Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia. Ninaomba nimtangulize Mwenyezi Mungu katika mchango wangu. Pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ambayo ameendelea kuifanya na kuhakikisha wanawake wanatuliwa ndoo kichwani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nimpe pongezi nyingi sana Mheshimiwa Waziri Jumaa Aweso, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, dada yetu Eng. Mwajuma kwa kazi nzuri ambayo wameendelea kuifanya katika Wizara hii ya Maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimpongeze pia Meneja wa Mkoa wa Iringa wa RUWASA pamoja na IRUWASA, kwani wamekuwa msaada sana katika mkoa wetu katika hii miradi ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Kilolo wanaendelea pia kumpongeza Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, tumepata miradi 40 ambayo imeweza kusaidia vijiji 46 katika Wilaya yetu ya Kilolo. Hata hivyo, wananchi zaidi ya 246 wameweza kufaidika na miradi ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Kilolo bado vijiji 20 havijapata maji. Kwa hiyo, ninaomba sana Mheshimiwa Waziri, hivi vijiji 20 viweze kufikiwa na miradi ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao ujenzi wa miradi ya maji inayoendelea kutekelezwa. Mradi wa Maji wa Kihesa Mgagao, Masege na Masalali, huu mradi umeshafika zaidi ya 80%, lakini mkandarasi anadai shilingi bilioni 1.2. Kwa hiyo, tunaomba Mkandarasi alipwe ili huu mradi uweze kusaidia wananchi kwa vijiji vilivyobaki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, upo mradi ule wa Ng’ang’ange ambao Naibu Waziri alikuja pamoja na Makamu Mwenyekiti wakati huo Mheshimiwa Anna Lupembe, wakasaini huu mradi. Sasa mwaka mzima bado wananchi hawajapa maji. Kwa hiyo, tunaomba huu mradi pia ukamilike ili wananchi waweze kupata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao Mradi wa Kisima, ule tumeuita Injinia Mwajuma kwa sababu ni mradi ambao tulipewa wakati wa Siku ya Wanawake, bado tu usambazaji. Tunaomba Injinia Mwajuma aje sasa kwenye ule mradi ili maji yaweze kusambazwa, wananchi waweze kupata maji. Tunao mradi mwingine wa Ikula. Hii ni tank tu, shilingi milioni 200 tu wakipewa wananchi wa Ikula watapata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao pia mradi wa kuboresha maji katika Mji Mdogo wa Kilolo, gharama yake ni shilingi milioni 800, na huu mradi umeshafikia 95%. Kwa hiyo, tunaipongeza Serikali, tunaomba tu waweze kutupatia fedha ili mradi uweze kukamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunao mradi wa kuboresha maji Mji Mdogo wa Ilula. Huu ni mradi wa shilingi bilioni 1.3, na 70% tayari. Kwa hiyo, tunaipongeza Serikali kwa kazi nzuri, lakini tunaomba miradi hii sasa ikamilike kwa wakati ili wananchi sasa waweze kufaidika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba, kwa kuwa miradi hii imesimama kutokana na wakandarasi kutolipwa vyema, tunaomba sasa Serikali ifanye utaratibu, Wizara ya Maji iongezewe fedha ya kutosha na pia tuangalie na vyanzo vingine ili wananchi wote waweze kupata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Martha hapa amesema maji ni kila kitu. Kila kitu kinahitaji maji. Kwa hiyo, tunaomba Serikali iangalie Wizara ya Maji, fedha zote zinazotengwa zipelekwe kwa wakati ili miradi iweze kukamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti hata hivyo, tunaomba tuongeze nguvu kwenye utunzaji wa vyanzo vya maji, kwa sababu vimeharibiwa sana. Hivi vyanzo tusipovitunza, basi hatutapata maji ya uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kilolo IRUWASA gari ni shida, barabara hazipitiki, wananchi hawafikiwi, miradi haikaguliwi kwa sababu hawana maji. Tunaomba gari katika Wilaya ya Kilolo, IRUWASA waweze kufanya kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeweza kushika shilingi, lakini ninawapenda sana wake wa Mheshimiwa Waziri, tena wote ni rafiki zangu, siwezi kuchukua mshahara wake, kwa sababu kwanza anafanya kazi nzuri sana. Kwa hiyo, ninaomba Mheshimiwa...
MBUNGE FULANI: Unawapenda wake zake? (Kicheko/Makofi)
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Ndiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sitachukua mshahara, ila ninakuomba miradi ambayo tayari wakandarasi wpo, walipwe ili miradi iweze kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja na Mwenyezi Mungu awabariki, ahsante sana. (Makofi)