Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Hawa Subira Mwaifunga

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba hii ya Wizara ya Kilimo. Kwanza kabisa ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya na uzima nimeweza kusimama hapa kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ninaomba nimshukuru sana na nimpongeze sana Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kututoa kwenye kilimo tulipokuwa mpaka hapa sasa tulipofikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukisema kwamba hakuna kinachofanyika kwa kweli tutakuwa hatutendi haki. Mnyonge mnyongeni haki yake mpeni, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya vizuri sana kwenye sekta nzima ya kilimo. Miaka 10 iliyopita nilikuwa upande wa pili, nilikuwa sehemu ya kusisitiza kuhakikisha kwamba wananchi wananufaika na kilimo na leo tunavyozungumza hata mimi kwenye Mkoa wangu wa Tabora tunasema yes kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kwanza nizungumzie kuhusiana na suala zima la hii miradi mikubwa ya umwagiliaji. Hapa hata watu wakiangalia kwenye taarifa ya Kamati imeeleza vizuri sana na ninaungana na Wanakamati. Ninaungana moja kwa moja na Kamati kuishauri Serikali kuhakikisha kwamba miradi hii mikubwa ya umwagiliaji zaidi ya miradi 26 inatafutiwa fedha maalum na siyo tusubiri bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukisema tutasubiri bajeti kwenye miradi hii hatutamtendea haki Mheshimiwa Rais. Tutapiga mark time miaka 20 hapa miradi hii ya mabwawa haijakwisha na kazi kule haitaonekana. Suala la kilimo cha umwagiliaji halina ubishi, suala hili lina tija na tunaamini kwamba tukiwekeza, kwenye suala zima la mabwawa haya, ninaamini kabisa kwamba tutakwenda kubadilika kutoka kwenye kilimo cha kusubiri mvua na kuwa kilimo chenye tija cha umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niishauri Wizara ingalie uwezekano wa kuhakikisha kwamba fedha inatafutwa nje ya hizi fedha za bajeti kwa ajili ya kumalizia miradi hii mikubwa, tuweze kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais ili akiondoka mwaka 2030, aondoke kifua mbele akiwa amehakikisha kwamba Watanzania sasa tuko vizuri kwenye sekta nzima ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuelezea kuhusiana na suala zima la viwanda vya mbolea na hususan ahadi ya Chama Cha Mapinduzi kwa wananchi wa Tabora. Nimekuja na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, kijitabu hiki unachokiona, kidogo, lakini kimesheheni kwelikweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 5/9/2025 Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alikuwepo katika Mkoa wa Tabora, Jimbo la Tabora Mjini, alizungumza na akatoa ahadi ya kuhakikisha kwamba, Tabora tutapata kiwanda kikubwa cha mbolea. Ipo kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, haya siyo maneno yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya Mheshimiwa Rais kuzungumza alitukabidhi vitabu hivi na alipokuwa akinikabidhi aliniambia, mwanangu huu ndiyo mkataba baina yetu Chama Cha Mapinduzi na wananchi hawa, utakapokwenda kuzungumza nao. Siku 63 sikuwahi kuacha kutembea na kitabu hiki na kuwaambia Watanzania, Wananchi wa Tabora, kata 29, Chama Cha Mapinduzi kitakwenda kufanya nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa leo ninaomba kumwambia ndugu yangu, mimi sina mashaka kabisa na Mheshimiwa Chongolo, Waziri msikivu, mpole na mwelewa. Ninaamini Mheshimiwa Waziri anaijua Tabora kuliko inavyomfahamu, amepita kwenye changamoto mbalimbali katika Mkoa wa Tabora, anaijua vizuri, anajua jinsi ambavyo tuna eneo kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi watu wa Tabora, ninavyozungumza na Waziri hapa, tuna kilometa za mraba zaidi ya 76,151. Hakuna mkoa wowote ambao unazifikia kilometa hizi za mraba, lakini tumetengewa sisi watu wa Tabora zaidi ya 26.6%, hili eneo linafaa kwa kilimo na bado halijakwisha. Hizi ni zaidi ya kilomita za mraba 20,199 na hili eneo halijakwisha. Ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri, kama maeneo yaliyotengwa yanaonekana kwamba, yana gharama kubwa, Tabora siyo maskini wa maeneo. Twende tukamwoneshe, kama imeshindikana huko, sisi tupo, tutakwenda kumwonesha maeneo. Waje wawekeze kwenye kiwanda cha mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuna maneno mengine ya kuwaambia Wananchi wa Tabora kuhusiana na suala la kiwanda, lazima kiwanda cha mbolea kije Tabora kwa sababu, mama ameahidi na mama akiahidi anatekeleza. Twende tukatafute eneo tujenge kiwanda cha mbolea katika Mkoa wetu wa Tabora. Haijalishi hata kama haitakuwa kwenye Jimbo la Tabora Mjini, lakini kijengwe kwenye Mkoa wetu wa Tabora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na sisi kuomba kiwanda cha mbolea, sisi ndiyo wenye soko. Tabora tunalima tumbaku kwa zaidi ya 70%, kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Kilimo, zaidi ya 70% ya tumbaku ya nchi hii tunalima sisi Mkoa wa Tabora. Tuna majirani zetu, Katavi, Kigoma, Shinyanga na Simiyu, hawa wote wanalima tumbaku. Kiwanda kikijengwa pale Tabora ni centre ya mikoa yote hii kupata mbolea kwa urahisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haijalishi, malighafi tunayo inasafiri nchi mbalimbali, inafanya kazi na mbolea inakuja hapa. Kwa nini Tabora? Tabora itafika; tujengewe kiwanda, malighafi itatoka Ruvuma, malighafi itatoka Songwe, malighafi itatoka kokote katika nchi hii, ifike Tabora tutengeneze kiwanda. Mwekezaji anajua hawezi kupata soko kubwa kama lililoko Mkoa wa Tabora, la tumbaku tunayoilima pale Tabora kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, leo tunacho kiwanda kingine cha mbolea hapa Dodoma, kipo pale Nala. Ninakumbuka mwaka jana Mheshimiwa Rais alikwenda kukizindua kiwanda kile. Kiwanda kile kinazalisha zaidi ya tani milioni moja kwa mwaka, lakini kimeajiri zaidi ya Watanzania 1,000. Ninaiomba sana Wizara iende ikakae chini na hawa wawekezaji, inawezekana wakaweza kutuzalishia zaidi ya hiki ambacho wanakizalisha sasa, ili sisi suala la mbolea ikitokea vita na kukitokea changamoto zozote, sisi kwenye suala la mbolea tunatakiwa tuwe sawasawa kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bado ninaendelea kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa miradi ya umwagiliaji katika Mkoa wa Tabora.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ya Tabora ya umwagiliaji…

MWENYEKITI: Muda wako umekwisha, Mheshimiwa.

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: …imebaki sita peke yake, ndiyo ambayo fedha zake zimetengwa, ili ziweze kutumwa. Mingine yote angalau imeishia 50%, lakini mingine imekamilika kabisa…

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa kwa mchango wako.

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)