! Wapi panaitwa hapa, Idibo, Chakwale na sehemu nyingine, lakini hakuna hata kitu kimoja kimetekelezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuache, labda Waziri tunaweza tukasema ni mpya, lakini Naibu Waziri ameniona sana ofisini kwake, sana tu. Kila siku tukikutana, tukiongea na watu wa maji, utasikia hiyo bado kidogo, bado hakuna pesa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninaomba, kama ahadi haziwezi kutekelezeka tungekuwa tunakaa kimya maana na sisi kwenye majimbo tunaonekana waongo. Sasa hivi wanasema kwamba, wewe Mbunge kila ukija Bwawa la Malindika, bwawa lenyewe halipo. Kwa hiyo, tunaomba sana, kwa mfano hii nchi sasa hivi vyuo vya kati mpaka vyuo vikuu wanaomaliza ni watu zaidi ya 800,000. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeenda kuanzisha ule mpango wa BBT, lakini nao haujafanya vizuri. Haujafanya vizuri kwa sababu, huwezi kumchukua mtu ukammilikisha ardhi, sijui miaka 66, wakati hata katika ule mpango wa kwanza palikuwa na ekari chache, hata watu 10,000 walikuwa hawafiki wakati vyuoni wanamaliza watu 800,000. Wakimaliza watu 800,000 halafu mpango wote kwa mwaka mzima au kwa miaka miwili ni watu 10,000, kwa hiyo tulikuwa tunaleta nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa hatufanyi vitu vya maana. Tuachane na hivi vitu twende kwenye mashamba darasa, ndiyo maana tunayaita mashamba darasa na yawe kila halmashauri. Kila halmashauri yawepo haya mashamba darasa, hizo pesa ziwe zinakwennda huko kwa sababu, kila halmashauri kuna vijana, wawe wanawezeshwa huko na wawe wanapewa kama kuna shamba la Halmashauri, basi mtu anapewa analima miaka minne, kuna mtandao kuna nini, ukitoka hapo umeshaelewa umuhimu wa kulima na nini, ondoka aje kijana mwingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi hii haizaliwi wala haikui, ardhi tuliyonayo ni ileile. Sasa tukianza kuiwekea mipango mibaya tutakwenda kwa watu wachache halafu vijana wengine watakuwa hawajui tena umuhimu wa kilimo. Tuache hizi habari za kuanzishaanzisha, nimeona hapa kuna hii inaitwa NAESA. Watanzania sasa tumekuwa kiboko kwa kuanzisha hizi agency halafu zinagongana zenyewe kwa zenyewe kazi moja. Tuangalie halmashauri zetu, kwa maana tunaenda tunaanzisha NAESA haya, tumeanzisha TARURA, tumeanzisha maji, zote tumezitoa halmashauri, sasa halmashauri zina kazi gani? Madarasa pekee yake?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuache hivi vitu, lakini tuongeze nguvu ya usimamizi. Kuna vyama vya ushirika, kuna vitu gani, tuongeze nguvu, ili kilimo kile kiendelee kuwa vizuri. Tusipoangalia kwenye hizi BBT tunaanzisha vijiji vya ujamaa vya kisasa. Vijiji vya ujamaa vya zamani vilikuwa nyumba za nyasi, sasa hivi unampa mtu hekari 10 unammilikisha miaka 66, kinachotokea ni nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku akipata kazi TRA na yeye ana elimu ya chuo kikuu ataita pale mjomba, ataita shangazi, ataita nani, watajenga nyumba za bati. Kwa hiyo, watakuja kushangaa wanaanzisha vijiji vya ujamaa vya kisasa badala ya mashamba, huo ndiyo ukweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeongea, ninamshukuru sana Mheshimiwa ni msikivu na tumekubalina kwamba, tutakwenda Gairo akaangalie mabwawa. Nilichimba mabwawa binafsi saba, alikuja Naibu Waziri, wakati ule Mheshimiwa Mavunde, alinisifu sana, hata ukiangalia hapa. Nimetoa mashine za umwagiliaji zaidi ya 400 pale jimboni kwangu, leo hii wanalima, kila siku wanatoa semi trailer tano, nne za mbogamboga na mazao mengine kwenda Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana tukapewa yale mabwawa, lakini hayo mabwawa mpaka leo hayapo. Tunaomba sana Mheshimiwa Waziri atusaidie, atupatie hayo mabwawa. Ninajua ni msikivu na Naibu Waziri wake anamnong’oneza hapo, amwambie ukweli, ninashukuru sana na ninawapongeza. (Makofi)
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, enhe! Lete Taarifa hiyo. (Kicheko)
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa. Hapa, Kingu.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, labda niseme tu.
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tulikuwa tunaomba sana hivi vitu vya…
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa! Of course, ni haki yangu, yes.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Shabiby, endelea.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwa sababu, dakika ulizonipa ni chache, ninashukuru na ninaomba Wizara ya Kilimo ituangalie sana watu wa Gairo kwa sababu, hatupati mbegu za ruzuku, hatupati mbolea ya ruzuku. Inakuja kiujanjaujanja kidogo tu, pale tunatumia samadi tu. Kwa hiyo, watuangalie kwenye haya masuala ya mabwawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)