Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Patrick Adkin Mwalunenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbeya Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. PATRICK A. MWALUNENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa fursa hii na mimi kuchangia Bajeti yetu pendwa ya Wizara ya Maji. Kwanza, kabisa ninampongeza Mheshimiwa Rais kwa dhamira yake ya dhati ya kumtua mama ndoo kichwani na amejipambanua wazi kwa kutenga bajeti kubwa, kuiwezesha Wizara ya Maji, shilingi trilioni moja na kitu, dhamira yake ni njema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niko Jimbo la Mbeya Mjini. Mheshimiwa Waziri anafahamu Jimbo la Mbeya Mjini, kwa maana ya Jiji la Mbeya. Tuna changamoto ya maji, lakini tunaamini ule Mradi wa Kiwira utakuwa ndiyo solution, kwa sababu, una uwezo wa kutoa lita zaidi ya milioni 117. Zaidi ya watu milioni 1.5 wataweza kunufaika na ule mradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo, ninamwomba Mheshimiwa Waziri, apelike speed ule mradi ukamilike ili watu wa Mbeya Mjini na wilaya nyingine waweze kunufaika. Tumezungumza mara nyingi changamoto za pale na amenihakikishia kwamba, ataziondoa ili ule mradi aweze kuendelea, na watu wetu wapate maji. Kwahiyo, ninamwomba sana ndugu yangu Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema wazi, katika biashara rahisi kuifanya duniani ni biashara ya maji. Sasa sielewi tunakwama wapi? Hata tuki-involve private sectors. Ninashukuru, kwenye hotuba wamesema kwamba, sasa tutazi-involve private sectors na financial institutions ku-facilitate hii miradi ya maji. Hilo ni jambo bora, nina uhakika tunaenda kufanya mapinduzi makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, angalia kampuni ngapi zinazalisha maji ya kunywa? Ni lita na lita zinapita kwa malori na malori. Hawawezi kushindwa wale watu. Kama tutawawekea mazingira mazuri ya kufanya miradi mikubwa ya maji, tutaipunguzia Serikali kazi nzito ya kutafuta fedha na hasa kwenye miji mikubwa, ibaki kuhangaika kutafuta pesa kwa ajili ya vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halmashauri na majiji ambayo yana uwezo wa mapato, tuangalie namna nyingine ya kuhakikisha kwamba hawa watu wanakuwa financed na private sectors na benki, ili tuweze kutatua miradi ya maji. Kuanzia jana wachangiaji wote wanaona kwamba, maji yana umuhimu, kila Mbunge, lakini ninaona shida mnayoipata ni upatikanaji wa fedha na dhamira ya Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu wake na watendaji wote, nikiwaangalia usoni na mioyo yao ni kuhakikisha kwamba, wanamtua mama ndoo kichwani. Tatizo liko kwenye upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba, kwanza waanze kubana matumizi. Nimeona kwenye bajeti yao, sehemu kubwa ya fedha inaenda kwenye miradi, waendelee hivyo hivyo. Pia, waendelee kubana zaidi matumizi ili fedha iende kwenye miradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajua Waziri wa Fedha yuko hapa, Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuwa Waziri wa Fedha, anafahamu ni kiasi gani cha fedha kinatumika kwenye kununua magari kwa watumishi wa umma. Hebu tujibane kama Serikali, angalau kwa miaka miwili. Hakuna mtumishi wa umma atakayeugua kwa kukosa gari jipya, lakini watu wataumwa kwa kukosa maji. Tuangalie ni kiasi gani cha fedha kinatumika kununua magari mapya kila mwaka, ile fedha tuipeleke kwenye miradi ya maji, tuisaidie Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wako wawekezaji mbalimbali wanakuja kuwekeza kwenye nchi yetu, wanakuja kuwekeza kwenye migodi na biashara kubwa. Tuwabane wale iwe kama sehemu ya condition, wanapokuja kuwekeza hapa, basi wawekeze pia kwenye miradi ya maji, iwe kama, sehemu ya kutoa CSR kwenye jamii yetu. Nina uhakika tutaisaidia Wizara yetu na maeneo mengi yatapata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Mji wa Chunya unazalisha dhahabu pale, lakini maji hakuna. Ni jambo la kusikitisha sana. Kwa hiyo, tuangalie mechanism nzima, kama Serikali, kuangalia ni jinsi gani tunaisaidia Wizara ya Maji iweze kupata fedha na kuweza kuhudumia wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusiana na miamala ya simu. Ni kweli kabisa inatusaidia na kila mtu hapa akiamka asubuhi, akinawa uso, amepiga mswaki na maji, anakwenda kwenye simu, kununua vocha ya shilingi 500 au shilingi 1,000, na kwenyewe tuangalie ni shilingi ngapi miamala, inaweza ikachangia kuleta fedha kwenye Mfuko wetu wa Maji ili Wizara ya Maji iweze kupata fedha na kutekeleza miradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri hapa amesoma hotuba, ni nzuri na ina matumaini makubwa sana kwa wananchi, lakini bila fedha hawezi kutekeleza ile miradi. Ninatamani kuona Bajeti ijayo mwakani, asiyongee tena habari ya miradi ambayo haijakamilika; Bwawa la Kidunda, Bwawa la Kiwira, kutoa maji kwenye gridi ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana. Ninaunga mkono hoja, ahsante.