Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Charles Mhando Njama

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Korogwe Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. CHARLES M. NJAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kulipa nafasi. Awali ya yote nianze kwa kuipongeze sana Serikali chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa namna ambavyo imeendelea kukamilisha adhima yake ya kumtua mama ndoo kichwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sisi watu wa Korogwe Mjini tunayo miradi miwili mikubwa ya maji. Tunao Mradi wa Miji 28, ambapo mradi huu ni tegemeo kubwa na tumaini lililojaa kwa wananchi wa Jimbo la Korogwe Mjini kwamba sasa tunakwenda kusahau changamoto ya maji Korogwe Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tunao mradi wa Ndemaha. Mradi huu nao utakwenda kutusaidia kuongeza wingi wa maji katika Jimbo letu. Pamoja na miradi hii miwili, tunafahamu kumekuwa na changamoto kwa kiasi, hasa katika mradi wetu wa Miji 28 kwa kuwa tulitazamia kupata maji katika Jimbo letu la Korogwe na kuanza kuyapokea mwezi wa Nne, lakini katika ufuatiliaji inaonekana tutayapata mwezi wa Saba. Bado tuna matumaini makubwa, kwamba mradi huu utakamilika na tutapata maji haya kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wetu wa Mto Ndemaha, bado unasuasua sana. Ninamwomba kaka yangu Waziri Aweso atusaidie, twende tukaukamilishe mradi huu ili kuhakikisha kwamba maeneo yote ya Jimbo la Korogwe Mjini, katika kata zetu zote 11, tuna uhakika wa kupata maji yanayotosha, ambayo ni safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa Jimbo la Korogwe Mjini tuna wasiwasi. Pamoja na miradi hii mikubwa, ambayo tuna uhakika ikikamilika tutapata maji takribani cubic meter za ujazo milioni 16 ambapo ukilinganisha na uhitaji wetu wa sasa wa milioni saba, tutakuwa na ziada ya takribani lita milioni tisa ambazo tunaamini hatutakuwa na changamoto ya maji ndani ya miaka 25 hadi 30 ijayo katika Jimbo letu la Korogwe Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, changamoto ambayo tunaiona mbele yetu ni wasiwasi wa kuwepo kwa upotevu wa maji baada ya maji haya kukamilika kufika katika Jimbo letu la Korogwe Mjini. Hii ni kwa sababu, miundombinu ya maji tuliyokuwa nayo katika Jimbo la Korogwe Mjini, mingi ni chakavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafahamu Wizara inao mpango wa kwenda kurekebisha miundombinu ile ili kuhakikisha kwamba upotevu wa maji tunaukabili iwezekanavyo. Ninamsihi Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake, tukaweke kipaumbele katika kukarabati miundombinu hii, ili maji yatakapofika hasa haya ya miji 28, tusiwe na upotevu wa maji katika eneo lile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ile nia ya maji kufika kwa wananchi iweze kukamilika. Tusije tukawa tuna maji mengi lakini wananchi wanashindwa kupata maji kwa sababu ya miundombinu ambayo imekuwa chakavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuongelea upotevu wa maji katika ujumla wake kama nchi, ninaona kama tunayo fursa kubwa ya kwenda kuimarisha huduma ya maji katika jamii. Takwimu zinaonesha kwamba takribani 35% ya maji yanapotea, ukiya-quantify katika fedha, ni takribani shilingi bilioni 240. Ukiangalia bajeti yetu ya mwaka huu, ambayo ni shilingi trilioni 1.12, kiasi hiki kinachopotea, ni karibia 22% ya bajeti ambayo tunaenda kuipitisha mwaka huu. Maana yake ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza hatuwezi kurudisha gharama za uzalishaji wa maji ambazo tunazitumia. Ukiangalia kwa hii 35% inayoongelewa ya upotevu, kama ni sahihi, maana yake ni kwamba katika kila shilingi 100 ambayo unaitumia kuzalishia maji, shilingi 35 zinapotea njiani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukiweza kwenda kukabiliana vizuri na changamoto ya upotevu wa maji, tunao uwezo wa kuipunguzia Serikali mzigo wa kuendelea kuingiza fedha katika bajeti hii, na Wizara hii ikawa na vyanzo vya kuweza kuisaidia ku-fund bajeti yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninamwomba Mheshimiwa Waziri, na nimeona namna ambavyo amekuwa mkali katika eneo hili la upotevu wa maji, na ameleta transformation nyingi katika Wizara hii ya maji, ninaamini na hili tunao uwezo wa kwenda kulikabili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja, na ninakushukuru tena kwa nafasi.