Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Aysharose Ndogholi Mattembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hoja hii muhimu ya Bajeti ya Maji. Nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kibali cha kusimama katika Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii pia kuwapongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Maji, Naibu wake, Mheshimiwa Eng. Kundo na Katibu Mkuu kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuhakikisha wananchi wanapata majisafi na salama. Ninawapongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nitumie nafasi hii kuwashukuru sana wanawake wa Mkoa wa Singida kwa kunichagua kwa kura nyingi na kuniwezesha kurudi tena Bungeni. Ninaomba niwahakikishie wanawake wa Mkoa wa Singida, nitawatumikia kwa nguvu zangu zote na moyo wangu wote, kuhakikisha Singida inapaa kwa maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ni kinara namba moja wa kumtua ndoo mwanamke kichwani na kwa mageuzi makubwa aliyoyafanya katika Wizara hii ya kuhakikisha wananchi wanapata majisafi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo, ninaomba sasa nijielekeze moja kwa moja kwenye mchango wangu. Nianze na gridi ya Maji ya Taifa. Ninaipongeza sana Serikali kwa kuja na mpango mkakati huu wa kumtua ndoo mwanamke kichwani kwa kutumia vyanzo vya maji vya maziwa na mito kuhakikisha changamoto ya maji inamalizika kabisa nchini. Ninaipongeza sana Serikali. Ninampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wangu wa Singida, Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria umeshafika katika Mji wa Shelui. Ninaiomba sana Serikali, usanifu unaoendelea katika mradi huu wa Ziwa Victoria, uzingatie mahitaji yote kwa wananchi wa Mkoa wa Singida, kwa kuwa endapo mradi huu utakamilika, nina hakika kabisa wananchi wa Mkoa wa Singida watapata majisafi na salama kwa uhakika. Kwa hiyo, ninaomba hilo lichukuliwe kwa jicho la tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kulichangia ni suala la Mradi wa Maji wa Miji 28. Katika Mkoa wangu wa Singida, Mradi huu unatekelezwa Kiomboi, unatekelezwa Singida, na unatekelezwa pia Manyoni. Ninashukuru sana kwa Manyoni mradi huu umefikia 80%, lakini kwa Mradi wa Mji wa Singida na Mji wa Kiomboi, kwa kweli bado kuna changamoto. Ninaomba sana, Mheshimiwa Waziri ni msikivu, mradi huu sasa uweze kukamilika, kwa kuwa miji hii ya Kiomboi, Singida na Manyoni inakua kwa kasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ningependa kulichangia ni uhaba wa vitendea kazi. Jiografia ya Singida ni kubwa sana. Ninaomba sasa watendaji wetu wa RUWASA waweze kupata magari. Wanatembea na pikipiki, umbali ni mrefu kutoka kijiji kimoja kwenda kijiji kingine, ili sasa miradi hii iweze kukaguliwa kwa kina na iweze kufanyika kwa uhakika, ni lazima magari yawepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya kama Ikungi, Wilaya ya Singida Vijijini, pamoja na Manyoni hawana kabisa magari. Ninaomba katika bajeti hii tuliyotengewa, magari yaweze kupatikana ili kazi hizi ziweze kufanyika kwa uhakika kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kulichangia ni kuishukuru sana Serikali kwa miradi ambayo tumeipata, na miradi hii imetumia zaidi ya shilingi bilioni 10. Mradi wa Maji Tulya, Mwangeza, Msingi, Makuro, Mpambaa, Kinangali na miradi wa maji wa vijiji 11 wa Kintinku, Lusilile lakini ipo miradi ambayo imekamilika, na miradi mingine haijakamilika na ukiuliza ni kwa nini miradi hii haijakamilika? Unaambiwa wakandarasi hawajalipwa madeni yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na Waheshimiwa Wabunge wote kwamba Wizara hii iongezewe bajeti ili sasa wakandarasi wetu waweze kulipwa madeni yao na miradi hii iweze kukamilika kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuwapongeza sana watendaji wa RUWASA wa Mkoa wa Singida wakiongozwa na kaka yangu Said kwa kazi nzuri na kubwa wanayoifanya katika Mkoa wangu wa Singida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ninaunga mkono hoja. (Makofi)