Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Urambo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwa kunipa nafasi ili nichangie hoja iliyopo mezani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninamshukuru Mwenyezi Mungu pia ninawashukuru wananchi wa Urambo na familia yangu kwa ushirikiano wanaonipa, lakini kipekee niishukuru Serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan na hasa kwa kutilia mkazo suala la kuinua kilimo chetu Tanzania. Suala kubwa ambalo linatusaidia sisi katika Mkoa wa Tabora kwa upande wa uchumi ni zao la tumbaku ikiwemo Wilaya ya Urambo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumbaku ndiyo inatusaidia kuendeleza hali yetu ya kiuchumi na tulifurahi sana sisi watu wa Tabora tuliposikia kwamba Serikali inatambua sisi ndiyo tunaozalisha zaidi 70% ya tumbaku nchini, wakaona ni vizuri walete Kiwanda cha Mbolea katika Mkoa wa Tabora. Jambo ambalo tunaishi kwa matumaini makubwa, tunajua tutapata sasa mbolea kwa wakati. Ninamwomba Waziri pamoja na kumpongeza yeye na Naibu Waziri na watendaji wote kwa kazi yao, ninamwomba atakapokuwa anahitimisha hotuba yake atuambie je, kiwanda hiki ambacho kinasubiriwa sana na wananchi wa Mkoa wa Tabora, kitaanza kujengwa lini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbolea ni ya muhimu sana, kwa mfano kama sasa hivi tayari watu wameanza kuwa na wasiwasi kama mbolea itafika mwezi Mei, unaokuja mwezi Juni kwa sababu tarehe Mosi Agosti wananchi wanaanza kupanda mbegu, wanapandikiza, tayari wameshaandaa vitalu vyao, tarehe Mosi Agosti wanaanza kuweka mbolea na kupandikiza. Je, mbolea imefika, unawahakikishiaje watu wa Tabora wanaolima tumbaku kwamba mbolea itafika kabla ya mwezi Agosti ili wapande mbegu kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo huo nichukue nafasi hii kuwashukuru kwa kweli hawa wanaonunua tumbaku, kampuni mbalimbali zinazonunua tumbaku, wapo wanaolipa kwa wakati tunashukuru sana, lakini kwa sababu ya muda siwezi kuwataja ila tunawapongeza, lakini wapo ambao bado wakulima wanawadai. Serikali inatuambia nini kuhusu wakulima waliouza tumbaku yao mpaka sasa hawajalipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikutajie madeni waliyonayo, kwa mfano, wakulima ambao wanadai mpaka sasa ni dola 452,513, ushuru ambao unatokana na mauzo bado tunadai dola 329,218, Halmashauri yenyewe inadai 920,000,823. Serikali inatuambia nini, hawa watu watapataje fedha zao na mtu anapolima anategemea kwamba akipata ndiyo ataweza kusomesha watoto na kufanya shughuli zingine za maendeleo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la umwagiliaji na sisi kama Mkoa wa Tabora na mimi kwa upande wangu wa Urambo, tunaomba suala la umwagiliaji na sisi tupate maji ya kuweza kuanza kusaidia kupanda, kwa mfano tumbaku pale kupanda mapema, tunaomba suala la umwagiliaji na sisi lipewe umuhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo siwezi kuacha kulizungumzia ni suala la mbegu ya mahindi. Mahindi pia ni zao mojawapo kubwa sana tunalolitegemea sisi kwa chakula, lakini pia na kwa mauzo. Wananchi wananiuliza mimi huko Urambo, kwamba, hivi Serikali ilivyo na wataalam wa kilimo waliosoma kwa muda mrefu, hawawezi kuja na utaratibu wa kupata mbegu ambayo siyo lazima wanunue kila mwaka. Kila mwaka mkulima ananunua mbegu mpya, je, Serikali inaweza kutuletea utaratibu mwingine ambao mbegu itakuwa nzuri, lakini ambao siyo lazima anunue kila mwaka? Kwa msingi huo tutashukuru sana pia suala hilo atakapolizungumzia Waziri mwenyewe.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo makubwa ni hayo, kwamba kiwanda kijengwe, lakini pia tujue lini kitafunguliwa kitaanza kujengwa, pia kama tulivyosema madai ya wakulima waliouza tumbaku yao, nitashukuru sana kupata majibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimalizie jambo la mwisho, tunaomba inapoletwa mbolea tuwe tunaambiwa ni mbolea gani ambayo imepewa ruzuku, kwa sababu wakati mwingine kunakuwa na mchanganyiko, hujui ni ipi, aina gani ya mbolea ambayo imekuja labda kwa ajili ya tumbaku au mazao mengine, ipi ina ruzuku na ipi haina ruzuku. Waziri atatusaidia sana kwa sababu wakati mwingine kunakuwa na mchanganyiko ambao mtu anashindwa kujua aina ya mbolea ambayo imepewa ruzuku na ambayo haina. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ikifika kama ni ya ruzuku, Mheshimiwa tunaomba wawasogezee wakulima ili wapate karibu na maeneo yao, kwa sababu kipindi kilichopita kupata mbolea ya ruzuku ilibidi wengine wasafiri kwenda sehemu ya mbali na wakati mwingine hata kulala ili aweze kupata mbolea ya ruzuku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaendelea kuwapongeza Wizara kwa kazi kubwa wanayofanya, lakini tunaomba majibu ya kiwanda na mengine kama tulivyoomba kwa niaba ya wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)