Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi ninashukuru kwa kunipa nafasi, ili niweze kutoa mchango wangu kwenye Wizara ya Maji. Ninampongeza sana Mheshimiwa Aweso kwa kazi nzuri ambayo anaifanya. Ninaamini ameona kila Mbunge alivyosimama hapa ametambua namna ambavyo amekuwa kijana mchapakazi na msikivu. Kwa hiyo, tunampongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Waziri anafungua hotuba yake, amegusia Mradi wa Maji wa Mto Momba na ninajua, hata nilivyosimama hapa, Mheshimiwa Waziri anajua kabisa kwamba, ninazungumzia Mradi wa Mto Momba. Yapo mambo mengi sana ambayo Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita, Mama yetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameyafanya ndani ya Mkoa wa Songwe na ametuandikia historia kubwa, ambayo kwa kweli, haitakaa ije ifutike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo kubwa mojawapo ambalo Mheshimiwa Rais ametufanyia ni kutuletea Mradi wa Maji wa Mto Momba. Mradi huo ni mkubwa sana na ni mradi wa kimkakati. Mkoa wa Songwe tumekuwa tunaiomba sana Serikali kuweza kupata mradi wa kimkakati. Mradi huo una thamani ya shilingi bilioni 119 na sisi kama Wabunge wa Mkoa wa Songwe tuna imani kwamba, mradi huo utakapokamilika, kwa kiasi kikubwa sana utasaidia kuweza kumaliza changamoto kubwa ya maji inayowakumba wanawake wenzangu wa Mji wa Tunduma, inayowakumba wanawake wenzangu wa Mji wa Vwawa na inayowakumba wanawake wenzangu wa Mji wa Mlowo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu umesainiwa mwezi wa Tatu mwaka 2025. Ninakiri kwamba, huu mradi umetusaidia sana hata kwenye kutafuta kura za Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na hata ushindi mkubwa ambao ameupata ndani ya Mkoa wa Songwe ni kutokana na ahadi ya umaliziaji wa mradi huu wa Mto Momba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni miezi 13 sasa imepita tangu mradi huo uweze kusainiwa. Kwa bahati nzuri siku ya kusaini Mheshimiwa Aweso ulikuja na Waziri wa Fedha, ambaye sasa hivi ndiye Mtendaji Mkuu wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kwamba, Mheshimiwa Waziri ameona namna ambavyo wanawake wamehamasika na ambavyo wameufurahia huu mradi. Imepita miezi 13 sasa na hivi ninavyoongea imebaki miezi 15 tu mradi unatakiwa uweze kukamilika, lakini mpaka sasa hali ya kule site kwa kweli, bado hairidhishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajua Mheshimiwa Aweso ni mfuatiliaji, na anajua kinachoendelea kule Songwe. Mpaka sasa hivi, kwenye yale makubaliano, mkandarasi alipaswa apewe malipo ya awali, shilingi bilioni 15, lakini mpaka sasa amepokea shilingi bilioni 5.9 pekee yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwa nature ya mradi jinsi ulivyo mkubwa ni wazi kwamba, shilingi bilioni 5.9 zitaishia tu kwenye kufanya yale maandalizi ya awali. Bado mradi hautaweza kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba sana Mheshimiwa Aweso, amefanya mambo makubwa na sisi wananchi wa Mkoa wa Songwe tumesikia miradi mbalimbali ambayo imetekelezwa. Mradi wa Kidunda wa kutoa maji kwenye Ziwa Victoria na Mbunge mwenzangu hapo amesimama, amesema sasa hivi mradi umefika Singida na sisi wananchi wa Mkoa wa Songwe tunakuomba sana, tunaiomba sana Serikali iweze kutilia mkazo kwenye kuhakikisha kwamba, mradi wa kutoa maji Mto Momba unakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa changamoto ni fedha, mimi ninaiomba Serikali, kwanza, iongeze speed ya kutoa fedha kwenye mradi ili mkandarasi asisimame na wananchi waone kwamba, mradi unaanza kutekelezwa. La pili, tunafahamu dhamira ya Serikali ni kutekeleza mradi huu kwa kutumia mapato ya ndani, siyo jambo baya, lakini pia, tumeona miradi mingi ya kimkakati, ambayo Serikali imeitekeleza kwa kutafuta mikopo yenye masharti nafuu. Kama inawezekana, Serikali iangalie uwezekano wa kutafuta mkopo nafuu kwa sababu, kwa miezi 15 iliyobaki siyoni uwezekano wa huu mradi kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko jambo zuri sana ambalo Mheshimiwa Waziri ameliongelea kwenye hotuba yake, amesema kwamba, wana mpango sasa hivi wa kuanzisha water body. Hili ni jambo jema na linaonesha namna gani ambavyo Wizara hii imekaliwa na Waziri, ambaye ni mbunifu. Kila siku anaumiza kichwa kuhakikisha kwamba, tunamaliza changamoto za maji. Kwa hiyo, ninaomba Mheshimiwa Waziri atakapoanzisha huo mkakati wa water body, kwa sababu amesema ni mpango ambao lengo lake ni kumaliza ile miradi ya kimkakati, kipaumbele namba moja ninaomba sana asiusahau mradi wa kutoa maji kwenye Mto Momba.

(Hapa, kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho…

MWENYEKITI: Hakuna la mwisho Mheshimiwa, malizia.

MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo miradi 24 ndani ya Mkoa wa Songwe. Tunaomba iweze kukamilika kabla hamjatuletea miradi mingine, ahsante.