Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Rorya
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara yetu hii ya Maji. Kwa sababu ya muda nianze kwa kuazima maneno ya Mheshimiwa Waziri wa Maji mwenyewe ambayo amekuwa akiyatumia sana; kwamba ‘Moyo usiyokuwa na shukrani hukausha mema yote’. Kwa kweli kwa mtu ambaye hatakuwa na moyo wa shukrani kwa kazi kubwa nzuri ambayo Mheshimiwa Waziri ameifanya kwa muda wote ambao amekuwa kwenye wizara hii, basi atakuwa anakausha mema yote ambayo kimsingi halitakuwa jambo jema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua dhamira nzuri ya Mheshimiwa Dkt. Samia, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo inakwenda kutafsiriwa na Waziri wa Maji kwa namna ya utendaji wake wa kazi, yeye pamoja na wasaidizi wake, Mheshimiwa Naibu Waziri pamoja na watendaji wote wa Wizara. Sisi tunawaombea kila la kheri Mheshimiwa Waziri, tunajua kuwa atafika kule ambako kunakusudiwa kwa namna ambavyo anaendelea kutafsiri maono na dhamira ya Mheshimiwa Dkt. Samia ya kumtua mama ndoo kichwani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda, pamoja na dhamira nzuri aliyonayo Mheshimiwa Waziri nimwombe autazame sana Mkoa wa Mara. Katika tafiti ambazo zipo za ukiangalia hata tafiti zake katika mikoa yote 26 atatambua kwamba Mkoa wa Mara ndiyo mkoa ambao kama si wa mwisho, basi ni wa pili kutoka mwisho kwa changamoto kubwa sana ya maji. Wakati tunakumbana na changamoto hii, ni mkoa ambao unazungukwa na maji kwa isiyopungua 60% kwenda mpaka 70%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano Wilayani kwangu Rorya; mimi peke yangu ninazungukwa na maji; kwa maana ya Ziwa hili Victoria ambalo linatoa maji kwenda mahali parefu, yanakwenda Nzega, yanakwenda Dodoma na maeneo mengine; ninazungukwa na maji 77%. Yaani eneo la nchi kavu ambalo tunaishi sisi na kufanya shughuli zetu za kiuchumi ni 23% pekee yake, 77% ni maji pekee yake; lakini unaweza ukaona katika wilaya zote za Mkoa wa Mara, wilaya ambayo ina changamoto kubwa ya maji ni Wilaya ya Rorya. Ninatambua juhudi zake na kazi kubwa nzuri alizofanya katika awamu iliyopita kwa miaka iliyopita, amenisimikia miradi kadhaa pale, lakini miradi ile imesimama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba Mheshimiwa Waziri, pamoja na majibu mazuri atakayoyatoa hapa leo sina sababu ya kumshikia shilingi, lakini apange namna ya kufanya ziara; twende tukatembelee miradi ile ambayo Mheshimiwa Dkt. Samia ametupa fedha lakini miradi mingi imesimama na haitoi maji. Ninamtegemea sana Mheshimiwa Waziri, kwa sababu kwa kufanya hivyo ninaamini kuwa tutaondoa manung'uniko ya wananchi kwenye maeneo yale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upo Mradi wa Miji 28, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri; ninajua ni juhudi zake yeye. Bila yeye Wana-Rorya wasingepata ule mradi pamoja na Tarime. Alikwenda akamshawishi Mheshimiwa Rais, akaridhia mradi ule uingizwe kwenye bajeti na sasa unatekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi ule unakwenda kwa kusuasua sana, tuombe fedha. Nichukue nafasi hii kuomba sana Wizara ya Fedha wautazame mradi ule. Mradi ule ndilo suluhisho la changamoto ya maji kwenye wilaya zaidi ya tatu zenye population zaidi ya watu 200,000 wanakwenda kutatuliwa na changamoto ya maji kwa kukamilika kwa mradi ule. Niombe sana Wizara ya Fedha watoe fedha ili mradi ule uweze kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kutambua na changamoto zilizopo, mimi nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwamba wakati tunaingia 2021 changamoto ya maji kimkoa tulikuwa kwenye 