Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Dr. Yahaya Esmail Nawanda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyumbu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. DKT. YAHYA E. NAWANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia nichukue nafasi hii kumwambia kaka yangu Chongolo sasa ashike peni, nimpe elimu ya korosho kwa dakika saba, halafu niende zangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la korosho katika Mkoa wa Lindi na Mtwara zaidi ya 85% inazalishwa na wananchi wa Mkoa wa Lindi na Mtwara. Mikoa ya Mtwara na Lindi ina jumla ya wakulima 462,803 na jumla kuu ya wakulima wote nchi nzima ni 549,936. Hoja ya msingi inakuja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mtwara na Lindi ndiyo vinara wa uzalishaji wa korosho nchini. Hoja yangu kubwa hapa leo nitachangia kuhusu bima ya afya. Chongolo kaka yangu katika jambo kubwa ambalo atatusaidia wananchi wa Mtwara na Lindi hususan wanaolima korosho na tukumbuke na zahanati zetu zote tuweke sanamu yake twende na bima ya afya kwa kila mkulima wa korosho na hesabu iko ifuatavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika zao la korosho mjengeko wa tozo kuna jumla ya fedha shilingi 469. Ushuru shilingi 59, uhifadhi wa korosho, magunia na kila kitu. Leo ninataka nijikite hapa ukisema kwa makisio ya mwaka huu 2026/2027, tunategemea kuzalisha tani 750,000 sawa sawa na kilo milioni 750. Sasa Chongolo kaka yangu katika hizi tozo zote ambazo ni shilingi 469, hapa ninaomba tu tufanye hesabu kidogo, tutoe shilingi tano tano kwa kila mtu hapa na kwa sababu wengine hawa tumekuwa tunawachangia lakini mambo mengine wala hatuyaoni, sasa tukiamua kuchukua hizi fedha tukarudisha kuwapa bima wananchi wote wanaozalisha korosho inawezekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawezaje? Twende tukisema kwa makisio ya korosho kilo milioni 750 tukisema tutoe tu shilingi 15 kwenye kila kilo moja tutaenda kutengeneza jumla ya bilioni 11.25 hizi bilioni 11.25 tunaweza kuwahudumia wananchi 75,000 lakini kwenye kitita cha afya ya msingi ambacho mwananchi anaenda kulipa shilingi 150,000 hapa ukijumlisha au ukizidisha mara sita jumla ya wananchi 450,000 wanaenda kunufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukisema tunatoa tu shilingi 15 maana yake Lindi yenyewe ina jumla ya population ya wananchi 1,192,000. Kwa hiyo unaweza kusema tukiweza kuwapa bima ya afya wananchi 450,000 maana yake nusu ya watu wote wa Lindi wanaenda kupata huduma ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo kubwa sana na hapa nimekupa mfano wa Lindi pekee yake. Kwa hiyo, tukiweka na Mtwara tukisema tuweke shilingi 20 tunaenda kuongeza na kupata fedha bilioni 15 ambayo itasaidia wakulima 100,000 tukizidisha mara sita maana yake ni 600,000. Maana yake wakulima wa Lindi na Mtwara 50% ya wananchi wote wanaenda kupata bima ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukisema tuweke shilingi 30 tu Chongolo kaka yangu tunaenda kuongeza au tutapata bilioni 22.5, shilingi bilioni 22 ni sawasawa na wakulima 150,000, ukizidisha mara sita unaenda kupata wakulima 900,000. Wakulima 900,000 ukizidisha mara sita watu wote tunaenda kuhakikisha wananchi wa Lindi na Mtwara wanaenda kupata bima ya afya. Ukisema sasa umalize kabisa chukua shilingi 40 na huu katika mjengeko hatuongezi hata shilingi moja kwa mkulima. Tunachofanya ni kupunguza tozo ambazo tayari tunazo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiweka shilingi 40 tunaenda kupata shilingi 30,000,000,000 ambayo jumla ya wananchi 1,200,000 wanaenda kunufaika. Kwa hiyo, hapo hatujamwingilia dada yetu katika zao lake la COPRA, dada yetu Irene, sisi tumejikita kwenye korosho peke yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda kwa Irene dada yetu wa COPRA anaweza kutupa jumla ya wakulima, tukiweka kwenye hesabu hiyo kwa sababu ya projection yake ni kilo 98,000,000 za ufuta, pekee yake tunaenda kusaidia wakulima 58,000 wa Mkoa wa Lindi na Mtwara. Hii ni idadi kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninachomwomba Mheshimiwa Waziri aje na mkakati wa kuhakikisha sasa tuweze kuwasaidia wananchi wa Mkoa wa Lindi na Mtwara, tuwape bima ya afya bure na inawezekana ndiyo ndoto ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Hapa nimempa hesabu na inawezekana. Kwa hiyo Waziru anapokuja kwenye majumuisho aje atuambie sasa tumekubaliana tutakwenda kuendeleza jambo hili zuri la Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa wananchi wa Mkoa wa Lindi na Mtwara. Kwa kufanya hivyo atawasaidia hawa wananchi na hatutamsahau na namhakikishia tutamjengea sanamu katika zahanati zetu zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine na la msingi ambalo pia ningependa kuchangia ni kuhusu suala la korosho. Korosho tunapopeleka ghalani tumekubaliana mikoa yote inayolima korosho; minada inafanyika siku ya Ijumaa. Siku ya Ijumaa ikifanyika minada watu wote hatutaki korosho hela siku hiyo. Ijumaa sisi hatutaki fedha zetu, Jumamosi hatutaki fedha zetu, Jumapili hatutaki fedha zetu lakini Jumatatu na Jumanne tunataka fedha zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna minada ilifanyika ilichukua zaidi ya miezi miwili bila kulipa fedha. Sasa Mheshimiwa Chongolo akija hapa aje na majawabu hayo, majawabu makubwa ya bima ya afya, lakini pia kero ya wananchi kukaa muda mrefu bila kulipwa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuseme ukweli COPRA inafanya kazi mzuri sana kwenye ufuta, kwenye mbaazi na kwenye mazao mengine na kwa sababu dada Irene ana miaka miwili tu, bado ni mchanga, ninafikiri baada ya miaka mitano na yeye atakuwa mbobezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)