Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Mecktridis Fratern Mdaku

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Malinyi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. MECKTRIDIS F. MDAKU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuchukua nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti ya Wizara ya Maji ya mwaka 2026/2027.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote ninapenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa baraka na neema zake. Pia, kwa nafasi ya kipekee ninamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nzuri anayoifanya katika Taifa letu, lakini pia kuendelea kuwa Rais wa maono kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi nzuri anayoifanya, anatuwakilisha vyema upande wa Serikali, pia na kazi nzuri anayoifanya ya ziara anayozunguka katika Mikoa yote Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nafasi ya kipekee, ninapenda kumpongeza sana Waziri wa Maji, kaka yangu, Mheshimiwa Jumaa Aweso, Naibu wake, Mheshimiwa Kundo Mathew pamoja na Dada yangu Mwajuma Waziri na timu nzima ya watendaji wa Wizara ya Maji kwa kazi kubwa wanayofanya kuhakikisha sekta ya maji iko vizuri na kumtua ndoo mwanamke kichwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninampongeza Kaka Kirita, Engineer wa RUWASA, kwa kutusaidia watu wa Malinyi kwa kushirikiana na Mhandisi wa Mkoa, Eng. Lutonja wa RUWASA Mkoa wa Morogoro. Pia na mhandisi wangu wa RUWASA Wilaya ya Malinyi, kaka yangu Marco Chogelo. Kwa kweli ninawashukuru sana kwa sababu Jimbo la Malinyi ni Jimbo lenye changamoto ya maji, lakini wamejitahidi kadiri walivyoweza kuhakikisha Malinyi inakaa vizuri na watu wanapata majisafi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Maji, na mchango wangu mkubwa nimeutoa kwa njia ya maandishi, lakini hapa leo ninapenda kuongelea tu kuhusu Jimbo langu la Malinyi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishukuru sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Maji kwa kutupa miradi katika Wilaya yetu ya Malinyi. Zaidi ya shilingi 1,100,000,000 zinakwenda kutekeleza katika maeneo ya Malinyi, Ihowanja, Biro, Misegesi, Mbalinyi pamoja na Kilosa Mpepo. Kwa kweli ninasema ahsanteni sana, ninashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa kuwa Malinyi tumekumbwa na changamoto nyingi kubwa ukiacha ya mafuriko ambayo pia na yale mabwawa yetu yanaharibika, lakini Serikali imetuangalia kwa jicho la huruma na inakwenda kutekeleza miradi hii. Hii miradi ilikuwa imekwama lakini sasa Serikali nadhani inatoa fedha kuhakikisha miradi hii inakwenda kukamilika na inakwenda kutekelezeka (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina imani kubwa sana na Mheshimiwa Aweso na timu yake, na nitawapa ushirikiano mkubwa kuhakikisha hii miradi inakwenda kukamilika ili adha ya maji katika Wilaya ya Malinyi iweze kuondoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya miradi hii iliyotajwa katika bajeti ya Wizara ya Maji ya mwaka huu, bado Malinyi tuna changamoto ya miradi miwili ambayo ni chakavu sana ikiwa ni mradi wa maji tiririka wa Mtimbira, ulijengwa miaka ya 1980 iliyopita na ilijengwa wakati huo ilikuwa inahudumia watu 12,000, lakini sasa hivi inahudumia wananchi 72,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa ninaomba Serikali iangalie uwezekano wa kwenda kukarabati mradi huu, itoe fedha ili mradi huu nao uende ukakamilike ufanyiwe ukarabati wa upanuzi wa miundombinu yake, matenki pamoja na mabomba. Pia, mradi wa Itete nao pia ni mradi wa maji ya mserereko lakini pia ni chakavu kama ulivyokuwa mradi wa Mtimbira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna uhaba wa maji katika vitongoji vya pembezoni mwa maeneo ya Madega, Njasa, Lumbanga, Mkanga, Butu pamoja na Shinyanga. Ninaomba maeneo haya pia ikiwezekana yaweze kupatiwa maji ya visima virefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Malinyi hatuna changamoto ya vyanzo vya maji, tunavyo vyanzo vya maji vya kutosha vya mito pamoja na mabwawa, lakini tumekuwa hatupati yale majisafi na salama. Licha ya Wizara kujitahidi na RUWASA kujitahidi, dada yangu Mwajuma aliniambia siku moja: “Mheshimiwa Mbunge tena kwenu Malinyi mbona mnapata majisafi na salama mazuri kabisa! Katika Wilaya zote Mkoa wa Morogoro Malinyi tumejitahidi kuleta huduma hii.” Ni kweli kabisa ninamshukuru sana, lakini bado hayatoshelezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba Wizara iangalie kwa jicho la huruma hii miradi ya visima pamoja na hii miradi michakavu ikienda kukamilika itahudumia watu wengi sana wa Wilaya ya Malinyi na wao pia wataishukuru Serikali yao kwa kuwajali na kuwapa majisafi na salama. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. MECKTRIDIS F. MDAKU: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja. (Makofi)