Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Kakulu Burchard Kakulu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbagala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. KAKULU B. KAKULU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa nafasi ya jioni, ili nami nipate nafasi ya kuchangia kidogo kwenye sekta muhimu ya kilimo ambayo kwa nchi hii ni sekta mahususi na sekta ya kipaumbele sana. Nitakuwa na mambo matatu ya kuchangia leo kwa ufupi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja nitazungumzia kuhusu ushirika kama nyenzo muhimu sana katika mapinduzi ya viwanda vijijini. Pili, nitazungumzia kuhusu umuhimu wa kuanzisha mamlaka mahususi ya usimamizi wa vyama vya ushirika vya akiba na mikopo, nje kabisa ya usimamizi wa ushirika wa jumla. Tatu, nitazungumzia kuhusu mikopo kwa vijana kwenye sekta ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa pongezi kwa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kinachoongoza nchi yetu kwa sasa, kwa kazi nzuri iliyoifanya katika kipindi kifupi kilichopita kwenye sekta ya kilimo. Yametokea mapinduzi makubwa sana kwenye sekta ya kilimo katika kipindi cha miaka minne, mitano iliyopita. Ruzuku katika mazao mbalimbali ambayo imepelekea kuongezeka kwa tija na uzalishaji mkubwa sana kwenye sekta yetu ya kilimo na kwa hiyo kama nchi kujitosheleza kwa sehemu kubwa katika chakula na katika mazao ya biashara na kuongeza mapato ya Taifa hasa kupitia mauzo nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, yametokea mageuzi makubwa sana hasa katika sekta za kipaumbele za mazao makubwa ya kilimo hasa korosho na sekta ya kahawa katika kipindi cha miaka michache iliyopita. Tunaipongeza Serikali na haya yote pongezi mahususi na za kipekee zimwendee Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dr. Samia Suluhu Hassan na wanaomsaidia kupitia Waziri wetu wa Kilimo, ndugu yetu na kiongozi wetu wa chama mstaafu, Mheshimiwa Dkt. Daniel Chongolo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajielekeza mchango wangu wa kwanza kwa ufupi sana kuzungumzia ushirika. Ukiniuliza ushirika nitakwambia ushirika ndiyo nyenzo namba moja ya kufanya mapinduzi muhimu sana vijijini hasa kupitia sekta ya viwanda. Jaribu kufikiria idadi ya vyama vya ushirika vilivyoko takribani katika kila sekta nchini. Sekta ya kilimo ikiongozwa kwa vyama vingi vya ushirika, sekta ya madini, sekta ya uvuvi, sekta ya mifugo na kila aina ya sekta unayoijua. Hebu jaribu kufikiria kwamba umefanya mageuzi kidogo sana ya kuhamasisha uanzishaji wa viwanda vya kuongeza thamani kidogo kwenye maeneo ya vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kwanza kitakachofanikiwa ni kusaidia kuongeza mazao yetu na kuyaongeza thamani kwenye maeneo ya vijijini. Pili, utasaidia kuchochea ajira katika maeneo ya vijijini na kwa hiyo kusaidia vijana wetu ambao wanakimbilia mijini kubaki mahali walipo. Tatu na muhimu zaidi, itasaidia kufungamanisha sekta nyingine zilizoko vijijini na kwa hiyo kuchochea ajira kwenye sekta nyingine zaidi nje ya ushirika wenyewe na shughuli zinazohusika na ushirika wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasisitiza kwamba, Mheshimiwa Waziri pamoja na kazi nzuri sana anayoifanya nimwombe; tunamfahamu, ni mchapakazi mzuri sana na juzi nilimshuhudia akitangaza ajenda maalum na kampeni maalum ya kuhamasisha uadilifu, uaminifu na uzalendo katika kusimamia na kuendesha vyombo vya ushirika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri, na ninamwamini kwamba ni mtu ambaye ana msimamo, ni mtu mwadilifu. Ni mtu ambaye akiamua kusimamia jambo analisimamia kweli. Kwa hiyo, tunamtarajia kwamba angalau kwenye eneo hilo na maeneo mengine kwenye sekta yake atayasimamia vizuri. Kwa hiyo, la kwanza lilikuwa ni hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, msisitizo ni kwamba, kwa sababu sekta hii ndiyo inayoajiri watu wengi zaidi kuliko sekta yoyote. Kama tukifanya mageuzi hayo katika viwanda vidogo vidogo kwenye sekta ya ushirika itatusaidia kufanya mageuzi makubwa zaidi na katika muda mfupi sana kuliko eneo lingine lolote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili nizungumzie umuhimu wa kuanzisha mamlaka maalum ya kusomea Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo. Kwa umuhimu wake na kwa sababu inahusika na transaction za fedha na Mheshimiwa Waziri na Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi, kwamba eneo hili limekuwa kwa kasi kubwa sana na kuna SACCOS kubwa zaidi hasa zinazochukua amana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasisitiza kwamba ni muhimu tuanzishe chombo maalum ambacho kitahusika kabisa kusimamia sekta hiyo ya vyama vya ushirika vya fedha, ili tuviondoe katika usimamizi wa jumla wa vyama vya ushirika. Moja, itatuhakikishia usalama wa fedha; Pili, itasaidia kuchochea kukua kwa haraka kwa sekta hiyo; na Tatu itatusaidia kuongeza kasi ya ukuaji wa akiba na mikopo na ku-mobilize resources nyingi sana kutoka kwa watu wadogo wadogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nisisitize jambo moja kuhusu mikopo kwa vijana. Kwa umuhimu wa sekta yetu na kwa wingi wa vijana walioko maeneo ya vijijini na kwa umuhimu wa sekta yenyewe, ninaamini, pamoja na kwamba ninajua tumeanza, lakini inabidi tuwe na kasi zaidi ya kuongeza ukubwa wa mikopo kwenye sekta hii ili vijana wetu waliosomea kilimo ambao hawajasomea kilimo walio na uwezo wa kufanya ujasiriamali kwenye sekta hii waweze kufanya vizuri zaidi, tuongeze ajira kwenye sekta hiyo ili ituongezee na kuchochea sekta ya biashara kwenye maeneo ya sekta ya kilimo. Vilevile itusaidie kuchochea na kuongeza mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wetu pamoja na maendeleo ya jumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba zaidi na muhimu, kilimo kama nyenzo muhimu ya kupunguza umaskini, tukiongeza mikopo kwenye eneo hili, hasa kwa vijana, tutachangia pakubwa katika kupambana na tatizo la umaskini kwenye maeneo ya vijijini na kwa hiyo kuisaidia nchi yetu kupiga maendeleo kwa kasi kubwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufupi nina hayo kwa leo. Wakati mwingine tutachangia na kushauriana na Mheshimiwa Waziri kuona namna gani tunavyoweza kusaidia sekta yetu kuendelea mbele. Asante sana. (Makofi)