Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Cosmas Mtesigwa Bulala

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. COSMAS M. BULALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa fursa hii adhimu ya kuleta mchango wangu kwenye hotuba ya bajeti ya Wizara ya Kilimo iliyoletwa mbele ya Bunge letu Tukufu na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo. Nimpongeze Waziri wa Kilimo kwa bajeti nzuri yenye kuleta matumaini, lakini pia yenye kutoa dira njema kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutupatia uhai na afya njema na kutuwezesha kusimama hapa katika Bunge hili Tukufu siku hii ya leo. Pia nitumie fursa hii kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Kwimba kwa kuniamini na kunichagua kwa kura nyingi sana kuja kuwa mwakilishi wao hapa Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta mapinduzi makubwa kwenye kilimo. Hii inaonyesha maana halisi kwamba kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa letu na Mheshimiwa Rais Samia amekuwa kinara katika kuliendeleza hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2021 wakati Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anakuwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bajeti ya Wizara ya Kilimo ilikuwa shilingi bilioni 294, lakini leo hii miaka mitano baadaye tunazungumzia bajeti ya trilioni 1.2. Hii ni ishara kwamba Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni daktari bingwa wa matatizo ya wakulima wa nchi hii ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, sasa nijielekeze kushauri mambo machache katika presentation ya Waziri wetu wa Kilimo ambayo ninahisi yataweza kusaidia ukuaji wa sekta yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo ni sayansi na sayansi yoyote huwa inaendeshwa na tafiti. Nitumie fursa hii kumwambia Mheshimiwa Waziri wa Kilimo tuna haja ya kuongeza bajeti yetu kwenye eneo la utafiti. Sisi kama nchi tumejiwekea malengo makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Dira yetu ya Mwaka 2050 tume-project kwamba kipato cha mtu mmoja mmoja kiwe dola za kimarekani 7,000. Hili ni lengo kubwa sana. Pia, Wizara ya Kilimo imesema kwamba thamani ya biashara ya kilimo au thamani ya sekta ya kilimo kufikia mwaka 2050 iwe ni shilingi 100,000,000,000. Haya ni malengo makubwa ambayo ni mara tano ya thamani ya sasa. Mheshimiwa Waziri ili tufikie malengo haya tunahitaji kuwekeza katika utafiti na hasa utafiti wa mbegu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nikisema hivi simaanishi kwamba Wizara haijatenga bajeti ya kutosha kwenye utafiti, lakini tukiangalia bajeti ya mwaka jana kwa mfano, pesa iliyowekwa kwenye utafiti ilikuwa ni chini ya asilimia moja. Hii ni kinyume na lile Azimio la Umoja wa Mataifa la Malabo linalosema kwamba ili tuondokane na umaskini tunatakiwa kuweka angalau asilimia moja ya bajeti yetu ya kilimo kwenye utafiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiacha mbegu za mahindi ambazo ASA ambayo ni Taasisi yetu ya Mbegu ya Serikali na wazalishaji binafsi wanazalisha kwa wingi, leo hii ukihitaji mbegu za mazao mengine, kwa mfano ukienda pale TARI Uyole ukataka mbegu au TARI Ilonga ukataka mbegu ya Mbaazi huwezi hata kupata tani 30.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ukienda hata TARI ya pale kwetu Ukiriguru ukawaambie wakupatie mbegu mama ya Dengu hawawezi kukupatia hata tani 20. Tulikuwa na progamu pale Kwimba, tumeanzisha programu tunaiita Ekari ya Mbunge ambapo tumegawa mbegu za Dengu tani 700 kwa kaya zaidi ya 20,000 za wananchi wa Jimbo la Kwimba. Tulipata tabu sana kupata mbegu na matokeo yake tuliamua tu kutafuta mbegu ambazo ni improved tukazi-grade hatukuzipata kwenye Taasisi ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nitoe wito kwa Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atuambie mkakati wake ni upi kwenye kuongeza bajeti ya utafiti hasa kwenye eneo hili la mbegu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbegu sio tu suala la kutufanya tupate tija katika uzalishaji, lakini mbegu pia ni suala la usalama wa Taifa. Mtu akitaka kucheza na sisi kwenye mambo ya usalama wa chakula anacheza na sisi kwenye mbegu. Kwa hiyo tuweke jitihada nyingi kuwekeza kwenye eneo la mbegu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anaweza kuwa ana-wonder atapata wapi pesa ya kuendesha na kuongeza bajeti ya utafiti, nitoe ushauri kwa Mheshimiwa Waziri. Kuna mashirika kwenye Wizara ya Kilimo, Shirika kama CPB (Cereal and Other Produce Board) inafanya biashara ya mazao yaani kununua na kuuza mazao kwa wakulima. Kuna shirika kama hilo TFC (Tanzania Fertilizer Company), umeweka mtaji wa shilingi bilioni 118 kwenye Kampuni ya Mbolea Tanzania, lakini leo hii ile kampuni inafanya turnover ya shilingi 300,000,000,000, this is a joke!

