Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muleba Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ADONIS A. BITEGEKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Bajeti ya Wizara ya Maji. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo anaifanya ambayo kwa dhahiri ameonesha kwa vitendo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona dhamira yake ya dhati kabisa kuwezesha wananchi wengi kupata huduma ya maji mpaka sasa hivi imefikia 85.2% kutoka 70.1% mwaka 2021 wakati anaingia madarakani. Kwa hiyo, tunashukuru sana kwa sisi wakazi wa vijijini kuona kwamba huduma hiyo imeimarika zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninawapongeza sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri wake na Katibu Mkuu kwa kazi nzuri sana wanayoifanya. Mimi kama Mbunge wa Muleba Kaskazini nimekuwa nikipata ushirikano mkubwa sana kutoka kwao hasa pale ninapofuatilia miradi ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawashukuru sana, kwa kuwa katika miaka mitano iliyopita Jimbo la Muleba Kaskazini lilipata miradi mitano ya maji ambayo yamesaidia sana kuimarisha huduma za maji na kuongeza asilimia ya upatikanaji wa maji mpaka kufikia 81% kutoka 74%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali na mafanikio haya, sisi katika Jimbo la Muleba Kaskazini bado tuna miradi miwili mikubwa ya maji ambayo tunaisubiri. Tuliahidiwa katika mwaka huu wa fedha miradi hiyo itakuwa imetekelezwa (mradi wa maji wa Iroba na mradi wa maji wa Makongora).
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni miradi ambayo wananchi wa Jimbo la Muleba Kaskazini wamenituma niiombe Serikali iweze kuitekeza miradi hii, kwani itasaidia sana kuleta huduma za maji katika wakazi takribani 9,000 katika maeneo hayo na maeneo ya jirani ya vijiji hivyo. Pia tunatarajia kwamba katika mwaka ujao wa fedha tutapata visima vitatu ambavyo vitasaidia sana katika kuboresha huduma ya maji katika Jimbo la Muleba Kaskazini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la msingi ambalo ninaomba niliseme hapa leo ni kwamba katika miradi mitano ambayo imetekelezwa katika Jimbo la Muleba Kaskazini, tuna mradi mmoja wa Kagoma ambao utekelezaji wake umefikia 96% bado asilimia nne kukamilika, lakini bado mkandarasi anadai fedha shilingi milioni 119 ili kukamilisha mradi huo. Tunaomba sana Serikali isimamie ili mkandarasi huyu aweze kulipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali ya kuleta maombi hayo ya Jimbo la Muleba Kaskazini, ninapenda pia kushauri Serikali kwamba ukiangalia dira yetu ya 2050 imetoa kipaumbele sana katika sekta ya binafsi kuweza kuchangia katika kuleta mafanikio ya maendeleo. Ninaamini kwamba maji pia ni uchumi. Ninaamini kwamba ni wakati mwafaka sasa hivi Serikali ikafungua milango kuruhusu sekta binafsi iweze kushiriki katika kutoa huduma ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni suala la msingi sana, tumeona mafanikio kule Tanga kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge aliyetangulia kwamba imesaidia sana uuzaji wa hatifungani. Ninashauri kwamba sisi tufungue pia fursa zaidi kwa wawekezaji waingie kuwekeza katika sekta ya maji ili kusaidia sana katika kuongeza zaidi miradi mingine ya maji, lakini pia kufadhili miradi ya maji. Tumeona pia katika upande wa barabara, Samia Infrastructure Bond imesaidia sana katika kuongeza uwezo wa Serikali katika ujenzi wa barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaamini kabisa sekta binafsi ikishirikishwa, basi tutaweza kufika mbali katika kufanikisha mipango yetu ambayo kimsingi itasaidia sana maendeleo yetu ya sekta ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hili pengine ni jambo la jumla la Kitaifa, nimeona kwamba katika bajeti ya mwaka huu wa fedha 2025/2026 kwamba ilipangwa miradi 1,318 vijijini, lakini mpaka tunafikia mwezi wa nne ni miradi 54 tu imeshatekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba Serikali iongeze nguvu zaidi katika kukamilisha miradi mingine 992 ili tuweze kupata huduma zaidi ya maji na kufikia yale malengo kusudiwa ya kuona kwamba kila kijiji kinapata huduma ya maji ifikapo mwaka 2030. Ninaamini kabisa kwamba kwa mpango kabambe wa Serikali ambayo imeuandaa, tutaweza kufikia yale malengo tarajiwa ya kutoa huduma za maji kwa kila kijiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ninapenda kutumia fursa hii kwa kuwa ninahitimisha pia mchango wangu, ni kwamba ninawashukuru wananchi wa Jimbo la Muleba Kaskazini kwa jinsi wanavyoniamini. Nami ninapenda kuwahakikishia kwamba chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, mimi pamoja na madiwani tutapambania kuona kwamba wanapata maji ya uhakika na usalama katika vijiji vyote.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Bitegeko, ahsante sana.
MHE. ADONIS A. BITEGEKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuunga mkono hoja.