Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DEVOTHA D. MBURARUGABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa nafasi. Nichukue fursa hii kwanza kuwapongeza wafuatao: Ninampongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo anaifanya. Ameonyesha umahiri mkubwa sana, ameonyesha kwamba yeye ni mama ambaye analipeleka Taifa letu mbele. Sisi kama Waheshimiwa Wabunge tunampongeza sana. Nami binafsi nimeiona kazi yake ameonesha kwamba yeye ni kiongozi mchapakazi; tunampongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia nichukue fursa hii kuwashukuru sana wananchi wa Mkoa wa Kagera hususani wanawake, ambao waliweza kuniamini na kunipigia kura za kutosha na kunipa imani yao. Ninawaahidi kuwa nitawafanyia kazi kulingana na uwezo wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichukue fursa hii pia kukishukuru Chama Cha Mapinduzi ambacho kimeweza kuniamini na kupendekeza jina langu mpaka nikawa Mbunge Viti Maalum Mkoa wa Kagera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nielekeze mchango wangu kwenye sekta ya kilimo. Tunafahamu kwamba sekta ya kilimo ni sekta kubwa sana, ni sekta ambayo 70% ya Watanzania wanategemea sekta ya kilimo. Tunafahamu kabisa kwamba sekta ya kilimo inachangia 26% ya pato la Taifa letu. Hivyo ninukuu maneno ya Mheshimiwa Rais, alizungumza bayana kabisa kwamba kilimo ni biashara na mkulima ni mwekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haya matamshi makubwa ambayo aliyatoa Mheshimiwa Rais inabidi tutambue kwamba engine itakayotupeleka kwenye Dira ya 2050 ni sekta ya kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niipongeze Serikali kwa miradi mikubwa sana ambayo imeifanya kupitia viongozi wetu hawa; Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kazi kubwa ambazo wamezifanya. Tumeshuhudia miradi mingi ya umwagiliaji imeanzishwa, tumeshuhudia takribani bilioni 633.4 zimekwenda kwenye pembejeo. Hili ni jambo kubwa sana. Ninaomba tuwapongeze sana sekta ya kilimo kwa sababu wakulima wengi; tunafahamu huko tunapotoka; 70% ya Watanzania wanategemea kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kushauri yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakwenda kwenye Mkoa wa Kagera. Tunafahamu kabisa Mkoa wa Kagera ni mkoa ambao unazalisha kahawa 50% na kahawa hiyo ni aina ya robusta ambayo inapatikana ndani ya Mkoa wa Kagera. Zao hili linachangia pato la Taifa, tunapata fedha kupitia zao hili na inachangia fedha za kigeni ndani ya Tanzania hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze sana Bodi ya Kahawa wakiongozwa na Mkurugenzi wa Kahawa na Mwenyekiti wa Bodi kwa kazi kubwa ambayo wameifanya ndani ya Mkoa wa Kagera. Tumeona wameanzisha utaratibu wa kutoa miche kwa wananchi. Hili jambo ni kubwa sana na nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, kwa sababu wananchi wanao utayari mkubwa sana wanaonyesha jinsi ambavyo wamelipokea jambo hili. Wengi wameandaa mashamba mapya na wanakwenda kuanzisha kilimo ambacho kitaleta tija. Ningependa kushauri yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kagera tuna wakulima wa kutosha. Wakulima wale wamejitolea wamejizatiti kupata miche ya kutosha. Nimeona wamepambana, kwamba bajeti ya kilimo inaelekeza tutakwenda kupata miche ya kahawa. Kilio changu, ninaomba hawa wakulima wapate miche ya kahawa ya kutosha. Kwa nini ninasema hayo, Mkoa wa Kagera unategemea zao la kahawa; na tunafahamu kabisa kwamba kahawa ni moja ya zao ambalo linatumika sana duniani. Tukiwa-support kwa kuwapatia miche ya kutosha tutakuwa tumeinua uchumi wa Mkoa wa Kagera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda pia kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa sababu zao la kahawa lilikuwa lina tozo 45. Hadi sasa tunavyozungumza zao la kahawa lina tozo tano tu. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa sana kuhakikisha wakulima wanapunguziwa tozo. Sasa twende tuwapatie miche ya kutosha, tuhakikishe wanapata miche ya kutosha na tunawapa elimu jinsi ya kupanda ile miche na ukaguzi ufanyike; hapa ninamaanisha accountability.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyo vitalu vya kahawa ambavyo tunaotesha ile miche, lakini bila kuwa na accountability ya kutosha tutakuwa tunapeleka miche hatima yake, wananchi watabaki wanalalamika hawajapata miche ya kutosha. Ninaamini bodi tuliyonayo ya kahawa ni bodi makini, ikiongozwa na mwenyekiti; na wale wote waliopo kwenye Bodi ya Kahawa wako makini sana. Tumemwona Mheshimiwa Waziri wetu wa Kilimo ni mtu mpambanaji anafanya kazi kubwa sana. Kwa hiyo, ninawaamini. Kilio changu, wananchi wa Mkoa wa Kagera wapate miche ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kwamba wananchi kwenda kwenye mstari, wanapanga kuanzia asubuhi, lakini miche haitoshi, siyo zuri. Tuhakikishe miche hii inatosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ningependa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha, hii ni kengele ya pili.
MHE. DEVOTHA D. MBURARUGABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, okay. Ninashukuru sana na ninazidi kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais achape kazi. Mheshimiwa Waziri wa Kilimo tupo pamoja naye. Ninashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru na ninaunga mkono hoja. (Makofi)