Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Asha Salum Motto

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ASHA S. MOTTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hii Bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dira inasema tujilishe na tuwalishe wengine kibiashara. Tunaweza kuona pia hata kwenye vipaumbele vya Wizara hii inasema kuongeza tija na uzalishaji hivi vyote vinaenda sambamba. Kilimo kama walivyokwisha kusema kwamba ni uti wa mgongo, lakini ukiangalia pia kilimo kimesaidia Tanzania kuajiri 70% ya Watanzania, kwa hiyo kilimo ni ajira. Pia kilimo hiki hiki kimeweza kuchangia pato la Taifa zaidi ya 25% kwa hiyo, hata Dira ya Maendeleo ya Taifa inatambua mchango wa kilimo kama ni kichocheo cha uchumi wetu hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila mbegu na siyo tu mbegu bila mbegu bora na bila mbolea hatuwezi tukasema kwamba tuna kilimo chenye tija. Mbegu bora ni msingi wa kilimo chenye tija na mbegu bora huongeza mavuno. Nitumie fursa hii kumpongeza sana Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya katika kuimarisha hii Wizara ya Kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona uzalishaji wa mbegu bora nchini unavyoendelea kufanya kazi vizuri. Ninatokea Mkoa wa Mtwara mpaka sasa ninaishukuru sana Serikali kupitia Bodi ya Korosho imeendelea kuzalisha miche ya korosho na kuisambaza Mkoa wa Mtwara kwa wananchi wote, wakulima wote wa zao hili la korosho, kwa hiyo na sisi ni wanufaika wa mbegu bora na miche bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na usambazaji huo, ninaomba nitumie fursa hii kumwomba Mheshimiwa Waziri, Waziri wangu ni msikivu sana usambazaji wa miche hii bado unasuasua, wananchi wengi bado hawajafikiwa, hawajapa miche hii na maeneo bado yako mengi. Sisi kama Wabunge wa Viti Maalum tumeendelea kusisitiza na kuhamasisha wanawake wajitokeze kwa wingi kwa ajili ya kuhakikisha na wenyewe wanapanda mikorosho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapozungumzia mbolea kilimo chochote kama hatuna mbolea toshelevu maana yake ni kwamba hatutakuwa na tija na kama tulivyoona katika vipaumbele vya hapa wanasema kwamba lazima kuongeza tija na uzalishaji na mbolea huongeza tija na uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kutupatia mbolea na viuatilifu. Mheshimiwa Rais ametoa ruzuku ya bilioni 300, hii ilisaidia sana kupunguza gharama za pembejeo, lakini pia itaongeza tija katika kilimo. Mkoa wa Mtwara wakati anaingia Dkt. Samia madarakani korosho tulikuwa tunalima tani 100,000, lakini sasa hivi zimeongezeka mpaka tani 600,000. Sisi kwetu tumeona na tumefaidika na hiyo ruzuku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nishauri, pamoja na kwamba tuna viwanda vya mbolea hapa Tanzania takribani 48, tuna viwanda viwili ambavyo ni vikubwa na vina uwezo wa kuzalisha tani takribani 1,200 na kitu, viwanda hivi kuna INTRACOM na Minjingu lakini tuna viwanda 14 vya size ya kati, tuna viwanda pia vidogo vidogo takribani 32, viwanda hivi vina uwezo wa kuzalisha tani 150,000 kama tulivyoona. Uzalishaji huu ni mdogo sana ukilinganisha na uhitaji wetu Nchini Tanzania ambapo sasa hivi tuna uhitaji takribani wa tani 1,500,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia sana takwimu hiyo inatupelekea sisi kwenda kutegemea 80% ya mbolea kutoka nje. Uzalishaji wa viwanda hivi havina tija, ninaomba sasa niishauri Serikali kwanza kabisa ione namna bora ya kuhamasisha viwanda hivi vya ndani kutumia rasilimali zetu tulizonazo hapa nchini, ikiwemo makaa ya mawe, gesi pamoja na mabaki yale ya taka kwa maana tunaweza tukazalisha wenyewe na tukajitegemea wenyewe bila kutegemea nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu, kama sisi tunazalisha 20% tunategemea mbolea inayotoka nje 80%, kwa kweli hatutaweza kufikia tija katika uzalishaji na hatutaweza kupata ajira, wala kutoa ajira kwa vijana wala kwa wanawake. Hatutaweza kufanya mutation kwa Taifa letu. Ina maana uchumi tunapoongelea kupandisha trilioni moja 2050, hatutaweza kufikia tija. Ni lazima tuhakikishe kwamba tunahamasisha hivyo viwanda ambavyo vipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba Serikali ina mpango wa kujenga kiwanda kikubwa sana cha uzalishaji wa mbolea cha Triple Sulphurs Phosphate, ninashauri pia Serikali kuendelea kuhamasisha wawekezaji kutoka nje kuja kuwekeza kuzalisha mbolea nchini kwa kutumia rasilimali tulizonazo. Kwa mfano, Mkoa wa Mtwara tunaye mwekezaji ambaye anaitwa Soil Solution na yeye anakuja kuwekeza mradi takribani US Dollar milioni 627 na anatarajia kutoa ajira kwa wananchi takribani 3,000. Hii kwetu ni advantage; vijana wengi watapata kazi na vilevile tutaondokana na utegemezi wa mbolea kutoka nje (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia niishauri Serikali. Maafisa kilimo waendelee kutoa elimu kwa vitendo kwa wakulima juu ya namna bora ya kutibu udongo. Maana pia udongo umekuwa na changamoto, lakini wananchi wengi kule vijijini hawajui hata namna ya kuutibu udongo; na Maafisa Kilimo wengi hawawafikii wakulima kule chini. Kwa hiyo ninawashauri Maafisa Kilimo watoke kwenye viti washuke chini waende wakawape elimu ya kutosha wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa mwenyekiti, kuna namna pia ya kuwapa elimu namna ya kufanya crop rotation. Wananchi wengi hawajui nini maana ya crop rotation...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Muda wako umekwisha Mheshimiwa.

MHE. ASHA S. MOTTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na ninaunga mkono hoja. (Makofi)