Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lupa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana nami kupata nafasi kuweza kuchangia kwenye hii Wizara muhimu sana, Wizara ambayo haina mbadala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake yote ya Wizara kwa kazi kubwa ambayo wanaendelea kufanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kilio cha Watanzania wote ni maji na wao wamejizatiti kuhakikisha kwamba hakika hawalali kuhakikisha kwamba wanafikisha maji kwa kila Mtanzania, hongera sana kwao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kumpongeza Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa champion kuhakikisha kwamba anaendelea kuwatua akina mama ndoo kichwani. Hili kwetu sisi tunampongeza yeye na tutaendelea kumwombea ili azma yake ile iweze kwenda kutimia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze pia RUWASA kuanzia DG wake na viongozi wake kwa Mkoa mpaka Wilayani kote wanafanya kazi kubwa nzuri na tumeona miradi mingi ambayo tumeenda kuitembelea. Hata kule Wilayani kwangu Chunya fedha nyingi ambazo zimekwenda kwenye upande wa RUWASA kule vijijini zimeweza kwenda kufanya kazi na matokeo yanaonekana na DM wangu Engineer Oleneno Sanga kwa kweli anafanya kazi kubwa sana. Tusipowasifu wakiwa hai hatuwezi tukawasifu wakiwa hawapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi kubwa ambayo inaendelea kufanyika tumeona hapa karibu Wabunge wote ambao wamesimama hapa jambo kubwa wanaipongeza Serikali kupeleka miradi kwenye maeneo yao. Hata hivyo, jambo kubwa ambalo wameenda kuwa kilio chao ni kutokamilika miradi hii kwa wakati na fedha kwenda kwa kusuasua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha zinapokwenda kwa kusuasua maana yake miradi hii yale malengo ambayo yamewekwa kwenda kuwafikia kwenda kumtua mama ndoo kichwani hayawezi kufikikiwa kwa wakati. Sasa, ushauri wangu ni nini? Ushauri wangu kama Serikali, kama nchi twende na mkakati wa pamoja kwenda kutafuta fedha ili miradi hii yote chechefu twende tukaitatue. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona mfano kupitia hatifungani kwenye Mkoa wa Tanga imeweza kufanya vizuri. Hii tuchukue kama sample kwenye nchi nzima twende na model hiyo twende tukauze hatifungani hizi tupate fedha ili miradi kwenye kila Jimbo kila mahali iweze kukamilika ndiyo tutakuwa tumeenda kuwasaidia wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadaye lazima wajue wananchi wetu kwamba maji ni huduma, lakini maji ni biashara. Tunapofungua bombani maji yanapotoka wao watalipa. Kwa hiyo maana yake tukienda kwenye hatifungani tutapata fedha, ile fedha ambayo ataendelea kutumia ndiyo ambavyo itaenda kurudi na kurudisha ile fedha ambayo imetumika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo lakini wananchi wangu wa Chunya Mjini wamenituma maji. Leo ninapozungumza haya na Mwenyekiti wangu wa Bodi yuko hapa juu kwenye Jukwaa la Spika pamoja na wapiga kura wangu wengine, akina mama wameniambia usipozungumza habari ya maji Chunya Mjini hatutakuelewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Chunya Mjini tupo kwenye Mradi wa Maji wa Miji 28. Miji 28 kwa kweli kwa Chunya bado haijaanza hata kidogo na tunafahamu juhudi ambazo zinaendelea kufanyika. Pamoja na yote hayo, tuone namna nzuri na bora kuhakikisha kwamba mradi huu unaanza na wananchi hawa wanaenda kupata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi wakati juhudi hizo zinaendelea twende tukatatue changamoto hii kwenda kuchimba visima japo vichache kwa muda mfupi ili changamoto ya maji pale Chunya Mjini iweze kupungua au iweze kwisha ili wananchi wangu wa Chunya na wao waweze kuona Wizara ya Maji na yenyewe inasikia kilio chao na inakwenda kuwatatulia hili. Bila kufanya hivyo DM wangu wa pale Chunya Engineer Chamsa ataendelea kulalamika na wananchi wataendelea kumlalamikia anafanya kazi lakini watu wa Chunya Mjini wanataka maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja kwamba pale Chunya Mjini kuna changamoto ya maji, bado kuna miradi michache chechefu ya kule upande wa RUWASA, kuna Mradi mkubwa wa Matwiga phase two. Mradi huu uli-design-iwa kwa vijiji nane, lakini sasa hivi unatoa maji kwa vijiji viwili. Kwa hiyo ile pressure ambayo imetoka kwenye chanzo kwenda kwenye tenki mpaka kwenye usambazaji huo imekuwa kubwa kwa sababu design yake imekuwa ni vijiji nane na sasa hivi inakwenda vijiji viwili hivyo inapelekea changamoto ya mabomba kupasuka mara kwa mara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mitambo ambayo imefungwa pale na kile ambacho kinaenda kuzalishwa hivyo wananchi hawa wanalipa kidogo kuliko umeme ambao unatumika pale. Matokeo yake mradi uendeshaji wake ni mkubwa kuliko kile ambacho kinakusanywa. Niombe twende tukaumalizie mradi huu ili uweze kwenda kutekeleza na vijiji vingine kwa maana ya Kijiji cha Mazimbo kiweze kwenda kukamilika. Fedha zimeombwa na zikipatikana zaidi ya shilingi milioni 300 at least pale zitaweza kutusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji vingine vya Mtanila na maeneo ya jirani kwenye ule mradi vikiweza kukamilika ndivyo ambavyo tutaweza kwenda kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kupata nafasi hii na ninaunga mkono hoja. (Makofi)