Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ulyankulu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JAPHAEL M. LUFUNGIJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa nafasi. Ninatumia fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kibali cha kuweza kusimama siku ya leo tena Bungeni nikijadili Taarifa ya Wizara ya Kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa mapenzi mazuri ya kuwajali Watanzania, hasa kwenye Sekta kubwa ya Kilimo. Muda mwingi Wizara hii bajeti imekuwa ikipanda kila wakati, lakini Waziri wa Kilimo na Naibu Waziri pamoja na Watendaji wote, tumeona kwenye Kitabu cha Bajeti mambo mengi, mambo mazuri yamewekwa, kwa ajili ya Watanzania, kuwawezesha wakulima wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu ninaomba kuuelekeza upande wa zao la tumbaku. Kwa Tabora na Jimbo la Ulyankulu sisi ni wakulima wakubwa wa tumbaku. Ziko changamoto kubwa za upandaji wa mbolea na kushuka kwa madaraja ya uuzaji. Msimu uliopita wa 2024 mbolea ya NPK iliuzwa kwa Dola 60.77, lakini kwa msimu huu mbolea inauzwa kwa Dola 63, jambo hili ni ongezeko kubwa linalokatisha tamaa wakulima. Isitoshe, bei ya madaraja ya zao la tumbaku imeshuka mno, Dola 0 ina madaraja 18, lakini Dola 01 madaraja 29 na Dola 02 madaraja 16; Dola 03 yenye faida kubwa kwa mkulima imepewa madaraja mawili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili linakatisha tamaa kwa wakulima. Tunaiomba Serikali yetu ione namna ya kuweka ruzuku kwenye mbolea ya NPK ambayo ndiyo mbolea inayotumika kwa asilimia kubwa kwenye zao la tumbaku, ili kuwa-favor wakulima waweze kupandisha uzalishaji. Wakulima hawa wa tumbaku, Serikali ifikirie wako wakulima, Serikali ikubali wa-graduate, wako wakulima wanaoweza kulima kwa kujitegemea, ione haja ya kuwaruhusu wakulima wenye mitaji waweze kulima kwa kujitegemea kuliko kuendelea kuwang’ang’aniza wabaki kwenye kukopeshwa. Hilo ni ombi kutoka kwa wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, tumezungumzia issue ya kiwanda cha mbolea. Ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, mwenye mapenzi mema, Mkoa wa Tabora na Wanatabora aliwafurahisha kweli wakati wa kampeni yake. Kiwanda hiki kinahitajika kwa wananchi na wakulima wote wa Mkoa wa Tabora. Itambulike kwamba, watumiaji wakubwa wa mbolea ya NPK ni wakulima wa tumbaku na sisi Tabora ndiyo tunaozalisha kwa 70% zao la tumbaku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba Serikali, kama ambavyo watangulizi wamesema, Tabora tunayo maeneo mengi ya uwekezaji, tusitafsirike kwamba, eneo la Tabora linahitaji fidia ya hela nyingi, la hasha! Yako maeneo mengi na wananchi wako tayari kupokea kiwanda hiki. Tunamwomba Mheshimiwa Waziri na Watendaji wote waone umuhimu wa kuwekeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mabwawa. Kwenye Ilani, katika Jimbo la Ulyankulu, yameelezwa yatajengwa mabwawa matatu; Bwawa la Kona Nne, Bwawa la Mwamnange na Bwawa la Igombe. Ninaiomba Wizara itoe kipaumbele kwa sababu, jimbo hili wako wananchi wakulima wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili, kulingana na muda. Jimbo la Uliyankulu linazalisha pia, mazao ya chakula, zao la karanga, mpunga na mahindi; tutafutiwe masoko, kwa maana ya kujengewa maghala. Leo karanga iliyoko Jimbo la Ulyankulu, kwa eneo la Ulyankulu wanunuzi wanunua kwa shilingi 2,900 kwa kilo, lakini ikitoka inakwenda kuuzwa Kahama, Kahama wanauza shilingi 3,500. Unaweza ukaona namna ambavyo watu wanalangua, wanahama kwenda eneo dogo, wanapata faida kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mteja wetu mkubwa sisi ni watu wa Rwanda. Tuone haja ya kujengewa maghala na kuhakikisha kwamba, uendeshaji wa zao la karanga unafanyika katika maeneo husika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, kulingana na muda, ni suala la pembejeo za kilimo upande wa mahindi. Bado gharama ni kubwa, mkulima anatumia zaidi ya shilingi 370,000 kwa kiwango cha chini, lakini uangalie leo uzalishaji kwa Mkoa wa Tabora, kimsingi eka moja haizidi magunia 12. Leo mahindi yanauzwa, gunia moja la kilo 108 linauzwa, shilingi 42,000, ukichukua shilingi 370,000 ina maana faida yake ni kama shilingi 50,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili bado halijakaa vizuri. Tunawaomba Wizara, watusaidieni kutafuta masoko, ili kumpa tija mkulima huyu. Vitu vingine vinapanda, lakini upande wa wa mazao ya chakula bado bei zake ziko chini, kwa hiyo, tunakuomba sana Mheshimiwa Waziri...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. JAPHAEL M. LUFUNGIJA: ...hilo hatuna mashaka na Waziri. Yeye ni mchapakazi na watendaji wake wote tunawaamini.
MWENYEKITI: Muda wako umekwisha, Mheshimiwa.
MHE. JAPHAEL M. LUFUNGIJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana na ninaunga mkono hoja.