Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Handeni Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. CHARLES J. SUNGURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi jioni hii ili kuchangia katika Wizara hii ya Kilimo. Kwanza nitoe pongezi nyingi kwa Wizara na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo ndugu yangu Mheshimiwa Chongolo kwa wasilisho zuri. Ninaomba nianze kusema kwamba ninaunga mkono hoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipo hapa kwa ajili ya kuwakilisha Jimbo la Handeni. Jimbo la Handeni ni wakulima wakubwa sana wa zao la mahindi, tunalima sana mahindi na tunategemea sana mahindi katika kilimo, lakini pia katika biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka wananchi wa Jimbo la Handeni wanalima tani takribani 120,000 mpaka 150,000; na kwa wastani wananchi hawa wanatoa gunia tano mpaka nane kwa hekari moja. Ukiangalia Jimbo la Handeni lina wastani wa hekta 600,000 mpaka 700,000, ambazo ndizo zinazowezekana kufanyika kilimo cha mahindi. Hata hivyo, kwa masikitiko makubwa wananchi hawa wanalima hekta 60,000 mpaka 80,000 tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kwa sababu uwekezaji bado ni mdogo katika ulimaji wa mahindi Jimbo la Handeni. Takribani 85% ya vijana ndiyo wanaolima mahindi, lakini wanalima katika mazingira magumu sana. Hawana pembejeo za kutosha, hawana viuatilifu, hawana mbolea na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niiombe Wizara ihakikishe kwamba inaongeza jitihada kubwa sana kwa wananchi hawa ili waweze kulima mahindi kwa tija kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Handeni pia linaweza kustawi korosho, ufuta pamoja na mbaazi. Ninashangaa pia Wizara kwamba bado imeweka jitihada ndogo sana kuhakikisha kwamba mazao haya yanakuwa improved katika Jimbo la Handeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana tumepewa takribani miche 17,500 ya korosho; lakini ukifananisha na wenzetu wa Kusini wamepewa miche takribani 4,220,000 ndani ya mwaka mmoja. Kwa hiyo utaona kwamba bado uwekezaji ni mdogo sana katika Jimbo la Handeni na katika Wilaya ya Handeni na Mkoa wa Tanga kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana tumevuna tani 97.5 tu za korosho. Kwa hiyo unaona kwamba bado uwekezaji huu ni mdogo sana; na zao la korosho ni zao muhimu sana kwa wananchi wa Handeni, kwa sababu kutegemea mahindi kama zao la biashara bado haina tija sana kwa wananchi wangu wa Jimbo la Handeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia tabia ya nchi au ecological characteristics za Jimbo la Handeni na Mkoa wa Lindi vinafanana. Kwa mfano PH Jimbo la Handeni tuna PH ya ardhi 4.5 mpaka 6.5, ni sawasawa na Mikoa ya Kusini. Joto ni 20-30 degree centigrade ambazo ni sawasawa na Mikoa ya Lindi. Altitude from sea level kule tuna 400 hadi 700, ni sawasawa na mikoa inayolima korosho. Ukiangalia udongo navyo vinafanana, kwa hiyo sioni sababu ni kwa nini Wizara haiweki mkazo katika zao la korosho kwenye Jimbo la Handeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana Wizara hii watakapotoka hapa wanapokuja kwenye majumuisho yao waje na mkakati wa namna ya kubadilisha Jimbo la Handeni liweze kulima zao la korosho, zao la ufuta lakini pamoja na mbaazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwananchi wa Jimbo la Handeni akitaka kununua bati 30 ili ajenge kibanda chake inamlazimu lazima aandae shilingi 750,000. Fedha hizi ni lazima auze gunia 15 za mahindi, ni sawasawa na amelima eka tatu ili aweze kununua bati 30 tu za gauge 30. Ukimfananisha mwananchi huyu huyu wa Mikoa ya Kusini wanaolima korosho, yeye atahitaji miti 30 tu ya korosho kupata 750,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninadhani unaona ni namna gani zao hili ni muhimu sana kwa Jimbo langu la Handeni. Hii itasaidia sana wananchi wale waweze kubadilika kiuchumi kwa sababu nguvu wanazo, lakini tunahitaji tu kuwa-boost kidogo kutoka katika Wizara yake ya Kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia upande wa machungwa. Sisi ni wakulima wazuri sana wa machungwa, lakini bado machungwa yale hayana thamani stahiki. Wanatumia sana madalali ambao wanaenda shambani watanunua shilingi nane hadi shilingi 10, lakini chungwa inapaswa kuuzwa shilingi 50 mpaka shilingi 100. Kwa hiyo niiombe Wizara kupitia taasisi ya mazao mchanganyiko (COPRA) watuletee cold rooms ili wale wananchi waweze kuhifadhi machungwa yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sitamani kuona chungwa liuzwe katika msimu mmoja. Ninatamani kuona chungwa liuzwe ndani ya mwaka mzima; Januari, Februari, Machi hadi Disemba wananchi waweze kuuza machungwa yao kulingana na soko linavyoenda. Kwa hiyo niwaombe tafadhali sana Wizara watuletee cold rooms katika maeneo yale ya Handeni ili tuweze kuhifadhi machungwa yetu na tuyauze kwa bei nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, takribani 40% ya machungwa yote yanaharibika shambani; kwa kweli ni kuwa unfair sana kwa wakulima hawa. Kwa hiyo, mwisho kabisa niwasisitize tena, cold rooms ni muhimu sana katika Jimbo la Handeni. Ikishindikana cold rooms, basi watuletee viwanda vya kusindika machungwa ili tuongeze thamani ya zao hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)