Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mtera
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili nitoe mchango wangu kwa Wizara hii ya Kilimo. Wabunge wengi wamempongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kumteua Mheshimiwa Chongolo na Naibu Waziri pamoja na Katibu Mkuu na watendaji wote akiwemo Mtendaji Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, tunawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuna mashaka na Waziri wa Wizara ya Kilimo. Hatuna mashaka naye, kwanza ni kada asiyetiliwa shaka, lakini pili amekuwa Katibu Mkuu wa chama chetu. Katika majimbo mengi ya wabunge mlioko hapa, Mheshimiwa Chongolo amepita. Kwa hiyo, mengi tunayomwambia hapa Mheshimiwa Chongolo anayajua kwa kuyaona kwa macho. Hatuna shaka naye kwamba atakwenda kuyashughulikia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vitu ambavyo mimi ninawakubali sana, wenzetu Waislamu wanasema Mwenyezi Mungu ndiye anayetoa neema ndogo na neema kubwa, lakini leo mdogo wangu hapa anasema ikiwa neema ndogo bora tuache kabisa isitolewe. Kitu cha ajabu sana kuwahi kukisikia. Anasema kama bajeti yenyewe ni kidogo hivi basi bora tuache kabisa. Ikitokea hivyo basi ni hatari kubwa sana hata kwenye level ya familia, kwamba umepeleka leo ugali maharage halafu mkeo anasema leo hatupokei kabisa tunalala na njaa. Hapana! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo changamoto kwenye kilimo lakini tuna uhakika kwamba utatuzi wake na majawabu yatatoka kwenye Serikali ya Chama Cha Mapinduzi. Tuna uhakika majibu Mheshimiwa Chongolo na mwenzake wanayo, waendelee kutatua changamoto zinazotukabili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wengi wanazungumzia kuhusu miradi ya kilimo. Mimi hapa ni mnufaika wa BBT. Hilo shamba linalotajwa Ndogowe lipo kwenye jimbo langu, Jimbo la Mvumi. Ninapenda nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, nimeona sasa hata vijana wengine wameanza kuhamasika kwenye kilimo. Majuzi nilikuwa ninatembelea pale nimekuwa shamba kama eka 500 hivi, analima huyu kijana Msanii anaitwa Masanja Mkandamizaji. Hiyo imeamsha ari ya vijana wengi wa maeneo yale kuanza kuchangamkia kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumwombe tuendelee kutenga heka za kutosha kwa ajili ya wanakijiji chenyewe cha Ndogowe, wanakijiji wenyewe wa Mlazo na Kata nzima ya Ng'hambaku waweze kushiriki na kupata joto la maendeleo kwenye eneo lile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoitaka Wizara ya Fedha ipeleke fedha kwenye Wizara ya Kilimo, tunafahamu kwamba Wizara ya Fedha inapeleka pesa kwenye maeneo mengi ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge. Mvua nyingi tumepata tunamshukuru Mungu lakini barabara nyingi zimeharibika, ni Wizara ya Fedha hiyo inatakiwa kupeleka, lakini tunaomba mgawanyo wa hicho kidogo kinachopatikana walau usaidie kusukuma mbele Wizara ya Kilimo ili kuweza kutekeleza miradi yake mikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana Waheshimiwa Wabunge nami hapa tunashauri kwamba, ile miradi mikubwa ya kimkakati itafutiwe pesa nje ya bajeti ya Serikali. Ziende zitafutwe fedha kama zilizotafutwa za kujenga SGR, kama zilizotafutwa za kujenga Bwawa la Mwalimu Nyerere. Zitafutwe fedha kwa mkakati mahususi kwa ajili ya kukamilisha miradi mikubwa ya umwagiliaji ili bajeti iliyopo isukume mabwawa madogo madogo yaliyopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Mkoa wa Dodoma hatuna mto unaotiririsha maji mwaka mzima. Kwa hiyo, sisi tunapozungumzia kilimo cha umwagiliaji kwetu sisi hakitawezekana kama hatuna mabwawa ya kumwagilia maana mito yetu inakauka yote kwa haraka. Kwa hiyo, tunamsihi sana Mheshimiwa Waziri, ajitahidi kadri inavyowezekana tutafute fedha zisukume miradi mikubwa ili hii miradi midogo itengenezwe na bajeti iliyopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ninataka nizungumzie kuhusu Stakabadhi Ghalani. Stakabadhi Ghalani kuna maeneo ambayo wenzetu wameanza muda mrefu na sisi sasa hivi wametugusa. Siyo jambo baya, lakini tunaomba ugusaji wetu uwe tofauti na maeneo mengine. Kwa mfano, kwanza hatujawekeza kiasi kikubwa sana kwa wakulima wa ufuta, kwa wakulima wa mazao yanayoingizwa kwenye ghala. Kuna watu wamewakopesha pesa wakulima ili walime, hasa kwenye ukanda ule wa Tarafa ya Mpwayungu, Tarafa ya Makang’wa na kidogo Tarafa ya Mvumi. Sasa ninashauri nini Mheshimiwa Waziri?