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kuwekeza pesa nyingi namna ile kwenye kampuni ya Serikali kwa ajili ya kufanya kazi ambayo inaweza kufanywa na sekta binafsi. Leo hii TFC inaenda kushindana na kampuni kama ITRACOM, ETG (kampuni binafsi). Kwa nini tusiache hii kazi kwa kampuni binafsi zilizowekeza mitaji yao hapa na TFC ifutwe. Tunaomba Waziri alete hoja kwenye Kamati yetu ya Mitaji ya Uwekezaji wa Umma na sisi tutambariki kampuni hii ifutwe, pesa hii iende kuwekezwa kwenye TARI tuweze kuboresha utafiti wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia niongelee eneo la umwagiliaji. Nchi yetu tumejaliwa. Eneo linalofaa kwa umwagiliaji tuna hekta milioni 29, lakini mpaka sasa tunachotumia ni chini ya asilimia tano kwenye umwagiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kuendelea ku-fund miradi ya umwagiliaji kwa kutumia ukomo wa bajeti ya Wizara ya Kilimo. Ninapendekeza miradi ya umwagiliaji kwanza isiwe social, isiwe miradi ya kijamii, iwe ni business undertaking.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuitafutie ufadhili nje ya bajeti ya ukomo wa bajeti ya Wizara ya Kilimo. Mheshimiwa Waziri ametuletea presentation hapa kwenye bajeti yaeo kwamba tuna miradi ya mabonde 26 ya umwagiliaji ambapo tayari Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imeshafanya feasibility na wanatafuta fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mradi mkubwa wa umwagiliaji tunaouandaa wa maji ya Ziwa Victoria na maji ya Ziwa Tanganyika. Miradi hii miwili thamani yake ni zaidi ya trilioni sita. Hatuwezi kuendelea kuipatia pesa kupitia ukomo wa bajeti ya Wizara ya Kilimo. Ninamshauri Mheshimiwa Waziri atafute namna bajeti ya umwagiliaji ijitegemee na tutafute fedha za kui-fund miradi hii kama tulivyotafuta fedha kwenye ku-fund Daraja la Kigongo - Busisi au tulivyofanya Mradi wa Mwalimu Nyerere au tulivyofanya Mradi wa SGR. Mheshimiwa Waziri tutafanikiwa sana na tutafikia malengo katika umwagiliaji. (makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalize kwa kuzungumzia mifumo ya masoko ya mazao ya wakulima wetu. Ninatoka Jimbo la Kwimba. Kwenye Jimbo la Kwimba sisi ni wakulima wa mazao ya mikunde, mpunga, mahindi na alizeti. Wakati tunalima huwa hatuoni taasisi zozote zikija kwenye maeneo yetu. Huwa hatuoni COPRA, TMX, AMCOS, hatuoni zote…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante kwa mchango wako.

MHE. COSMAS M. BULALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe kutoa ushauri kwa Mheshimiwa Waziri, tumeanza taasisi yetu nzuri sana ya COPRA ili iweze...

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha.

MHE. COSMAS M. BULALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru na ninaunga mkono hoja. (Makofi)