Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Yustina Arcadius Rahhi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ya bajeti ya Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya yote ninaomba nimshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa nchi hii kwa jinsi ambavyo moyo wake uko kwenye kilimo na anachangia kilimo kwa jitihada zake zote, ndiyo maana katika zama hizi za Dkt. Samia Suluhu Hassan mpaka yule mkulima wa chini kabisa ameona mkono wake, aidha kwa kununua pembejeo zenye ruzuku, kwa kuona miradi ya umwagiliaji. Hata sasa hivi kawasaidia wakulima kupunguza gharama za kilimo kwa kuwapelekea trekta 360 na sasa hivi zinapelekwa trekta 500, power tiller 200 na kufufua Ward Resource Centres karibu 100, hizi ni habari za Dkt. Samia Suluhu Hassan, tunamshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru pia kwa kutupa Mtendaji mahiri sana, mtoto wa mkulima, Mbunge wa Makambako, Mheshimiwa Daniel Chongolo, moto alioanza nao na kukipenda kilimo na kukibeba, ninawaomba watendaji wa Wizara ya Kilimo, wampeni ushirikiano, huyo ndiye atakayetupelekea ufanisi katika Agenda ya Kilimo 2030. Ninamshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupa kiongozi mahiri sana katika kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa kwanza ninaulekeza katika Jenga Kesho Iliyo Bora - BBT. Haya pia ni maono ya Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa na nia njema ili vijana na wanawake waweze kushiriki katika kilimo na kwa azma kubwa ya kupunguza changamoto ya upungufu wa ajira, hizi ajira milioni tatu ambazo tunazitegemea zipatikane ndani ya Wizara ya Kilimo, zingeweza kupatikana ndani ya mpango wa BBT.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kila jambo likianza linaanza na magumu, lakini sasa tume-refine BBT, ndiyo utaratibu pekee utakaoweza kuwachukua wasomi vijana kujiajiri katika mpango huu. BBT ilitengewa shilingi 16,000,000,000 mpaka sasa hivi fedha zilizopelekwa ni shilingi 6,000,000,000. Mpango wa BBT kwa mfano kwenye shamba la Chinangali, wanatakiwa miundombinu yote iishe ili waweze ku-phase out, watoke sasa kwenye shamba hilo waende kwenye shamba lingine la Ndogoye, lakini washuke kwenye Halmashauri. Kutokukamilisha miundombinu wale vijana kule hawawezi kuendelea na mpango peke yao, ambao wanafanya vizuri wana mashamba, wako kwenye ushirika AMCOS na wanalima kilimo cha contract farming, wako vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishauri Serikali, kwanza mpango huu ushuke Halmashauri, Wakurugenzi wote watafute mashamba, na mashamba haya wayatoe kwa mpango wa kuwakodisha vijana kwa kila mwaka, wanapomaliza waombe tena, kwa sababu ukisema wapate title deed kama ilivyo Chinangali pengine hatuna ardhi ya kutosha, lakini BBT imeenda mbali, kuna BBT ugani ambapo vyuo vya kilimo wanawatoa Maafisa Ugani nao washuke mpaka kwenye Halmashauri, wakafundishe wale kama shamba darasa. BBT siyo lazima iende kwenye kilimo tu, wengine wawepo kwenye usindikaji, kwa namna hiyo, tutatoa ajira za kutosha na BBT itakuwa iko vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu mwingine niuelekeze kwenye pembejeo za kilimo. Msingi mkubwa wa kuongeza tija na uzalishaji katika kilimo ni kuwa na pembejeo bora kwa maana ya mbegu, mbolea pamoja na viuatilifu. Ninaipongeza TARI. TARI wamekuwa wakigundua aina mpya ya mbegu kila mara, kwa mfano kama kipindi hiki wametoa mbegu karibu aina 73 ya mbegu za mazao, lakini vilevile kwa mbegu ya asili wameweza kuchambua, kusafisha na kutunza aina 5,325.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tabia zetu za ulaji sasa hivi watu wamerudi kwenye kutaka mbegu ya asili. Ninaiomba Serikali izalishe hii mbegu ya asili kwenye daraja la kuazimia linaloitwa QDS na iitungie sheria ipitiwe na TOSCI ili mbegu hizi zipatikane kwenye maduka ya wakala, mkulima atachagua kama anataka hizi mbegu za asili azipate akitaka chotara azipate.