Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Ado Shaibu Ado

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Tunduru Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili niweze kutoa maoni yangu katika Bajeti hii ya Kilimo iliyowasilishwa na Waziri mwenye dhamana, rafiki yangu sana, Komredi Daniel Chongolo. Katika kuanzia, ninaomba mapema kabisa niwasilishe salamu ambazo wakulima wa Tunduru wamenituma nizilete kwa Waziri, Mheshimiwa Chongolo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, wamenipa ujumbe wa wakulima wa korosho kwamba pembejeo za korosho bado hazijafika Tunduru na upuliziaji katika jimbo letu unaanza mapema mwezi Mei. Kwa hiyo, wamenituma nifikishe ujumbe kwamba pembejeo zifike mapema ili uzalishaji uweze kupanda na tuweze kumudu maisha yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujumbe wa pili, walionituma Wanatunduru, wamenieleza kwamba mfumo wa stakabadhi ghalani licha ya mafanikio yake bado una changamoto kwenye malipo. Wanamwomba sana Mheshimiwa Waziri yale mambo mepesi mepesi, kwa Kiingereza tunaita low hanging fruits, tuyafanyie kazi. Kwa mfano mmoja, wakulima wa korosho mpaka sasa wanakumbana na tatizo la kinachoitwa dormant accounts. Yaani akaunti zao zikiwekewa fedha kwa sababu hawazitumii mara kwa mara, wakienda kufuata malipo yao wanaambiwa kwamba hawawezi kuyapata kwa sababu akaunti zimelala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwamini komredi Chongolo hili anaweza kulifanyia kazi kwa kuweka tu utaratibu maalum wa kwamba tunazitambua akaunti za wakulima hawa wa korosho na tunazipa hadhi maalumu kwamba hizi hazikabiliwi na tatizo la kulala. Utapofika wakati fedha zao zimewekwa zitakatwa kama kawaida sababu wakulima hawa maskini wanasafiri kilomita nyingi, unakwenda benki unaambiwa fedha hakuna tatizo dormant account, nenda chama kikuu, rudi kwenye chama cha msingi, hili linawasumbua sana wakulima. Haya nikasema niyatangulize kwa sababu nimepewa ujumbe niufikishe, nami ni mjumbe na mjumbe hauwawi. Ahsante sana na ninaamini Waziri ameyachukua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina michango mingine miwili katika eneo linalohusu mwelekeo wa kitaifa. Niwe mkweli kwamba leo nimesikitika sana, kwa sababu nilikuwa na matamanio kwamba mwenendo katika sekta ya kilimo uweke mazingira ambayo ndugu yetu, Mheshimiwa Waziri wa Kilimo tutaweza kumpima, lakini kwa masikitiko makubwa sana hali ninayoiona sioni kama tunaweza kumpima ipasavyo Waziri wa Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayasema haya kwa makusudi ukitazama Kamati yetu ya Bunge imefanya kazi nzuri sana. Utaona kwamba bajeti iliyowasilishwa leo imeporomoka kwa asilimia saba. La pili, utaona utekelezaji wa bajeti kwa Mwaka wa Fedha uliopita 2025/2026, nao mpaka sasa mwezi Machi ni 42% tu ya utekelezaji. Hii maana yake ni nini? Mipango tunayojiwekea hatuitekelezi na hii inatoa picha mbaya sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, picha inayozaliwa ni kwamba Serikali ya Chama Cha Mapinduzi imeitupa sekta ya kilimo na imemtupa mkulima wa Tanzania. Hiyo ndiyo picha tunayoipata na yeyote anayewatupa wakulima wa Tanzania anacheza na mustakabali na maslahi ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pendekezo langu, kama tunakuja bungeni tunapitisha bajeti halafu hatuitekelezi, ni bora tuache kabisa katika msimu huu wa bajeti tusipitishe bajeti ya kilimo mpaka utekelezaji wa bajeti iliyopita ufanyike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kufanya hivyo zoezi la kupitisha bajeti litakuwa ni zoezi la kinadharia. Kwa hiyo, mchango wangu tunaitaka Serikali iwe serious katika utekelezaji wa bajeti na hasa katika utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji, kwa sababu hatuwezi kuleta mapinduzi ya kilimo bila kuwekeza vya kutosha katika umwagiliaji. Huo ndiyo mchango wangu wa pili.

MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Mwenyekiti ninaomba nimpe Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa. Mheshimiwa Mwantumu Zodo.

TAARIFA

MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ninaomba nimpe Taarifa mzungumzaji, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupitia Wizara yake kwa kuliona hilo, kuwa nchi haiwezi kusonga mbele kwenye kilimo bila miradi ya umwagiliaji, licha ya kuwa amepeleka pesa kwenye miradi, lakini amenunua magari 26 kwa ajili ya kuchimba visima ili ku-support miradi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyozungumza hapa magari yapo site, yameshatoka Mkoa wa Dodoma na sasa hivi yamehamia mkoa mwingine na yatazunguka nchi nzima licha ya kuwa miradi ya umwagiliaji ipo lakini na magari yanaendelea ku-support. Ninakushukuru. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ado unaipokea Taarifa hiyo?

MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei taarifa hiyo. Siipokei ndyio maana nilitanguliza shukurani kwa Kamati yetu ya Viwanda, Biashara na Kilimo. Taarifa kwenye Kamati inaonyesha kwamba miradi zaidi ya 50 ya umwagiliaji ambayo ilipangwa kuanza haikuanza kabisa. Miradi mingine ambayo ilianza inachechemea na haya ninayoyasema yapo jimboni kwangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mradi mkubwa wa umwagiliaji wa skimu ya Nambarapi mpaka sasa unachechemea ilibidi mwezi Januari uwe umekamilika. Kwa hiyo, haya tunayoyazungumza tunayazungumza kwa ajili ya mapenzi kwa Taifa letu kwamba, Serikali iwe serious kwenye utekelezaji wa bajeti. Huo ndiyo mchango wangu wa pili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wa tatu na wa mwisho, Serikali imefanya vizuri sana kubadilisha sera yake kutoka sera ya zamani ya kuingilia fedha za kwenye Mifuko Maalum ya Uendelezaji wa Mazao, kwenye korosho tuna export levy.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)