Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Santiel Eric Kirumba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. SANTIEL E. KIRUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, ninapenda kuipongeza Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa Mkoa wa Shinyanga kwa awamu iliyopita, iliweza kutuletea takribani shilingi bilioni 145 za mradi wa maji. Hii inaonyesha kabisa ajenda ya Mheshimiwa Rais kwa Mkoa wa Shinyanga ni kumtua mwanamke ndoo kichwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ameweza hii kuitekeleza; Mkoa wa Shinyanga una vijiji 506, mpaka sasa hivi tunavyoongea vijiji 46 tu ndiyo havijafikiwa na mtandao wa maji. Kwa hiyo, nina imani Waziri Mheshimiwa Aweso, tutakapoipitisha bajeti hii, ataweza kutukamilishia mradi huu wa maji katika vijiji vilivyobaki 46. (Makofi

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ninapenda kuipongeza Menejimenti Nzima ya Wizara ya Maji, ukianzia Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Engineer Mwajuma, RM wetu wa mkoa pamoja na Meneja KUWASA Mkoa. Wote wamekuwa ni watu wa kufikia kirahisi tunapopata changamoto yoyote ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendelea pia kuipongeza Serikali. Kwa Wilaya yetu ya Kahama tulikuwa na changamoto kubwa sana ya maji, hasa hasa kwenye maeneo mengi, lakini Mheshimiwa Rais akaidhinisha fedha. Wakishirikiana na Barrick wameweza kujenga chujio la kisasa katika Kata ya Mwendakulima na hii imepunguza adha ambayo ilikuwa inatokea. Chujio lile la KASHWASA likipata shida, wananchi wa Kahama wanakosa maji, ambapo kwa Mkoa wa Shinyanga wananchi wa Kahama ni wengi, walikuwa wanakosa maji pamoja na vijiji vya jirani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana Mheshimiwa Waziri amesema, yeye nyumbani kwake anapata utulivu, lakini sisi wanawake wa Mkoa wa Shinyanga baadhi ya vijiji hatupati utulivu kwa sababu hatupati maji safi na salama kwenye baadhi ya maeneo. Hii huwafanya wanawake wengi kutoka asubuhi kwenda kutafuta maji na maji hayo wanayafuata kwa umbali mrefu sana na hata kulazimika pia kununua maji yale kwa gharama kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii imewapelekea wanawake wale hata kushindwa kujishughulisha na shughuli nyingine za kiuchumi kwa sababu wanakwenda kufuata maji umbali mrefu na hii imewafanya wanawake wengi wa Shinyanga pato lao kushuka. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, anapoongelea utulivu na sisi kwetu kwenye ndoa zetu Shinyanga bado utulivu haupo vizuri, tunahitaji maji safi na salama ili tuweze kujihusisha na shughuli nyingine za kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakandarasi wengi kwetu wamefanya kazi na Serikali kweli imejitahidi inalipa, lakini, kama kuna miradi mingine haina ulazima kuifanya kwa haraka tusubiri ile ambayo ipo kwa mapema iweze kulipwa. Wakandarasi hawa wanapitia shida sana tunapokuwa tunawaomba watufanyie miradi halafu tukawacheleweshea malipo. Wakandarasi hawa wengine wanakuwa wameshachukua pesa benki, kwa hivyo tunakuwa tumewaletea usumbufu mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakuomba kama Serikali turudi tena tujipange, ile miradi ambayo tuna ulazima na pesa tumeshaitenga ninaomba tuifanye kwa haraka na tuwalipe wakandarasi hawa kwa haraka. Maana hawa wakandarasi ni wananchi wetu, kwa hiyo wanapokuwa wanapitia hii adha ya malipo na kwengine wanaondoka kwenye baadhi ya miradi, inakuwa ni changamoto kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi katika maeneo yale wanaona huu mradi upo, lakini mkandarasi hayupo na wanakuwa na kiu ya kutumia maji na hawana mbadala wa sehemu nyingine wanayoweza kupata maji isipokuwa Serikali yetu inatakiwa iwatimizie kwamba waweze kupata maji safi na salama. Kwa hiyo, ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri, kwa mwaka huu wa fedha akawe na bajeti yake, awalipe hawa wakandarasi wa nyuma kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kusisitiza pia Waziri anafanya kazi nzuri sana na Serikali ya Mheshimiwa Rais imekuwa ikikuunga mkono kwa kiasi kikubwa sana kuhakikisha maji safi na salama yanafika kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana. (Makofi)