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaongea kila siku kupambana na GMO, tunapozalisha mbegu zetu wenyewe ndiyo usalama uko hapa, lakini kwa mbegu za chotara ni kweli tumeongeza uzalishaji kutoka tani 79,214 mpaka tani 127,650, zaidi ya 70% tunazalisha wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado mbegu ya mahindi bei yake iko juu, kama pakiti ya kilo mbili inauzwa kwa shilingi 14,000 hadi shilingi 15,000 bado ni gharama kubwa kwa wakulima. Niiombe Serikali iongeze bajeti na kuwasaidia wakulima wa ndani tujitosheleze kwa uzalishaji wa mbegu yetu ya mahindi huku ndani ya nchi. Tuna uwezo, tuna fursa na tuna mazingira ambayo ni very conducive. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hivyo, pengine wakulima sasa wa-graduate kwenye kupewa ruzuku kwenye mbegu ili hizi fedha za ruzuku ziingie kwenye kuzalisha mbegu na mbegu zipatikane kwa gharama ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mbolea, kutokana na mgogoro wa vita ulioko Marekani, Israeli na Iran sasa hivi ni wazi kwamba mbolea zitapanda bei, kwa vyovyote vile. Sasa hata kwa viwanda vinavyozalisha ndani na kuchanganya mbolea bado kuna virutubisho vitatakiwa vitoke nje kwa wenzetu wenye gesi na mafuta. Kwa hiyo Serikali iwe makini, iwasaidie waingizaji wa mbolea sasa hivi. Kama tunavyoweka mikakati kwenye upatikanaji wa mafuta, mbolea zije za kutosha, zipewe ruzuku kabla ya msimu wa mbegu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile niiombe Serikali, wale wasambazaji wa pembejeo walipwe fedha zao ambazo wamekwisha ku-supply ruzuku kwa njia ya pembejeo ili wakulima wasipate shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu mwingine ni kwenye umwagiliaji. Tukitaka kuongeza tija kwenye kilimo ni lazima tuachane na kilimo cha kutegemea mvua; na hapa Serikali iweke kipaumbele kwenye miradi ya umwagiliaji na iweke kipaumbele kwa kutoa fedha kwenye miradi ya umwagiliaji. Kwa mfano, kipindi kilichopita Tume ya Umwagiliaji ilikuwa imeidhinishiwa shilingi 382,138,408,000 lakini mpaka Februari walikuwa wamekwishapewa bilioni 150.6 hii ni sawasawa na 39% au 40. Sasa, kweli tutaleta mapinduzi ya kilimo kwa namna hii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali, hizi fedha hata kama zinavuka mwaka Tume ya Umwagiliaji ipewe fedha ikamilishe miradi viporo. Ninaishauri wakamilishe miradi viporo kabla hawajaanzisha miradi mipya; na waende kwenye skimu za kati na miradi midogo ili ile miradi mikubwa iingie kwenye miradi ya Taifa ya kimkakati kwa sababu fedha zote zinaweza kwenda huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nizungumzie kuhusu ushirika. Ushirika umekuwa na historia mbalimbali katika nchi yetu; kuna wakati ushirika umefanikiwa sana. Tukiangalia Vyama vya Ushirika kama vya KNCU, ACU na sehemu zingine matokeo yake tunayaona. Ushirika umesaidia kusomesha, kupata makazi bora, na kupeleka pembeo. Hata hivyo kuna sehemu ushirika ulifeli na umefeli kwa sababu ya viongozi waliopewa dhamana katika chama cha ushirika husika, ambao hawakuwa waadilifu na wala hawakuwajibika. Ninaiomba Serikali iulinde ushirika kwa namna yoyote; iweke mfumo wa kidigitali katika mali za wanachama na wanachama walipewe kwa muda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushirika una rasilimali nyingi; tuna benki ya ushirika, tuna majengo tuna magari; sasa kwa nini Serikali isifikirie hata kuifanya hii ikawa kanda maalum kukaa na mfumo wa PCCB na Polisi humu ndani ili wananchi warudiwe na kuwa na imani na chama? Hii ni kwa sababu, salamu za wakulima wanasema mtetezi wa mkulima, ni mkulima mwenyewe na mtetezi wa mkulima, ni mkulima mwenyewe ndani ya ushirika. Kwa hiyo, ninaomba Serikali iangalie namna gani ushirika usifeli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wananchi namna pekee ya kupata masoko yaliyo bora ni kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani, lakini mfumo huo umekuwa ukipata migogoro mara kwa mara na unapata migogoro kwa sababu elimu haijatosha kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba elimu ipelekwe kwa wakulima kuhusu namna gani mfumo huu unawasaidia kuondokana na wale walanguzi wa katikati ili mkulima akakutane na bei ile ya mwisho ya mazao yake…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa, ahsante.
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru na ninaunga mkono hoja. (Makofi)