Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, ninaomba nimshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya dhati ya kutaka kumtua mwanamke ndoo kichwani, na dhamira hiyo tunaiona. Ninaomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake yote, akiwepo Katibu Mkuu, dada yangu Mwajuma, kwa kweli tunawaona Wizara hii wanavyokimbizana, na wote ni mashahidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa muda ni mfupi sana leo, ninaomba niende moja kwa moja tu kwenye miradi michache, ambayo ninataka kuiongelea, hasa ya mkoa wetu wa Tanga. Sisi kwenye Mkoa wetu wa Tanga, mradi mkubwa ambao unaenda kuwa mkombozi wa maeneo mengi, ni ule mradi wa miji 28.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kwenye mkoa wetu, maeneo ambayo yana changamoto kubwa za maji hasa, ni Kilindi, Handeni, Muheza na Korogwe. Kupitia mradi huu wa miji 28, ambao sasa hivi uko takribani 77% unaenda kuwa mkombozi kwa maeneo haya niliyoyataja, mpaka kwenye Jimbo lile la Mheshimiwa Waziri, Pangani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Wizara kuongeza nguvu kwenye mradi huu. Mradi huu upo katika hatua nzuri, kubwa zaidi ni fedha. Wote tutakuwa mashahidi, tangu jana kila mtu anayesimama hapa kuongea, na ndiyo maana nikasema nianze kumshukuru Mheshimiwa Rais, kwani kila mtu kwenye jimbo lake kuna mradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kuna mradi umekamilika au kuna mradi unaendelea, lakini miradi ipo inatekelezwa. Tutakuwa mashahidi wote, kwa Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, pamoja na timu yake yote ya Wizara, tunawaona kwanza wanavyokimbizana, pili ni wasikivu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa iliyopo hapa ni upatikanaji wa fedha. Tuiombe Serikali ipeleke fedha kwenye miradi hii ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemwona hapa Mkurugenzi wa Mfuko ule wa Maji, tukaongeze nguvu kwenye mfuko huu. Niwaombe Wizara ya Fedha tuongeze nguvu kwenye Mfuko wa Maji, tukaongeze hata shilingi 50 tu. Mfuko huu utakwenda kutusaidia, kwa sababu moja ya kazi za mfuko huu pia unasaidia kutatua ile miradi chechefu, ile ambayo imekwama. Mfano mzuri ni ule Mradi wa Same - Mwanga - Korogwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi ule umeenda kukamilishwa kupitia fedha hizi za Mfuko huu wa Maji. Niwaombe wenzetu wa Wizara ya Fedha tujaribu kuangalia mfuko huu na kuuongezea fedha hata kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe pia Wizara kujaribu kuongea na mamlaka nyingine za maji huku kwenye mikoa na huku kwenye halmashauri, waende wakajifunze Tanga kwenye ile green bond, maana lazima tutafute sasa vyanzo vingi vya fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hii ni mingi, hatuwezi kumaliza tu hivi kwa kusubiria hizi fedha bila sisi wenyewe kuanza kubuni vyanzo vingine. Kwa ile green bond, sisi Tanga tumefanikiwa. Uzuri hata gawio sasa hivi linaenda vizuri. Wameshagawiwa takribani mara nne. Kwa hiyo, tutangaze zile, watu wawekeze, tumalize miradi, halafu watu watapata gawio. Kwa hiyo, sasa na wengine waende wakajifunze pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimshauri kaka yangu, Mheshimiwa Waziri Aweso, tumeona pia hapa Waheshimiwa Wabunge wengi wameongea kuhusu kubambikiwa bili za maji na utatuzi mkubwa wa kuondoa kubambikiwa bili za maji, ni hizi mita za kulipia kabla ya matumizi (prepaid meters). Mita hizi ni nzuri, lakini kuna baadhi ya maeneo tutakwenda kukwama kwa sababu ya mitandao. Kwa hiyo, ninaiomba Wizara ya Maji wakae na Wizara ya Mawasiliano kuhakikisha tunapata mawasiliano ya uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi tu pale Tanga nilikuwa na hii mita ya prepaid, Engineer Hill mwenyewe ni shahidi, na mimi niko kilometa sita kutoka pale mjini kabisa katikati ya mji na hakuna mtandao. Kwa hiyo, nikawa nashindwa kuweka, lakini pia Mheshimiwa Engineer Ulenge naye pia hivyo hivyo alikuwa na hii mita, imebidi waje wazifungue.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sasa tuombe Wizara ya Maji wakae na Wizara ya Mawasiliano kuhakikisha mawasiliano yanakuwa sawasawa ili tusije tukakwama kwenye hizi mita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba kaka yangu Mheshimiwa Waziri, ule mradi wa Mkinga - Horohoro sasa hivi uko hatua nzuri na wakati ule Mheshimiwa Rais anapita kwenye zile siku 100 aliahidi tabasamu kwa wananchi wale. Ninawapongeza pia kuna kijiji kimoja pale cha Mtimbwani tayari wameanza kupata maji kama Mheshimiwa Rais alivyoelekeza, ninawashukuru wametekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninawashukuru kwa jitihada walizochukua kwa sababu sasa hivi wamenunua mabomba yote ya mradi mzima shilingi bilioni saba. Kwa hiyo, ninawaomba Wizara twende tukakamilishe ule mradi tuweke nguvu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ninaunga mkono hoja. (Makofi)