Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Sheila Edward Lukuba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. SHEILA E. LUKUBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia kwenye Wizara hii ya Maji. Awali ya yote, ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijalia kuweza kusimama kwenye Bunge lako Tukufu. Pia ninamshukuru Mheshimiwa Rais kwa niaba ya wanawake wa Mkoa wa Morogoro, kwa jinsi anavyopambana kuhakikisha anamtua mama ndoo kichwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Waziri Aweso pamoja na menejimenti yake yote kwa hotuba yake nzuri iliyoshiba yenye matumaini kwa wananchi wa Tanzania. Ninatoka Mkoa wa Morogoro, tuna majembe kule Mkoa wa Morogoro, Ndugu yangu Kejo na ndugu yangu Lusajo. Watu hawa wamekuwa ni wapambanaji, ukipiga simu moja tu wanapokea. Ninadhani kuna mafunzo ambayo wamepewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nitakwenda na mstari unasema Mathayo 10:42 Yesu anasema: “Na yeyote atakayemnywesha mmoja wa wadogo hawa kikombe cha maji baridi kwa jina la mwanafunzi, amini nawaambia hatopoteza thawabu yake”.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa tendo la Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan kuanzisha Gridi ya Taifa, sisi wanawake wa Mkoa wa Morogoro tunampongeza. Watu wote sasa wanakwenda kuoga, tunakwenda kumwagilizia, lakini wote tunakwenda nchi nzima kunufaika na maji safi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Morogoro pia tunamshukuru Mheshimiwa Rais, hadi Disemba, 2025, ameweza kutupa kiasi cha shilingi 456,000,000,000 ambapo miradi ya shilingi 58,000,000,000 imeshakamilika na miradi ya kiasi cha shilingi 397,000,000,000 wakandarsi bado wanadai. Niwaombe Wizara ya Fedha kupitia Wizara ya Maji, waweze kutoa fedha hizo ili miradi iweze kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumpongeze pia Mheshimiwa Rais, Mkoa wa Morogoro wakati anaingia tulikuwa na 53% tu ya upatikanaji wa maji safi na salama, lakini mpaka Desemba, 2025 Mkoa wa Morogoro upatikanaji wa maji kwa sasa ni 72%. Ahsante sana mama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na maji hayo kumekuwa na uchafuzi wa maji katika vyanzo mbalimbali. Niwaombe Wizara ya Maji kwa kushirikiana na TAMISEMI waweze kuvilinda vyanzo hivyo hata kwa kutumia mgambo wa halmashauri ili watu waweze kupata maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe kutoa ushauri kwa Mheshimiwa Waziri, TAMISEMI na Ofisi ya Rais na Mazingira kwamba Mkoa wa Morogoro urudishiwe misitu ya zamani ya Milima ya Uluguru, Udzungwa, Lumuma, Kipate, Lubeho, Turiani, Lumbiji na milima mingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, milima hiyo ni vyanzo vikuu vya maji kwenye Mkoa wa Morogoro. Mabwawa yote haya tunayoyajenga yanategemea maji kutoka kwenye vyanzo hivyo. Hivyo niwaombe turudishe ule uoto wa zamani wa milima hii. Pamoja na kwamba sisi Mkoa wa Morogoro tuna mabwawa, (Bwawa la Mwalimu Nyerere na Bwawa la Kidunda) lakini tuna upungufu wa maji kwenye vijiji 65. Vijiji hivi havina maji kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mbunge wa Mkoa ningeweza kutaja kijiji kimoja kimoja, lakini nitataja kwa ujumla. Wilaya ya Mvomero, vijiji 19; Morogoro Vijijini; vijiji 27; Kilosa; vijiji 14; na Gairo; vijiji vitano. Nitamwomba Waziri atakapokuwa anakuja kumalizia; je, Serikali haioni kuna umuhimu sasa wa kuweka mkakati wa muda mfupi ili vijiji hivi viweze kupata maji safi na salama? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimwombe Waziri Aweso ndugu yangu ana watendaji wazuri sana kwenye Mkoa wa Morogoro, lakini RUWASA – Kilosa, Ulanga, Malinyi hawana magari. Nimwombe ndugu yangu awapatie magari ili wakishindwa kufanya kazi aweze kuwawajibisha ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache, ninaomba niunge mkono hoja. Ahsante. (Makofi)