Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aliyetujalia uzima na afya njema. Pia ninampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya kwa kuonyesha nia ya dhati ya kumtua mwanamama ndoo kichwani kwa vitendo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, pia ninampongeza Mheshimiwa Waziri wa Maji, Naibu Waziri wa Maji, Katibu Mkuu, dada yangu Mwajuma pamoja na watendaji wote wa Wizara ya Maji kwa kazi nzuri wanayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, niendelee sana kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Waziri wa Maji kwa kuona umuhimu wa kutenga shilingi bilioni sita kwa ajili ya upembuzi yakinifu ya kutoa maji katika Ziwa Tanganyika na kuyaleta katika Mji wa Mpanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Mpanda ni mji ambao unakua sana na Mkoa wa Katavi ni mkoa pekee ambao umeonyesha katika sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kwamba ni mkoa ambao una ongezeko kubwa sana la watu wanaokuja kutafuta fursa mbalimbali za kibiashara ndani ya Mkoa wa Katavi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, Mkoa wetu wa Katavi ni dhahiri kwamba sasa unahitaji maji ya uhakika na maji ya uhakika ni kutoa Ziwa Tanganyika na kuyaleta katika Mji wa Mpanda kwa ajili ya wananchi waweze kupata maji ya uhakika muda wote na wakati wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutamani jambo zuri siyo mbaya kwa sababu, kama imewezekana kwa kutoa maji Ziwa Victoria na kuyaleta katika Mikoa ya Tabora mpaka Dodoma hapa tunaambiwa wanakuja, tunaamini na sisi wananchi wa Mkoa wa Katavi, Rukwa pamoja na Kigoma, mradi huu wa kutoa maji Ziwa Tanganyika unawezekana katika eneo letu na sisi tuweze kupata maji ya uhakika na maji salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee sana kumwomba Mheshimiwa Waziri wa Maji katika Kata ya Maji Moto Halmashauri ya Mpimbwe tunao mradi wa maji ambao kwa kweli unahitaji tuweze kupata chujio. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kabisa kipindi cha masika ambapo mvua zinanyesha, wananchi wale hususan akina mama, wamekuwa wakipata taabu sana kutokana na kwamba tu hatuna chujio. Wamepata maji yenye tope kutokana na ukosefu wa chujio, na kipindi cha masika kutokana na mvurugiko mkubwa wamepata maji ambayo siyo majisafi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri aweze kututengea fedha, atuletee, ili wananchi wa Kata ile ya Mamba waweze kupata maji ya uhakika. Pia ninaomba usambazaji wa maji kutoka Mamba kwenda Mbede na maeneo ya Kasansa mpaka Ikuba. Hili likifanyika, itawasaidia sana akina mama wale wa Mkoa wa Katavi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, akina mama wale wamenituma, wanaomba sana Mheshimiwa Waziri aweze kuwapatia fedha kwa ajili ya usambazaji. Hata hivyo, kikubwa zaidi ni chujio ili akina mama wale na wenyewe waweze kupata maji ya uhakika. Tunatambua panapokuwa na changamoto ya maji wanaopata changamoto kubwa sana ni akina mama. Kwani wamekuwa wakihangaika mpaka usiku kwenda kuhakikisha kwamba wanatafuta maji safi na salama kwa ajili ya familia zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anatambua maji hayana mbadala. Ni wakati sasa wa Taifa letu kutupia sana jicho katika Wizara ya Maji. Tunatambua kwamba, kwa kuwa maji hayana mbadala, mtu anaweza akawa hana umeme, lakini akaishi. Hauwezi ukaishi kama majisafi na salama hayapatikani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, ninaiomba sana Serikali yangu, ni muda sasa na wakati wa kuweza kuwaongezea fedha Wizara ya Maji kwa kuwa maji hayana mbadala ili sasa tuweze kutatua changamoto ya maji. Kwani tunatambua ni zaidi ya vijiji vingi sana ambavyo havina kabisa maji, hawajawahi kupata historia ya maji wala hawajawahi kuona maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri pamoja na watendaji wako, lakini tunaiomba sana Serikali hususan Wizara ya Fedha, ni muda sasa na wakati wa kuhakikisha kwamba Wizara hii inakuwa ya kipaumbele. Sote tunajua maji ndiyo yenye umuhimu. Hata mtu anapopoteza maisha, tunatambua kwamba huwezi ukapelekwa kupumzishwa katika makazi yako ya milele bila kuoshwa. Hapa pote tunaona tunatumia maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, kwa kuwa wote tunajua umuhimu wa maji, mama akijifungua yanahitajika maji. Kwa hiyo, tunaona maji ni kitu muhimu sana na hakina mbadala wowote. Ni muda sasa wa Wizara hii iweze kuongezewa fedha kwa ajili ya kutatua changamoto za maji na miradi mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana, ninaunga mkono hoja, na ahsante sana. Maji hayana mbadala. (Makofi)