Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Isack Joseph Copriano

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Monduli

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ISACK J. COPRIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru na mimi kwa kupatia nafasi hii ya kuchangia kwenye Wizara hii ya Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miradi ambayo ametupa Wilaya ya Monduli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba tu niseme, kwa sababu dakika tano hizi ni chache, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Maji na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maji na Watumishi wote wa Wizara ya Maji, ninajua wananisikia walioko kule Monduli, Arusha kwa sababu wote wanahudumu kwenye Wilaya ya Monduli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa na ushauri tu kidogo. Mheshimiwa Waziri ningetamani sana kwenye wilaya yangu pasianzishwe miradi mipya. Ninamwomba Mheshimiwa Waziri akasimamie miradi hii niliyopewa na Mheshimiwa Rais, miradi ya vijiji 13. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri, wameweka mguu chini, wametengeneza MoU kati ya Wizara na pipe industry kwa ajili ya ku-produce mabomba yale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefarijika sana na nilipata fursa ya kutembelea, na nimeona mabomba yanaendelea kutengenezwa. Ombi langu ni kwamba, ninajua mara nyingi ninakutana na Mheshimiwa Waziri, na aliniambia, “jambo moja ambalo nitakufanyia ni kuhakikisha vijiji 13 vilivyokuwepo Monduli vinapata maji.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba Mheshimiwa Waziri, vipaumbele visitolewe kwenye miradi mipya, vitolewe kwenye miradi ambayo imeanza kutekelezwa. Itatusaidia sana kuondoa changamoto ya maji kwenye wilaya zetu. Kuna mradi Makuyuni wa vijiji saba ambao unagharimu karibu shilingi bilioni saba. Mradi ule umeanza na tayari ulishapelekewa karibu shilingi milioni 800 pale inaendelea. Ninaomba mradi ule ukamilike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu, kuna mradi kule kata ya Mfereji - Donyonaado wa shilingi bilioni 1.5 umeshapelekewa shilingi milioni 250. Ninaomba mradi ule upelekewe fedha ili ukamilike. Siyo hilo tu, kuna mradi mwingine wa Bwawa la Somweinen, Mheshimiwa Naibu Waziri atakumbuka, alikuja nikiwa Mwenyekiti wa Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkandarasi pale alikuwa anasuasua tukamwondoa na mradi ule sasa unafanyika kwa force account. Ninaomba basi angalau ziongezwe fedha wananchi wale wapate huduma ile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua Wilaya ya Monduli ni wilaya ya kame. Kipindi hiki cha ukame, sisi tulivyopata matatizo mengi ya maji, ninajua kabisa jinsi Mheshimiwa Waziri alivyojitoa, na mimi ninashukuru sana Wizara yake. Juzi tumetukarabatiwa Bwawa la Nanja. Leo tunavyozungumza maji yale wameshayazuia na wananchi wangu wanapata maji. Sasa Bwawa la kule Somweinen likikamilika itanisaidia kupunguza tatizo la maji hususan kwa mifugo na wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri, apeleke fedha kwenye mradi ule unaotekelezwa na USA. Mradi ule umekwama pale msituni kwa zaidi ya miaka mitatu sasa na mradi ule unafanyika kwa force account. Mheshimiwa Naibu Waziri anakumbuka, jana niliuliza swali dogo na akaniahidi kwamba watapeleka fedha. Miradi viporo iliyoko Monduli ikikamilika itaniondolea kesi kubwa na wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nimesimama kumwomba Mheshimiwa Waziri kwa dhati kabisa, na ninajua anatosha kwenye kiti hicho na chenchi inabaki, kwa dhati kabisa ninaomba anipelekee fedha Monduli, wananchi wangu waondokane na tatizo la maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikiwezekana, wakati tunaendelea kutekeleza miradi hii, na kwa kuwa Mheshimiwa Waziri anajua Monduli ina shida ya maji, basi aninunulie hata boza wananchi wangu wachote maji kutoka Arusha kipindi tunatekeleza miradi hii. Itanisaidia sana kupunguza tatizo hili wakati tunatekeleza miradi mikubwa ambayo tumeletewa na Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimwomba Mheshimiwa Waziri tangu muda mrefu, na boza halitazidi hata milioni 300 au 250. Ukininunua boza, wananchi wataweka mafuta, watachangia, na maji yatakuwa yanapelekwa wakati tunatekeleza hii miradi mizuri ambayo kimsingi unaona ni jinsi gani Mheshimiwa Rais amewakumbuka wananchi wa Monduli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nimesimama kuomba sana kwa dhati nisianzishiwe miradi mipya Monduli, tukamilishiwe miradi hii viporo. Nitakuwa na amani na jimbo lile litatawalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo sina mengi, ninakushukuru na kuipongeza na Wizara hii, na niseme tu kazi inayofanyika kwenye wilaya yangu hususan ma-engineer wanafanya kazi nzuri, RUWASA wanafanya kazi nzuri, na AUWSA wanafanya kazi nzuri, ninawapongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, Mheshimiwa Waziri amesimama kidete kusema anawatua ndoo kichwani akina mama wa Monduli. Ninaomba sana kwa dhati aende kukakamilisha miradi hii ili wananchi wangu wakapate huduma ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja kwa 300%, wananchi wangu wapate maji, ahsante.