Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Martha Nehemia Gwau

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. MARTHA N. GWAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa nafasi hii ya kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, ninaomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ushindi mkubwa wa kishindo. Pia, ninaomba nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Emmanuel Nchimbi, Makamu wa Rais, na pia ninaomba nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri Mkuu wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shukrani kubwa kwa Chama changu cha Mapinduzi, na shukrani kubwa zaidi kwa akina mama wa Mkoa wa Singida kwa kunipa kura nyingi za kishindo na kufanya nije hapa Bungeni kwa awamu nyingine ya pili kuwawakilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichukue nafasi hii kupongeza Wizara ya Maji chini ya Mheshimiwa Waziri Aweso kwa kazi kubwa anayoifanya, na chini ya Katibu Mkuu mwanadada mahiri Engineer Mwajuma. Kwa kweli wanafanya kazi nzuri na wanahitaji kupongezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisiwe mchoyo wa fadhila, niwapongeze Mameneja wa Mkoa wa Singida wanaohudumia suala zima la maji. Meneja wa RUWASA, SUWASA, bonde na wale wa Mamlaka ya Miji Midogo, wanafanya kazi nzuri na wanatushirikisha Waheshimiwa Wabunge vizuri katika kuwatatulia wananchi wa Mkoa wa Singida changamoto zao katika suala zima la maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maji ni uhai, maji ni uchumi. Dira ya Taifa ya 2050, Ilani ya Chama cha Mapinduzi na dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kumtua mama ndoo kichwani. Tunakiri tulipo sasa siyo sawa na tulipotoka miaka 10 iliyopita. Kwa hiyo, jitihada kubwa imefanyika, mikakati mingi imefanyika kwa weledi mkubwa kututoa hapa tulipo. Tunashukuru na tusiwe wachoyo wa fadhila, tunashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ushauri au maombi machache kwenye Wizara ya Maji. Ombi la kwanza mikoa inatofautiana. Tuna mikoa ambayo ina changamoto ya vyanzo vya maji, na tuna mikoa ambayo ni kame kama Mkoa wa Singida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wetu wa Singida una changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji ya chini ya ardhi. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali na tunaomba Wizara ya Maji wawekeze kithabiti kuhakikisha kwamba tunapata vifaa vya kisasa ambavyo vitaenda kuchimba chini zaidi ya ardhi ili waweze kupata maji kirahisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto hii inasababisha zoezi la miradi kurudiwa, kutokufanikisha miradi kwa wakati, lakini hata ongezeko la fedha. Kwa hiyo, tunaomba mikoa yetu kame isaidiwe kuwa na mkakati mbadala wa kuhakikisha tunapata vifaa vya kisasa ili tunapofanya mradi tusirudie mara ya pili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunamwomba sana Mheshimiwa Waziri Aweso, pamoja na kazi kubwa anayofanya ila atuangalie mikoa kame isiyokuwa na vyanzo vya maji iweze kuwa na njia mbadala au vifaa vya kisasa vya kutusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni ombi. Tuna vijiji 59 Mkoa wa Singida ambavyo havijawahi kuona maji kabisa, wanatumia maji ya visima vya kienyeji, lakini maji yao siyo salama. Vijiji hivyo ni Mkalama, kuna vijiji sita; Manyoni, vijiji 21; Singida DC ina vijiji vitano; Iramba, vijiji nane, na Ikungi, vijiji 19. Tunaomba Wizara iwekeze sasa kwa wasiyonacho kabisa. Walionacho wasubiri wasiyonacho kabisa ili tuweze kufaidi keki ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Aweso alisema, wote tunatoka vijijini. Kama wote tunatoka vijijini, kuna wanaoongelea maji yanatoka mara mbili kwa wiki, kuna wanaoongelea maji yanatoka mara moja kwa wiki, na kuna yule Mtanzania ambaye hajawahi kuona maji kabisa. Kwa hiyo, tunaomba bajeti hii ya mwaka huu wa fedha iwafikirie wasiyonacho kabisa ili tuweze kuongea lugha moja, hata kama tukiwa na mgao, basi Watanzania wote tuwe nacho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Mheshimiwa Aweso ni msikivu, nina hakika kabisa anaenda kutatua vijiji vyote visivyo nacho kabisa ili wote tupate keki ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Singida tuna mradi wa miji 28 unatekelezwa katika Mji wa Manyoni, Mji wa Singida, Manispaa ya Singida, na Mji wa Kiomboi. Tunaiomba Serikali, imefika hatua nzuri, tunashukuru. Tunaomba mradi huu umaliziwe kwa haraka ili usaidie kutatua changamoto ya maji katika hiyo miji midogo niliyoitaja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mradi wa Ziwa Victoria, nilieleza changamoto ya vyanzo vya maji. Tunaomba na wenyewe ukamaliziwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)