Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Khalid Mussa Nsekela

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kyerwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. KHALID M. NSEKELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa nafasi hii niweze kuchangia hoja ambayo iko Mezani. Kwanza nimshukuru Mheshimiwa Rais na kumpongeza kwa kazi kubwa na juhudi za makusudi za kumtua ndoo mama kichwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nitoe pongezi kubwa sana kwa Mheshimiwa Waziri na timu nzima ya Wizara ya Maji kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya, lakini kwa wasilisho zuri sana la bajeti ambayo siyo tu kwamba inaonesha namba kwenye jedwali, lakini ni bajeti ambayo inaakisi maono ya Mheshimiwa Rais na Dira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikiliza vizuri na kuisoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri. Ukiangalia hii bajeti ya Wizara ya Maji ni bajeti ambayo inamgusa kabisa mwanamama ambaye anatembea kilometa zaidi ya tano kufuata maji saa 11 asubuhi. Pia ni bajeti ambayo inamhusu kabisa mwanafunzi ambaye anakosa masomo akiwa kwenye harakati za kwenda kuchota maji. Vilevile, ni bajeti ambayo inamhusu mkulima na mfugaji ambaye anategemea majisafi na salama na wingi wa maji katika uzalishaji wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti ukiangalia takwimu za Tanzania kutoka World Bank, ni kwamba tume-improve sana katika suala la kupata majisafi na salama. Ni 30% mpaka 40% ya wananchi wana majisafi na salama, 70% mpaka 85% wana maji ya msingi, lakini kwenye takwimu hizi kwa mimi ambaye ninatokea Kyerwa, bado ninakuwa na ugomvi nazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru kwa kazi kubwa inayofanyika. Kuna miradi ambayo inagusa vijiji 21 na nimeona kwenye bajeti fedha zimetengwa, ambazo zitaenda kukamilisha miradi hii. Ukiangalia idadi kubwa ya Vijiji vya Kyerwa bado tunategemea maji ya visima, maji ya chemchem na maji ya mvua ambayo hayana uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi ninaomba nitoe rai kwamba, bajeti tumeiona, lakini tunaomba fedha hizi zitoke mapema. Nimwambie Mheshimiwa Waziri kwamba, mafanikio ambayo anataka ayaone, na nimeona jitihada zake zilivyo, ni mafanikio ambayo yatakuwa na maana pale yatakapokuwa yamemgusa mwananchi wa kawaida, hasa mwananchi wa kijijini, vikiwemo Vijiji vya Kyerwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili ninaomba nitoe rai kwamba, vile vyombo vya watumia maji vya vijijini vijengewe uwezo, vipewe nguvu na viwajibishwe katika kukusanya mapato na kusimamia miradi. Hapa ninaomba kidogo Mheshimiwa Waziri aniazime masikio yake kwa sababu, kuna siku niliuliza swali la Mradiwa Kigorogoro, Rulamana Kashandana Mheshimiwa Naibu Waziri akanipa majibu kidogo, ambayo sikuridhika nayo, lakini nikaona nifanye kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetembelea mradi ambao uko Kigorogoro, Kata ya Kibale, ule mradi umejengwa 2009. Ule mradi uko kilometa tano kutoka makazi ya watu, uko msituni, lakini tenki la maji limejengwa kilometa 12 kutoka kisima kilipochimbwa. Sasa unaweza ukaona kwamba, tayari usalama wa mradi ni shida kwa sababu, uko msituni, lakini una gharama kubwa ambayo inatumika ku-pump maji kilometa 12 kutoka kwenye kisima kuja kwenye tenki la maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Kibale, Kigorogoro, Rulama na Kashanda wameji-commit. Nimeongea nao wanasema wao hawakushiriki kuharibu mradi, kama ilivyojulikana toka mwanzo, na mimi kwa niaba yao ninaomba, sasa wameahidi kwamba, wako tayari, wanaomba Serikali sikivu ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan iwapelekee mradi wa maji kwa sababu, miaka mingi hawana majisafi wala hata maji ya msingi hakuna. Kwa hiyo, wanaomba, na wako tayari kutoa ushirikiano wa kutosha wakipata kisima cha maji pale kwenye Kata ya Kibale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ninaomba nitoe rai kwamba, ni muda mwafaka sasa, wakati Wizara ya Maji inafanya kazi kubwa kusambaza majisafi na salama kwa wananchi, na kuna haja ya ushirikiano mkubwa sana na Wizara ya Nishati, nikimaanisha TANESCO, kwamba, wasambaze umeme pale pote kwenye miradi ambapo inapelekwa kwa sababu, ukienda Jimbo la Kyerwa, miradi mingi ipo sehemu, hakuna umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali inaingia gharama kubwa sana kwenda kuvuta yale maji kwa kutumia sola. Kama hakuna mvua, maji hakuna, kwa sababu, changamoto nyingi ambazo zinatokea kwenye shida ya maji ni uhakika wa maji. Miradi ipo, lakini uhakika hamna, umeme hamna, sola ina shida, mvua imenyesha, watu hawana huduma ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mwisho kabisa, kuna Mradi wa Kuvuta Maji kutoka Mto Kagera ambao unakwenda kugusa Kata ya Nyaruzumbura, Kyerwa, Nyakatuntu, Businde, Bugarana Kamuli, ambao utahudumia vijiji 21. Ninamwomba Mheshimiwa Waziri, hili suala la wanakijiji wa Kyerwa au Kyerwa kwa ujumla watashukuru watakapoona kuna jitihada za msingi zinafanyika ili mradi huu uweze kukamilika. Ninashukuru sana.