Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi jioni hii ya leo. Kwanza kabisa ninaomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kusimama hapa jioni ya leo. Pia, ninaomba nimshukuru Rais wangu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ni Mwenyekiti wetu wa Chama Cha Mapinduzi Taifa kwa kupitisha jina langu na hatimaye kuwa Mbunge. Kwa hiyo, ninaomba nimshukuru sana Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Wajumbe wote wa Kamati Kuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo sasa, ninaomba nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya dhati ya kutaka kuona kuwa sekta yetu ya kilimo inaendelea kusonga mbele. Dhamira hii ya dhati kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan inajidhihirisha kupitia bajeti za kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa kipindi cha bajeti ya 2021 bajeti yetu ya kilimo ilikuwa ni shilingi bilioni 294, lakini kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025, wakati wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, bajeti hii tumeona imeongezeka kutoka zaidi ya shilingi bilioni 200 mpaka shilingi trilioni 1.2 na ushee. Hii ni wazi kuwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ana dhamira ya dhati ya kutaka kuwakomboa wananchi kwenye kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati ninampongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitampongeza Waziri wetu wa Kilimo, ndugu yangu Mheshimiwa Chongolo. Wote tunamfahamu Mheshimiwa Chongolo ni mchapa kazi na ni mtu rahimu. Tunamfahamu ameongea sana hapa Kibajaji, alikuwa Katibu wetu wa Chama Taifa. Hii miradi hapa tunayoililia na mingine tunayoipigania yeye anaifahamu yote, kwa hiyo nimefurahi sana kuwekwa kwenye Wizara hii kwa sababu atakwenda kuisimamia vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata wakati Waziri Mkuu anahitimisha bajeti yake, Mheshimiwa Chongolo alisimama hapa akaongea. Kati ya mambo aliyoongea jambo mojawapo lililonifurahisha ni lile alilosema kuwa anakwenda kuweka nguvu kwenye uzalishaji wa mbegu na anakwenda kuziongezea zile taasisi bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kuweka nguvu kwenye uzalishaji wa mbegu, hii bajeti yote na hizi jitihada za Mheshimiwa Rais zitakuwa ni kazi bure. Kwa sababu kipindi cha nyuma wakati wa 2021 uzalishaji wa mbegu ulikuwa ni takriban tani 30,167 lakini kipindi cha Mwaka wa Fedha 2025/2026 ambacho na Mheshimiwa Chongolo ndiyo amekuwa Waziri, wameanza kutekeleza hiyo bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi hiki ambacho sisi tumekuwa hapa uzalishaji wa mbegu umeongezeka kutoka tani 30,000 mpaka tani 54,000. Kati ya hizo tani 54,000, tani 47,000 zinazalishwa na sekta binafsi na tani 7,000 zinazalishwa na taasisi yetu ya mbegu ya ASA. Tafsiri yake ni nini? Tafsiri yake ni kuwaongezea nguvu hawa wazalishaji binafsi wa mbegu ili tuweze kusogea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kuwapa nguvu hatuwezi kupata uhakika wa mbegu. Ninamwomba kaka yangu, Mheshimiwa Chongolo tunaweka nguvu kwenye uzalishaji. Nilimsikia hapa asubuhi amesema kuhusu miundombinu. Kuna baadhi ya mashamba yana miundombinu, lakini mengi hayana. Twende tukaboreshe miundombinu kwenye mashamba yetu ya mbegu ili yaweze kuzalisha mbegu mwaka mzima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tusipoboresha miundombinu wakulima watategemea mvua, mashamba ya mbegu yatategemea mvua, mvua isiponyesha mashamba ya mbegu hayatazalisha, wakulima hawatakuwa na mbegu. Ninaomba twende pia tukaweke nguvu kwenye miundombinu, tukaongeze spidi kwenye miundombinu ya haya mashamba. Wakati huo tunapambana na miradi hii ya umwagiliaji kwenye majimbo yetu, lakini tuyaangalie na mashamba haya ya mbegu kuendelea kuweka miundombinu ili tupate uhakika wa mbegu bora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la mbegu ni tatizo kubwa. Nilishuhudia mwaka huu 2026 ambao wakulima ndiyo wanasubiri kuvuna hapa Dodoma, Kata ya Itiso kwa kaka yangu Deo, wakulima walipanda mbegu zao za alizeti, walikuwa wamenunua kwa mdau mmoja Manyara, mbegu zile hazikuota zote. Walirudia kupanda tena mara ya pili. Hata akitaka idadi ya wakulima wale, wenye uwezo walirudia kupanda, ambao hawana uwezo hawakurudia, kwa hiyo wakulima walipata hasara. Kwa hiyo, sina mashaka na Waziri na nilipata nguvu sana baada ya kusikia anakwenda kuweka nguvu kwenye uzalishaji wa mbegu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri akienda kuweka nguvu kwenye eneo hili dhamira ya Mheshimiwa Rais itafikia malengo, lakini bila kuwa na mbegu za uhakika hatutakuwa na mazao ya uhakika na ziada ya chakula. Wakulima wetu wanategemea ziada ya chakula kama kipato chao. Wanalima ili kupata chakula, lakini wanalima ili kufanya biashara wapate pesa. Kwa hiyo, ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kule Mkoani kwetu Tanga tuna zao la mkonge. Ninaipongeza sana Wizara wanafanya vizuri, lakini changamoto ndogo ni wakulima wale wadogo wadogo wanapata tabu na zile korona. Hakuna korona za kutosha za kuchakata mkonge. Wakati mwingine mkonge wao unaharibika unakuta umeshakomaa, yule mnunuaji mkubwa haendi kununua kule, kwa hiyo hiyo ni changamoto kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine nimeona, mara nyingi, mashamba mengi ya mkonge yanaungua…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa kwa mchango wako.
MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la mwisho. Mheshimiwa Waziri ajaribu kutuangalia kule Tanga kwenye zao letu lile la machungwa. Ajaribu kutuangalia sana, atupelekee kiwanda kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na ninaomba kuunga mkono hoja ya Wizara hii ya Kilimo. (Makofi)