Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja ya Wizara ya Kilimo. Mwaka 2003 Wakuu wa Nchi za Afrika walikutana kule Maputo, Msumbiji na wakapitisha azimio kwamba bajeti ya kilimo ifikie 10% ya bajeti za Taifa na ikawa ni azimio la nchi zote za Afrika, lakini hapo mpaka leo, hakuna nchi iliyowahi kufikisha 10% ya bajeti ya kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kusema, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, yeye amethubutu na amefanya vizuri. Kwa sababu bajeti sisi sote tunajua, ilikuwa ni chini ya shilingi bilioni 240, yeye ameongeza zaidi ya mara sita, karibu imefika shilingi trilioni 1.1. Kwa hiyo yeye amefanya vizuri na tuna kila sababu ya kumpongeza kwa hatua alizochukua na maono hayo makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia, Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote waliopo kwenye Wizara ya Kilimo kwa kazi nzuri waliyoifanya, lakini pia kwa bajeti nzuri waliyotuletea. Ninawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapongeza Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ambayo imefanya kazi ya kuchambua bajeti hii. Wametushauri tupitishe hii bajeti, nami ninaungana nao, tuipitishe hii bajeti ili twende tukatende sasa, tupate manufaa makubwa ya Wizara yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo kimekuwa na majina mengi, toka miaka nenda rudi. Tulianza tukaiita “kilimo ni uti wa mgongo, siasa ni kilimo, kilimo kwanza, programu ya kuendeleza kilimo”, kimekuwa na majina mengi. Kwa nini kimekuwa na majina mengi? Kwa sababu ya umuhimu wa kilimo katika Taifa letu. Ndiyo maana tumekuwa na kila aina ya sera ambazo zimekuwa ziki-promote kilimo chetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, kwa nini iko hivyo? Iko hivyo kwa sababu, kilimo kinaajiri karibu takribani 55% ya Watanzania ambao wako kwenye kilimo. Wameajiriwa huko, wanakula maisha yao kwenye eneo hilo. Kwa hiyo, kilimo ni muhimu sana, lakini kilimo kinatoa 66% ya malighafi zote zinazotakiwa kwenye viwanda. Kwa hiyo, kilimo ni viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, la tatu, kilimo ni biashara kwa sababu fedha za kigeni zaidi ya 30%, tunapata kutoka kwenye kilimo. La nne, kilimo ni chakula, zaidi ya 100% tunapata chakula kwenye kilimo. Tanzania tunajitosheleza kwa chakula. Kilimo hiki ndiyo kinatuwezesha sisi kusema leo hapa, kwa sababu tumekula, tumeshiba kwa kazi nzuri iliyofanywa na kilimo, bila kilimo hatuwezi hata kusema. Mwaka huu pia tumeambiwa, kilimo kimechangia 24.6% kwenye pato la Taifa. Kwa hiyo kilimo ni uchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kutokana na hiyo, mambo haya ni muhimu sana na kwa sababu kilimo kina umuhimu katika maendeleo ya Taifa letu, tunahitaji mambo kadhaa yafanyiwe kazi na yaendelee kufanyiwa kazi. Ninajua wameshaanza kuyafanyia kazi na wameyafanyia kazi kwa kiwango kikubwa. Hata hivyo, ninataka nikumbushe, ardhi ya kilimo imekuwa ikipungua mwaka hadi mwaka. Sasa hivi ardhi ya kilimo inavamiwa kila mahali, kwa hiyo, kuna haja ya kuja na sheria ya kuilinda ardhi ya kilimo, ili hili ongezeko la watu lisije likamaliza ardhi, tukashindwa kupata chakula cha kututosheleza na kufanya biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, wakulima hawa wanapambana na changamoto nyingi. Ikiwemo ukame, yakiwemo magonjwa mbalimbali ya mazao yao, mafuriko, wanarudi na kuwa katika hali mbaya. Unakuta mkulima aliwekeza vizuri, lakini kutokana na hivyo, anakuja kurudi nyuma. Hivyo basi, suala la Bima ya Mazao kwa sasa hivi kwa ulimwengu wa leo, ni muhimu sana Wizara