Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Lucy Thomas Mayenga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kutoa mchango wangu. Kwanza kabisa, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kusimama leo hapa kuweza kutoa mchango wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuweza kunipitisha kugombea kwa mara nyingine na hatimaye kufanikiwa kubaki hapa Bungeni kwa kipindi cha tano. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisiwasahau wananchi wangu wa Jimbo la Kishapu, ni wananchi ambao kwa kweli wamenipa heshima kubwa kuanzia kwenye kura za maoni mpaka leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli kusimama kuchangia na kutoa mawazo kwenye Wizara kama hii kusema kweli Mbunge yeyote unapata faraja kubwa kwa sababu unajua unachangia kwenye Wizara ya watu makini ambao ni wasikivu, ambao ni wanyenyekevu na ambao wanajali maslahi ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninawapongeza sana Waziri wetu Aweso, Mheshimiwa Naibu Waziri, Kaka yangu Kundo na bila kumsahau dada yetu kipenzi Katibu Mkuu, Mwajuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Katibu Mkuu huyu ni mdogo sana, wakati anateuliwa nafasi hii ya Katibu Mkuu watu wengi walikuwa wanasema huyu dada mbona kama mdogo mdogo, lakini kwa kweli ameonesha kwamba umri haijalishi, kazi ndiyo kila kitu. Ninampongeza sana na atafika mbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kweli kwa kuinua sekta ya maji hapa nchini kwetu, ametubeba sana. Maji ni changamoto kubwa na katika maeneo mengi ninafahamu kwamba bado kuna changamoto katika maeneo mbalimbali, lakini kwa kweli kujitoa kwake mama yetu huyu, kuweka fedha nyingi kwenye sekta ya maji, wananchi wengi vijijini na maeneo hata ya mjini wanamkubali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapongeza wasimamizi wa sekta hii ya maji, CEO wa RUWASA ambaye ni kaka yangu, Eng. Walter, CEO wa DAWASA, Eng. Bwire, ninawapongeza kwa sababu moja kati ya jambo kubwa ambalo nimekuwa nikipingana nalo miaka yote nikiwa Bungeni ni ubadhirifu na wizi. Wameweza kupambana na haya mambo kwa kusimama kidete, hawa-compromise kwenye quality, ninawapongeza sana. Ninaona kabisa sekta hizi zimepata watu makini, ninampongeza Mheshimiwa Rais kwa uteuzi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme mambo yafuatayo: mpaka sasa hivi jumla ya miradi 3,302 imekwenda vijijini. Hii ni miradi mingi sana, lakini nilikuwa ninaomba Waziri atupe jicho la kipekee kwenye Jimbo langu la Kishapu. Mheshimiwa Waziri mwenyewe anafahamu, alikuja na Mheshimiwa Rais wakati wa kuomba kura na alisimama akasema kwamba kwenye Jimbo hili atafanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji vyote, Kata zote ambazo zina changamoto ya maji nimeshamwelezea, Kata kama ya Mwataga wanayo changamoto ya maji kubwa, Kata ya Sekebugoro, Shagihilu, Masanga, Kiloleli, Ngofiram, Mwaweja, maeneo haya yote yana changamoto kubwa sana ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimwambie Mheshimiwa Waziri kwenye Jimbo langu la Kishapu kuna Kata moja ambayo haina maji ya bomba kabisa. Wamehangaika sana, chini hakuna maji, kama ambavyo Mheshimiwa Waziri anafahamu kwamba katika eneo letu la Jimbo la Kishapu chini ni pakame. Kwa hiyo, wananchi wanalalamika sana na wanahangaika sana kuhusu changamoto ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya miradi kwa mfano kama Kata ya Igaga, kuna miradi imeshafanyiwa usanifu, Kata ya Mwataga kuna miradi imefanyiwa usanifu na maeneo mengine. Hii miradi ambayo tayari imeshafanyiwa usanifu ninaomba sana, tusaidiwe tuweze kupata fedha kwa ajili ya kupeleka maji katika maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, kwenye Kata zile nyingine ambazo zina mradi wa Ziwa Victoria unapita, Kata kama Sekebugoro, Kata kama Busangwa, Kata ya Mondo, Kata ya Bubiki, wananchi wanalalamika sana, hawana maji. Imagine mradi wa Ziwa Victoria unapita kwenye maeneo yao, lakini maji wao hawana, kwa kweli inasikitisha na inauma sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo tunajua kwamba maji ni uhai, ninakuomba uweze kutusaidia. Uwe na mkakati maalum wa kuangalia maeneo ambayo hayana kabisa maji, na yale mengine ambayo yana unafuu unaweza ukawaangalia kwa second hand. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua hilo, pia ninaomba sana baadhi ya miradi mikubwa katika Jiji la Dar es Salaam pale DAWASA, ninaomba DAWASA pale iwekewe mkakati maalum iweze kupata fedh. Kingine, madeni ya DAWASA yachukuliwe na Serikali ili uboreshaji wa maji katika Jiji la Dar es Salaam uende kwa kasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja. Ahsanteni sana. (Makofi)