Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Khadija Hassan Aboud

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa nafasi. Kwanza kabisa ninapenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza Wizara ya Kilimo kuanzia Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa kilimo kwa juhudi mbalimbali wanazofanya katika kuhakikisha sekta hizi za kilimo zinafanya kazi kwa manufaa ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoomba kuongezewa bajeti kwenye sekta za uzalishaji ikiwemo Wizara hii ya Kilimo, tumeona mafanikio makubwa yamepatikana katika kuongeza fedha hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii imefanya mambo mengi kupitia bajeti yetu ya kilimo ikiwemo kuimarisha TOSCI, kuimarisha ASA na kuimarisha TARI. Tuna maabara za kisasa ambazo kwa sasa tutatoa ithibati ya mbegu ambazo tutaweza kupeleka mpaka nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mafanikio hayo yameongeza huduma za ugani kuwapa vitendea kazi vilivyo bora na vya kisasa pamoja na kuongezea elimu ya kutosha kukabiliana na changamoto mbalimbali za kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Wizara yetu hii ya Kilimo iendelee kuongezewa bajeti kwa maana ya kwamba yale matarajio ya Mheshimiwa Rais ili yaweze kufikiwa. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuliona hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ambazo zimejitokeza kwenye taasisi yetu hii ya BBT zitaweza kutatuliwa tu ambapo bajeti ya kilimo itakuwa ya kutosha na inatoka kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nia ya Mheshimiwa Rais ni kuhakikisha vijana wa nchi hii wanapata ajira na kujiajiri na kupata kipato. Tukiongeza bajeti na fedha zikatoka kwa wakati mambo mbalimbali changamoto ya huduma za ugani zitaweza kutatuliwa na kuwafikia wananchi na wakulima kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea pamoja na hali nzuri ya sasa hivi kwenye kilimo imeonekana kwamba mazao ya kilimo yamezalishwa kwa wingi kwa wakulima wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajielekeza kwenye sehemu hii muhimu sana ambayo ni silaha kubwa kwa mkulima na kwa Taifa mbolea. Lazima tujihakikishie tuna mbolea ya kutosha katika maghala yetu ili changamoto hii ikijitokeza tuweze kukabiliana nayo hata kwa miaka miwili mpaka mitatu kutokana na changamoto za kidunia zilizoko hivi sasa ambazo kila mtu anazitambua ikiwemo kuwekeza viwanda vya ndani vya mbolea vidogo na vya kati kwa wananchi wazalendo wa Taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini kuna wawekezaji wazalendo kwenye sekta za saruji na sekta za mabati, isiwezekane kwenye mbolea wakati malighafi zimo ndani ya nchi na tunaweza. Njia tu ya Serikali kuwawezesha hawa namna bora ya kuwapatia mitaji ikiwa kwenye mikopo kwenye benki zetu ili na wao waweze kuwekeza kwenye sekta hii ya mbolea ambazo tuweze kujitosheleza wenyewe ndani ya nchi tuwe na uhakika na usalama wa mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninajielekeza kwenye umwagiliaji. Ninarudia tena kuhakikisha kuishauri Serikali uwekezaji mkubwa wa fedha kwenye sekta hizi za kilimo kutasaidia kilimo cha umwagiliaji. Yale mabwawa makubwa ya kimkakati yatafutiwe fungu maalum, fungu mahususi kwa ajili ya miradi ile mikubwa ya umwagiliaji ili tuweze kukidhi kilimo cha Mtanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea tujitahidi kulipa wakandarasi wa umwagiliaji ili ile miradi iliyosimama iweze kufunguka na tupate tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajielekeza tena kwenye mbegu za asili. Tuna mbegu zetu za asili ambazo zina virutubisho vya kutosha. Sasa hivi kuna watafiti vijana wetu wamegundua mbegu za asili, virutubisho vya asili, mbolea za asili, viuatilifu vya asili. Ni sasa Serikali iwaone hawa vijana kuwawezesha ili waweze kuzalisha kwa wingi ili mkulima aamue anatumia mbegu za aina gani na kilimo cha aina gani kikiwemo kilimo ikolojia, kilimo hai ili kuweka hali ya afya zetu kwa mazao tunayozalisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado hakuna sheria maalumu iliyowekwa kwa ajili ya mbegu hizi za asili ambazo zitatunza rasilimali hii na urithi huu wa Taifa tulioupata enzi na enzi. Tunataka mbegu za asili zipate ithibati ya kutumika rasmi ziingie kwenye mfumo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ifike wakati mkulima na mlaji aamue anakula mazao ya aina gani? Ya kupitia viwanda mambo ya hivi viuatilifu na mbolea za viwandani au mbegu za asili na uzalishaji wake wa asili kuanzia tangu kwenye udongo mpaka kufika kupata mazao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliposema kuongeza bajeti kumesaidia sana sekta hii ya kilimo. Mpaka mwezi Machi Wizara imesomesha shahada ya uzamili 43 na uzamivu 23. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashauri wale wataalam wetu wabobezi wa utafiti wa fani mbalimbali kwenye kilimo, maslahi yao yaangaliwe vizuri na watakapofika muda wa kustaafu wasiondoke watafutiwe njia ya kubaki ili waendelee kutusaidia. Kwa sababu inaonekana kwamba wanapomaliza muda wao wanabaki, wakibaki wanachukuliwa na nchi jirani wanakwenda kufanya utafiti wanazalisha mbegu na mbegu zile zile tunakuja kuuziwa tena ndani ya nchi. Hii ni rasilimali kubwa. Wataalam wetu wabobezi lazima tuwalinde na tuwatambue. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Tunakushukuru kwa mchango wako.

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendelea kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anavyozijali na kuthamini sekta zote za uzalishaji, anavyowajali wakulima na wananchi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na ninaunga mkono hoja. (Makofi)