54% peke yake, sasa hivi tupo kwenye 81%. Tumwombe aweke nguvu chini, akazane kadiri anavyoweza ili na sisi tuondokane na changamoto ya maji kwenye maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri mambo mahususi kama matatu. Kwanza, upo mradi wa Kata ya Kang'ombe, mradi ule ndiyo wanaouita Mradi wa Nyihara. Mheshimiwa Dkt. Samia ametupa zaidi ya milioni 600. Mheshimiwa Waziri autazame mradi ule. Leo wananchi wa kata ile zaidi ya 20,000 hawapati maji safi na salama pamoja na kupewa shilingi 600,000,000 kwa sababu ya upungufu wa shilingi 20,000,000 peke yake ya kukamilisha kuwalipa watu wa TANESCO waweze kuunganisha maji kwa kutumia umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shilingi 20,000,000 hii ninaamini Mheshimiwa Waziri akitamka leo haina sababu ya kusubiri bajeti ya mwakani. Mradi wa shilingi 600,000,000 tayari tumeshakamilisha, shilingi 20,000,000 ya kuwalipa TANESCO ili waweze kuweka transfoma pale wananchi wanufaike. Mradi umesimama; na nimeona kwenye bajeti humu tunaambiwa hadi 2027. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri atakaposimama jioni ya leo, aweze kusema neno.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ambalo ningetamani nimshauri Mheshimiwa Waziri ni kwenye hizi jumuiya za maji; zinahangaika sana. Tumepewa sana miradi kule vijijini, unakuta mtu ameishiwa LUKU ya shilingi 20,000, mlolongo wa maombi ya kununua luku anaanza yeye, inakwenda inapitishwa na wilaya, inakwenda mkoani, inakuja HQ, inakwenda Hazina; shilingi 20,000 peke yake wananchi wamekaa wanamsubiri. Niombe utaratibu huu ufumuliwe; ikiwezekana kama inawezekana iishie ngazi ya mkoa ili angalau tupunguze manunguniko kwa sababu miradi ipo, lakini inakaa muda mrefu haiwezi kutoa maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri jambo la pili; tumepewa mitambo ya kuchimba visima gharama za kukodisha mitambo ile ni kubwa sana. Kuna wakati Mheshimiwa Mbunge anatamani atoe fedha hata ya Mfuko wa Jimbo kusaidia kuchimba visima, lakini gharama za kukodisha mitambo ambayo tumepewa sisi wenyewe ni gharama kubwa sana. Niombe wazipitie gharama hizi ili ziweze kuwanufaisha wananchi. Tupo tayari sisi kuwasaidia wananchi kwa kuunga juhudi kama wadau lakini gharama za kukodisha mitambo zimekuwa ni kubwa wakati mwingine tunashindwa kufikia malengo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe lingine ambalo ninafikiri Mheshimiwa Waziri anaweza akalifanyia kazi; ni kuhakikisha kwamba; kama nilivyosema; miradi yote ambayo tayari Mheshimiwa Dkt. Samia alitoa fedha, ipo kwenye maeneo mbalimbali, tuhakikishe miradi ile inakamilika na inatoa maji. Ikibidi na ikimpendeza Mheshimiwa Waziri ahakikishe kuwa ile miradi ya zamani inakamilika kwanza kabla hatujaanzisha miradi mipya. Kwa sababu miradi ya zamani tayari ipo, Mheshimiwa Dkt. ameweka fedha, lakini wananchi hawanufaiki na miradi ile. Ikianzishwa mradi mpya na ilihali mradi wa zamani bado haujanufaisha wananchi; tunakuwa hatujafanya jambo sawa; kwa sababu tunakwenda na tunarudi nyuma. Matokeo yake ndiyo maana ukisema asilimia za upatikanaji wa maji bado tunaonekana tuna changamoto kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtakie Mheshimiwa Waziri kila la kheri, ninajua yeye ni msikivu na ninajua anakwenda kuyatatua haya Waheshimiwa Wabunge tunayoyasema. Ninaamini kabisa kwa uwezo wake na uchapakazi wake sina shaka juu ya hili. Hata hivyo, ningetamani atamke neno juu ya mradi wenye upungufu wa shilingi 20,000,000 ili wananchi wa Kata ya Kyang'ombe waweze kunufaika na maji ya shilingi 600,000,000 ya Mama Samia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)