Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Daniel Awack Tlemai

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Karatu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi ya kuweza kuchangia Wizara hii ya Maji, na pia ninatoa shukrani kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miradi mikubwa ambayo anatupatia sisi watu wa Jimbo la Karatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninamshukuru Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, watumishi wote wa Wizara ya Maji na pia watumishi wote ngazi ya Mkoa wetu wa Arusha na pia katika Jimbo langu la Karatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ametembelea Jimbo la Karatu mara nyingi na Naibu Waziri na changamoto kubwa katika Mji wa Karatu katika eneo la Mjini, Mamlaka ya Mji wa Karatu, Mheshimiwa Waziri anajua. Kuna bwawa pale linasumbua na kwenye lile bwawa kuna visima vitatu, ikifika kipindi cha masika tunapata changamoto kubwa sana ya wananchi wa Jimbo la Karatu katika Mji wa Karatu kukosa maji. Hilo Waziri na Naibu Waziri ni mashahidi, na pia Katibu Mkuu ni shahidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa visima vitatu vilivyopo katika eneo la bwawa lile la mjini, limepata changamoto tena kubwa. Sasa ombi langu ni nini kwenu ninyi Waziri na Naibu Waziri?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuja kuchimba visima vitatu, na kutokana na jiografia ya hali halisi ya Jimbo lile katika eneo la mjini, visima vile vitatu vimeonyesha vina maji lita 200,000 kwa saa na inaweza kupeleka kupunguza changamoto ya maji kutoka 52% kwenda 89%, mkitupatia fedha shilingi bilioni 2.7% na hilo mkifanikisha kwa maji, tunapanda kutoka 52% katika Mji wa Karatu kwenda 89% katika eneo la Mji wa Karatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo ni ombi kubwa la wananchi wa Jimbo la Karatu, na Waziri ni shahidi, na Wizara imetusaidia kuchimba mitaro ili kuokoa bwawa lile lisiendelee kuathiri wananchi wa eneo la mjini, na pia kuathiri nyumba za watu katika katika Mji wa Karatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa kupitia wananchi wa Jimbo la Karatu, mtupatie shilingi bilioni 2.7. Mheshimiwa Waziri ni shahidi, mwaka 2022 tuliweza kukaa vikao katika Jimbo la Karatu, alisema atatoa shilingi bilioni 4.5, hakufanikisha lile zoezi la shilingi bilioni 4.5. Akitoa shilingi bilioni 2.7 itakuwa imefikia azma ya wananchi wa Jimbo la Karatu kupata maji kwa 89% na atakuwa ametimiza ahadi yake ya mwaka 2022 kwa wananchi wa Jimbo la Karatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu miradi ya upande wa vijijini RUWASA, upatikanaji wa maji katika Jimbo la Karatu ni 82%, tunaishukuru Serikali lakini tuna ombi. Kuna wakandarasi ambao tayari wako kazini, wameomba fedha na wameandika certificate. Kwa mfano, kuna Kijiji kimoja kinaitwa Qorong’aida ambacho mkandarasi ameomba shilingi milioni 176. Pia, kuna Kijiji kinaitwa Mangisa - Jobaj ambacho mkandarasi ameomba shilingi milioni 255; kuna Kijiji cha Mang’ola Juu, mkandarasi ameomba shilingi milioni 85; na Kijiji cha Matala Endanyawet mkandarasi ameomba shilingi milioni 510. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kuna changamoto katika Tarafa ya Mbulumbulu vijiji vinne na RUWASA imejaribu kuchimba maji katika Kijiji cha Slahhamo imeshindwa kupata maji. Imechimba maji katika Kijiji cha Upper Kitete imeshindwa kupata maji katika vijiji vile; na kuna Kijiji kingine hiki cha Kitete, na Kijiji kingine cha Lositete. Ukanda huu ni mwambao ambao unaendana na ukanda wa Mto wa Mbu ambao uko juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Wizara ione namna ipi nzuri sasa ya wananchi wale wa vijiji vinne ambavyo viko kwenye Tarafa ya Mbulumbulu Kata ya Mbulumbulu ambavyo vina changamoto kubwa, na Wizara imechimba mara kadhaa na maji yamekosekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru na niseme kwamba, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Karatu tunaomba, haya ni maombi yao ambayo nimeyawasilisha mbele yako Seriksli iyazingatie kupitia Wizara, itupe ridhaa ya kutangaza sasa, miradi hii ya shilingi bilioni 2.7, Wizara itoe kibali cha kutangaza katika mji wa Karatu ili wananchi wa Mji wa Karatu waweze kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ninashukuru kwa nafasi na ninaunga mkono hoja. (Makofi)