ilitilie mkazo, iendelee kutekeleza Bima ya Mazao ili mazao yetu mengi yawe na bima, tuwakinge wakulima wetu ili wasikumbane na haya majanga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, wamempongeza Waziri nimesikia amesema wakulima waliosajiliwa sasa hivi ni milioni tano na kitu, lakini ninaamini ni zaidi na amesema anaendelea na usajili. Sasa ninataka kusema, ni vizuri tukaendeleza tukaweka nguvu zaidi kwenye kuwasajili wakulima, ili tuwatambue ili tuweze kuwahudumia. Kwa sababu kama hatuwajui, hatuwezi kuwahudumia ipasavyo, kwa hiyo, tuwasajili wote, tujue wako wangapi, wanatoa nini, wanafanya nini, wanachangia nini. Hiyo itatusaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la nne, iko haja sasa nchi yetu kutoka, kuuza mazao badala ya kuuza kama malighafi sasa, tuanze kuongeza thamani ya hayo mazao. Tujenge viwanda vya kuongeza mazao. Tulikuwa na ASDP II ile ambayo mkazo ulikuwa ni kuongeza thamani ya mazao yetu. Ni muhimu sasa hii programu tukaendelea nayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, tunayo mazao yetu mengi na Tanzania ilisikika miaka ya nyuma kwamba ina mazao mengi, tulikuwa na mkonge tunaongoza, lakini sasa hivi hakuna zao ambalo Tanzania inaongoza kwa uzalishaji duniani, wala katika Afrika. Sasa ipo haja, kama korosho tunaona inalipa, tuwekeze zaidi kule, lakini kahawa inalipa, tuwekeze zaidi kule ili wananchi wengi wakalime, tukazalishe tuwe ni nchi ya mfano katika mazao. Tuchague mazao machache, iwe ni mfano na tuweze kuzalisha kwa kiwango kikubwa na kwa tija zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wana-Songwe sisi, tunahitaji ujenzi wa Soko la Kimataifa la Mazao, ili wote wanaohitaji, waje kununua mazao. Sisi ni wakulima, ni wazalishaji wakubwa, watuletee soko pale, mambo yatakwenda vizuri. Tunahitaji kuongeza kilimo cha kahawa, tunataka watuongezee miche ya kahawai li tuongeze uzalishaji wakati huu ambapo bei zimekuwa nzuri. Wakulima wengi wanataka kwenda kulima zaidi, yaani kupanua mashamba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sasa mbegu zile, ile miche ya kahawa ipatikane kwa wakati, lakini pia mbegu za mazao ya kilimo zilizo bora zipatikane, zitatusaidia sana katika kuboresha maisha yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upatikanaji wa mbolea, upatikanaji wa madawa, upatikanaji wa mbegu kwa wakati, ni muhimu sana. Itatusaidia sana katika kuimarisha kilimo chetu. Bei ya kahawa sasa hivi na mahindi ni nzuri, lakini tunataka Mheshimiwa Waziri atakavyokuja kuhitimisha bei ya mahindi itakuwaje mwaka huu? Uzalishaji kwetu kule mwaka huu ni mkubwa kweli kweli kwenye mahindi. Tunahitaji sasa masoko, lakini pia tunataka kuwekeza zaidi kwenye mbogamboga na matunda, kwa hiyo sasa watutafutie soko ili tuweze kuuza. Tunahitaji mashamba ya umwagiliaji yaweze kutusaidia zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuongeza tija, tunahitaji mbegu zilizo bora; tunahitaji madawa yaliyo mazuri; tunahitaji mbolea zilizo nzuri. Mwaka jana katika maeneo mengi, katika baadhi ya kata, tulipata changamoto ya kupata mbolea na mbegu zisizofaa. Ninamwomba Mheshimiwa Waziri, akalitazame, wakasimamieni watuletee mbegu nzuri, watuletee mbolea nzuri itatusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuhitimisha, kilimo ni ajira, kilimo ni viwanda, kilimo ni chakula, kilimo ni uchumi, kilimo ni biashara. Uchumi wetu utapanda, utakua na utakuwa imara kwa kutegemea mchango wa sekta ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mungu akubariki na ninashukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)