Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Musa Godfrey Mbuga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisesa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. MUSA G. MBUGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kupata nafasi hii. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema zake na rehema zake. Baada ya kumshukuru Mungu, niipongeze na kuishukuru sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa fedha nyingi ambazo zimekuja kwenye Jimbo la Kisesa na kwa miradi yote ambayo inaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kisesa tumepata shilingi bilioni 6.9, ambayo ni kwa ajili ya miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mradi wa Inonelwa ambao una shilingi bilioni tano, na Mradi wa Mwashata ambao una shilingi bilioni moja, na Mradi wa Mbalagane, Semu ambao una shilingi milioni 592. Miradi hii yote, mingine inaendelea na mingine imeshakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninashukuru sana kwa juhudi za Serikali, na ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri Aweso pamoja na Mheshimiwa Eng. Kundo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, dada yetu Mwajuma, lakini pia ninawapongeza RM wa Simiyu Lufwetula pamoja na DM wa Meatu, ndugu yangu David Kaijage kwa kazi nzuri na kubwa ambayo wanaifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati ninapitia hii bajeti, nimevutiwa sana na jinsi ambavyo wameiweka kwamba asilimia saba inaenda kwenye matumizi ya kawaida na 93% inaenda kwenye maendeleo. Maana yake 93% inaenda kumtua mama ndoo kichwani, Wizara ya Maji hongereni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, nimepata wasiwasi sehemu moja. Ukiangalia kwenye fedha za maendeleo shilingi 1,039,000,000, financing structure yake ni 38.5% tu ndiyo ambayo inatoka kwenye fedha za ndani. Inanipa mashaka kidogo, na 61.4% ni fedha za nje. Ukiangalia Kamati wameelezea pia hiki kitu. Ninapata wasiwasi namna ambavyo hii miradi mikubwa ambayo tunategemea itekelezwe, kama kweli itaenda kutekelezwa kwa kiwango hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba Mheshimiwa Waziri, atakapokuja kwenye majumuisho, atoe ufafanuzi vizuri. Je, 38.5% ya mapato ya ndani peke yake ndiyo yanayoenda kwenye utekelezaji wa miradi. Kweli tutatoboa? Kama anavyosema kwamba wali wa kushiba unaonekana kwenye sahani, kwa wali huu, mimi ninaona hatushibi. Kwa hiyo, kuna haja ya kutazama vizuri kwenye eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati pia imeonesha kwamba upatikanaji wa fedha hizi ni 74.3%. Sasa ninajiuliza kama 38% kwa 61% na bado upatikanaji ni 74.3%, kwa hiyo, kuna maeneo ambayo yanatupa mashaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Wizara ya Fedha, kwanza ninaunga mkono hii bajeti. Pamoja na kuunga mkono, nishauri kwamba, ni vizuri wakandarasi wapewe kipaumbele, madeni ya wakandarasi yapewe kipaumbele ili waweze kurudi site.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo miradi Kisesa ambayo imesimama kwa sababu wakandarasi wanadai. Upo mradi wa Mwashata, mkandarasi anadai shilingi milioni 234. Upo mradi wa Mwasengela, Lingeka pamoja na Mwakasumbi, mkandarasi anadai shilingi milioni 114. Ninaomba, baada ya hii bajeti kuwa tumeipitisha, kipaumbele cha kwanza tunaomba wakandarasi wakalipwe madeni yao ili hii miradi iweze kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, Mheshimiwa Rais amenunua mitambo kwa kila mkoa kwa ajili ya kuchimba visima, lakini ninaona speed haiendani na shauku ya Mheshimiwa Rais. Kwa mfano, kwenye Jimbo langu la Kisesa, tangu hii mitambo imekuja, ni visima vitano tu ndivyo ambavyo vimechimbwa, kati ya hivyo vitano, ni vitatu tu ndivyo ambavyo vinatoa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Wizara iunde Kamati, au iunde Kitengo cha Evaluation, ili kuweza kufanya tathmini, lakini mwisho nimalizie kwa kusema, Mradi wa Ziwa Victoria ndiyo ambao utatusaidia kwa Meatu na Kisesa kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja, ahsante sana.