Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Mbarali
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kupata fursa jioni ya leo kuwa mchangiaji wa kwanza. Nianze kwa kumshukuru sana Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kweli katika Awamu yake ya Sita, wananchi wa Mbarali tumenufaika kwa kupata miradi mingi sana ya kilimo, kwa hiyo tunashukuru sana kwa maono yake mazuri kwenye sekta hii ya kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuwapongeza Waziri, Naibu Waziri na timu yao, kwa hakika hatuna mashaka na wakulima tunayo matumaini makubwa sana na ninyi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo mambo machache ya maombi, lakini na ushauri. Nafahamu Waziri kesho atafanya hitimisho la hoja yake, atakapokuja nimwombe Wanambarali wana kiu ya kusikia. Wakati Rais amepita Mbarali aliwaahidi wakulima wa Mbarali kwamba ameshaanza mazungumzo ya mwekezaji kuachia shamba moja ili wakulima wadogo wa Mbarali, chini ya uangalizi wa Wizara ya Kilimo wapatiwe eneo lile ili waanze kufanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tulitarajia msimu huu unaokwisha, wakulima wadogo wa Mbarali waanze kufanya kazi kwenye shamba hilo. Sasa tutaomba tufahamu ni lini jambo hili litakamilika ili wakulima wadogo wa Mbarali waanze kunufaika na ahadi hii ya Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuishauri Wizara, tunafahamu Tume yetu ya Umwagiliaji inafanya miradi kwenye mashamba ya watu, haina mashamba ya Serikali, inaenda kwenye sehemu ya mashamba ya wananchi, ndiko ambako inafanya miradi. Watakubaliana na mimi Wabunge ambao wana miradi hii ya umwagiliaji, kumekuwa kuna ombwe kubwa la watu ambao wana fedha nyingi kwenda kuyanunua maeneo yale na kuwaacha sasa wakulima wadogo wadogo kutokuwa na maeneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hata juzi, ninadhani mwezi huu nilimshuhudia Mheshimiwa Waziri akiwa Jimboni, pale kwenye Mradi wa Mbarali, Makambako, wananchi walikuwa hawautaki mradi wa umwagiliaji uende pale wakiogopa kuporwa maeneo yao. Sasa tutajikuta miradi hii mikubwa ambayo Serikali inaweka pesa nyingi itakuja kumilikiwa na watu wachache, lakini wakulima wadogo watashindwa ku-manage maeneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri, ninatambua Tume ya Umwagiliaji inayo policy ya namna ya kuangalia sehemu yote, miradi hii mikubwa inamopita, basi maeneo yale yanakuwa chini ya uangalizi wa Tume ya Umwagiliaji, vilevile kuwatambua wakulima wadogo wadogo wa maeneo yale, ili tuwalinde hawa wakulima wadogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, ukienda pale Madibira lile shamba la hekta 3,253 liligawiwa kwa wakulima wadogo wadogo na Serikali imeshawekeza zaidi ya shilingi 8,000,000,000 pale na tuna miradi mingine ambayo ikikamilika ni zaidi ya shilingi 60,000,000,000 Serikali inaenda kuwekeza, lakini wale wakulima wadogo wadogo wote wameshaondolewa. Tutajikuta tunakwenda mbele na watu wachache na kundi kubwa tunaliacha nyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala hili ukiangalia hata watu wa Iringa pale Pawaga, malalamiko ni hayo hayo. Wakulima wetu wadogo lazima walindwe kwa kuwekewa sheria, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri pamoja na kwamba pale nilipokuwa Jimboni aliwasaidia wale wananchi kwa kuhakikisha wanapata hati, lakini haitoshi lazima tuhakikishe hizi policy zinafanya kazi ili wakulima wadogo waweze kulindwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, ni maombi machache, tunafahamu changamoto zilizopo kwenye mfumo wetu wa stakabadhi ghalani, ni kweli hakuna jambo lolote zuri ambalo halina changamoto, lakini tusifikirie kuachana na jambo hili, ila tu tuboreshe tuhakikishe changamoto zinafanyiwa kazi. Tunayo miradi 26 ambayo imejumuisha kwenye mabonde yote ya nchi yetu, miradi ile ni miradi mikubwa na ya kimkakati. Niombe sana Serikali itafute fedha hata nje ya bajeti ili miradi hii mikubwa iweze kukamilika tuwasaidie wakulima wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ninaomba niishauri Serikali, tuwekeze fedha za ruzuku kwenye viwanda vyetu hivi vya ndani ambavyo vinatumia malighafi za ndani kwenye mbolea. Mfano, hawa Minjingu, INTRACOM ili tuweze kuwasaidia na tumeona tunapopata madhara makubwa labda kama Taifa tunashindwa kuagiza vitu nje. Kwa hiyo, hawa ambao wameanza kuwekeza tujitahidi kuweka ruzuku ili kuwasaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni miradi hii ya P4R, tunatambua kwamba miradi hii tayari imeshafanyiwa usanifu na inakwenda kuanza, sasa miradi hii huwa inapishana, Serikali inapotoa pesa. Miradi hii wakati wa mvua na shughuli za kilimo haiwezi kutekelezeka, kwa hiyo tuombe michakato yake ifanyike kwa haraka ili tuweze kuhakikisha mwezi Julai wakati wakulima wameshatoka mashambani, basi waweze kupatiwa nafasi, miradi hiyo itekeleze mpaka mvua zinapokuja msimu ujao tunakuwa tumepiga hatua kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, tunatambua, Wizara hii imebeba msingi mkubwa sana, ajira nyingi sana kwa vijana wetu na kwa Taifa letu. Niombe sana, tunasema tunakwenda kwenye uchumi jumuishi tusiache wakulima wadogo pembeni, tuwalinde wakulima wadogo, maana yake hao ndiyo kichocheo kikubwa cha uchumi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, niombe sana, sheria ziletwe tuwalinde wakulima wadogo, hali ya kwenye miradi huko inayoendelea ya Serikali siyo nzuri, watu wananunua maeneo kwa wingi, unakuta shamba moja wapo watu wawili au watatu na tayari Serikali imewekeza billions of moneys. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, tunamwamini sana, kama wanavyomwamini Wanamakambako na wakulima wa Taifa hili tunamwamini sana kaka yangu Chongolo, nimwombe sana, atusaidie sana na hatuna mashaka naye.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)