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashauri wale waliowekeza hela zao kwa wakulima wanunue wao kama wakulima wanapenda kuwauzia cash, halafu wale wakishanunua waweke kwenye ghala. Wakiweka kwenye ghala wakati wa kuja kuuza, wakulima waalikwe ili waone namna wanavyopunjwa ili mwakani wakulima wasikubali tena kumuuzia mtu. Mbona hili jambo ni rahisi sana? Wala hatuna haja ya kugombana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuwaombe wananchi wawe watulivu, wale wale wanaonunua kama wanayo cash wakanunue, lakini wale wanunuaji waingize kwenye ghala. Wakishaingiza kwenye ghala wakati wa minada, wakulima waalikwe waje waone namna wanavyopunjwa kwa kuwauzia wale. Matokeo yake yataonekana ndani ya mwaka, wala huhitaji kutumia nguvu, utamwona mkulima mwenyewe tu anaingiza kwenye ghala. Kwa hiyo, wakati mwingine tutumie hesabu kidogo tu kumaliza utata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, imezungumzwa hapa kuhusu mbolea. Tumeona disaster zilizotokea duniani, mipaka inafungwa, hebu tuimarishe viwanda vyetu vya ndani. Waheshimiwa Wabunge wamesema kwa uchungu sana na hili ninataka niishauri Serikali, viwanda kama ITRACOM hiki cha Dodoma, tuviwekee pale nguvu zetu kubwa ili viwanda vizalishe, mbolea yake inunuliwe ili itusaidie. Pale tuna Minjingu, utafiti umeshafanywa. Tatizo letu kubwa ni kwamba hatutaki kuthamini vilivyo vyetu, tuelimishane ndugu zangu, tutumie vitu vya nyumbani kwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, imezungumzwa sana hapa na Waheshimiwa Wabunge na ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri, tujitahidi sana. Tunapozungumza habari ya kilimo bora cha biashara tunazungumzia mbegu. Watafiti wetu wa TARI na taasisi zingine zote wanajitahidi sana kwenye kugundua mbegu na kuzisimamia lakini tatizo hatuwapi nguvu za kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua kama kuna Wizara ina mipango, ninataka nimwambie Comrade Chongolo Wizara yako ina mipango safi kabisa. Ina mipango ya kutosha na kila kitengo kimejipanga vizuri, tuwawezeshe nguvu ili wafanye kazi. Tunapozungumzia mbegu bora kuna watu wengine wajanja nao wanaingiza mbegu feki. Nchi yetu ina wajanja wengi. Hivi vitengo tuviwekee nguvu ili vikusanye mbegu feki zikamatwe na hatua kali zichukuliwe kwa wanaoingiza mbegu feki kwa ajili ya wakulima wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakusihi sana, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji nimeigusa, nimegusa viwanda vya ndani viongezewe nguvu. Tunataka tumhakikishie Mheshimiwa Waziri asife moyo hili suala la BBT, suala la kuinua vijana sasa hivi kuna vijana wasomi wameingizwa kwenye pamba, tumeona namna ambavyo wamelisisimua zao la pamba. Tumewaona wengine wameingia kulima zabibu, wengine wanalima alizeti, wengine wanataka kufungua viwanda vya mafuta ya alizeti. Tuwekeze nguvu za kutosha ili vijana wetu sasa wajikite kwenye kilimo ambacho kitawapa faida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa lililoshiba hata namna yao ya kuwaza ni tofauti. Vijana hawatawaza mambo ya hovyo, watawaza mambo ya maendeleo. Twende tufanye mabadiliko watu wakipende kilimo. Waimbaji wetu, vijana wasanii waimbe kuhusu kilimo, nyimbo za mapenzi zimeshatosha, sasa hivi tunataka tuone uhamasishaji wa kilimo kutoka kwa wasanii wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na ninaunga mkono hoja. (Makofi)