Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Edibily Kinyoma Kazala

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. EDIBILY K. KINYOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia. Kwanza ninaomba niipongeze Wizara kwa kazi kubwa ya kizalendo kazi ya kiwito kabisa ya kuwatumikia Watanzania. Pia, nimshukuru Mheshimiwa Rais, lakini pia nimpongeze kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya kazi ya utu ya kuhakikisha anamtua ndoo kichwani mama zetu na dada zetu wanaohangaika usiku na mchana kuhakikisha wanatunza familia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru Wizara nimeona kwenye bajeti yao pale wamenitengea shilingi bilioni 1.5 kuhakikisha Kijiji cha Chekenya, Kabulanzwili, Muzye, Nyakitonto, Malalo, Kazage, Makere, Nyangwa, Kalimungoma na Rusesa wanapata maji safi na salama bila kusahau Titye na kisima kinachokwenda kuchimbwa Kijiji cha Mvugwe. Kwa kweli ninawashukuru sana Wizara kwa moyo huu mzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe fedha hizi wasichelewe watuletee kwa haraka, wananchi wanayo hamu kubwa ya kupata huduma hii ya maji. Wakati ninamaliza ninaomba nishauri kitu kimoja tu kwenye Wizara pamoja na kazi kubwa wanayoifanya; bado kuna shida kubwa kwenye upotevu wa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mheshimiwa Waziri alivyozungumza mwenyewe wakati anawasilisha, tuna upotevu wa maji zaidi ya 30% kwenye Taifa letu. Tunapozungumza zaidi ya 30%, ripoti ya mwisho inaonesha zaidi ya 35% tunapoteza maji kwenye Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake hii 35%, kama tuna 100% kwamba 35% tunapoteza, maana yake maji hayawafikii wananchi. Tunaweza tukasema kwamba labda tumetoa milioni kadhaa za lita za maji zinawafikia wananchi, lakini ukienda maana yake field haya maji hayapo. Kwa hiyo, iko haja ya Serikali na Wizara kuongeza mbinu mbadala za kuhakikisha wanadhibiti maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri, ikiwezekana watumie teknolojia ya kisasa ikiwemo zile sensors za kujua wapi kuna leakage za maji. Ukienda mijini utakuta maji yanatiririka hovyo na vijijini mpaka pengine unaona huruma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine niwashauri waongeze uwajibikaji hasa wale watumishi wa chini, maana kuna eneo unaweza ukapita unakuta leakage ni ndogo tu, lakini maji yanatiririka zaidi ya wiki mbili na watumishi wako pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri watu wa RUWASA kwa kwetu kule vijijini wajitahidi unakuta changamoto ni ndogo tu hata ukifunga mpira tu, lile eneo linakuwa limezibika. Kwa hiyo, nishauri kwenye upotevu wa maji wajitahidi watumie sensors, lakini pia watumishi wawe active kupambana na hizi changamoto ndogo ndogo zinazowezekana kutibika kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa utafiti tunapoteza zaidi ya shilingi 185,000,000,000 kwenye upotevu wa maji. Kwa hiyo, unaweza ukaona ni fedha nyingi na mapato mengi yanapotea ambazo ni fedha za Watanzania ambazo zingeweza kusaidia kuchimba visima vya kutosha, vingeweza kusaidia kuwapelekea maji kwenye vijiji vingine ambavyo tunasema…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. EDIBILY K. KINYOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuunga mkono hoja na ninashukuru sana. (Makofi)