Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Zuena Athumani Bushiri

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia Hotuba hii ya Wizara ya Maji. Nianze kwa kusema kuwa mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Wizara hii ya Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea bajeti hii ya shilingi trilioni moja na point. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri Jumaa Aweso, nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri Kundo, niwapongeze wafanyakazi wote wa Wizara ya Maji wakiongozwa na Engineer Mwajuma Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaongelea kuhusu Mkoa wangu wa Kilimajaro. Katika Mkoa wa Kilimanjaro tumepata mradi mkubwa wa shilingi bilioni 406 na point. Mradi ule umekwenda vizuri sana katika awamu ya kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na shukrani, tunaishukuru sana Serikali ya Awamu Sita kwa kupitia Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan. Waswahili wanasema ‘Kushukuru ni kuomba tena’. Tunaamini kwamba awamu ya kwanza iliyotekelezeka imefanya kazi vizuri, imewatua akina mama ndoo kichwani kwa kiasi fulani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba Serikali iendelee kutoa fedha kwa ajili ya kuendeleza mradi huu katika awamu nyingine ya pili ambayo itachochea sana maji kwa matumizi ya nyumbani, na zoezi la kumtua mama ndoo kichwani litakuwa linaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuongelea Mradi huo wa Kilimanjaro, nitaongelea RUWASA, Wakala wa Maji Vijijini. RUWASA ni chombo ambacho kinafanya kazi katika vijiji vyetu vyote vya Tanzania. RUWASA wanafanya kazi nzito na ngumu kwa mazingira yao. Waheshimiwa Wabunge wenzangu wote tunafahamu kwamba asilimia kubwa ya wananchi wetu wanaishi vijijini na vijijini kule ndipo hapo palipo na ile kauli ya kumtua mama ndoo kichwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona kazi aliyoifanya Mheshimiwa Rais katika kuchimba maji chini kwa kupitia magari. Maeneo ambayo hakuna maji kabisa tumewaona akina mama, hii ni kazi ya RUWASA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, RUWASA hii hii, ukiangalia bajeti yake ni ndogo sana. Ili ifanye kazi vizuri inahitaji kuongezewa bajeti. Kwa kuwa bajeti yao ni ndogo na watumishi wao ni wachache, ili wafanye kazi vizuri tunaiomba sana Serikali iongeze bajeti RUWASA. Isitoshe kwenye kuongeza bajeti tu na watumishi hawatoshi. Pia iende mbali, ihakikishe kwamba inaweka mipango mizuri ya kuwapanga watumishi hawa kikanda ili kusudi lililokusudiwa likapate kutekelezeka vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la mabonde. Tunayo mabonde tisa nchini. Watu wote tumesimama hapa tunaongelea kuhusu vyanzo vya maji, tunaongelea kuhusu uchafuzi wa maji, tunaongelea kuhusu matumizi mabaya ya maji; lakini wanaohusika na haya ni hawa watu wa mabonde. Watu wa mabonde ndiyo wanaosimamia vyanzo vya maji. Tumeona, wote ni mashahidi; tumesimama hapa tumeongea katika Bunge lako Tukufu, yako maeneo ambayo ukipita, sisi wenyewe tukipita kurudi majimboni kwetu tunaona jinsi wananchi wanavyofanya shughuli za maendeleo za kilimo kwenye mifereji. Tunaona jinsi ambavyo wananchi wanafanya shughuli zao za maendeleo kwenye nishati kinyume na utaratibu wa matumizi ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe sana Serikali, hawa watu wa Bonde la Maji waweze kuangaliwa kwa jicho la tatu. Maana ya jicho la tatu ni nini; kwanza waongezewe bajeti ili waweze kufika katika vyanzo vya maji ambavyo wanavyo ambavyo vinaharibiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niseme kwamba ninaunga mkono hoja. Niishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita, iendelee kutoa fedha ili kazi ya maji inayoendelea nchini ikapate kukamilika vizuri. Ahsante sana.