Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Neema Gerald Mwandabila

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika Wizara yetu hii nzuri ya Maji ambayo kimsingi ni Wizara ambayo ina dhamana kubwa sana kwa maisha ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuungana na wenzangu kuendelea kuwapongeza kwa namna wanavyofanya kazi na kutusaidia kusogeza huduma za maji majumbani kwetu. Kwa kuwa dakika ni chache ninaomba nijielekeze kwenye haya mambo machache: kwanza, ninatamani nimwombe Mheshimiwa Aweso kipekee kabisa kutupatia gari la RUWASA kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli katika Wilaya yangu ya Ileje. Hili ninamwomba kwa heshima na kama ningekuwa na uwezo wa kupiga magoti hapa ningempigia, kwa hiyo, ninamwomba sana Mheshimiwa Aweso. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ninataka nimpatie taarifa Mheshimiwa Aweso kwamba, tunashukuru kwa fedha shilingi bilioni 5.9 ambazo wamezitoa kwa ajili ya Mradi wa Momba, Tunduma na Vwawa. Kati ya shilingi 17,000,000,000 ambazo walitakiwa watoe kama fedha za awali tunawashukuru kwa hizo fedha, lakini ninatamani Waziri ajue kwamba pamoja na kwamba amesema mradi unatekelezeka, mkandarasi hajaanza kazi bado mpaka saa hizi pamoja na kwamba wamempa hizo fedha. Kwa hiyo, kipekee pia nimwombe sana Mheshimiwa Aweso, atusaidie huyu mkandarasi kwa hizo fedha alizompatia aanze kazi angalau sisi kama wananchi tupate matumaini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe pia kaka yangu Aweso kwamba, pamoja na kwamba anafanya kazi nzito ya kuhakikisha miradi mipya inaanza, atusaidie tu kulipa madeni ya wakandarasi wetu ambao wameondoka site, kazi hazipo. Tuna shilingi 821,000,000 ambayo wakandarasi wameondoka site kazi haziendelei. Sasa hii miradi ingetusaidia kusogea kutoka 55% ya maji tuliyonayo kwenye Mji wetu wa Vwawa Mlowo, ingetusogeza tufike angalau 84%. Kwa hiyo, hili nalo pia nimwombe Mheshimiwa Aweso atusaidie. Ninajua, anakuwa na fedha nyingi sana kiasi kwamba shilingi 821,000,000 kwake siyo changamoto kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niendelee kusisitiza kwamba Wizara hii ni ya muhimu, lazima ije na mkakati maalum wa ku-strategize yaani ni kama wafanye reform au watafute namna bora nzuri yaku-operate kutekeleza kazi zao. Hivi tunavyoongea pamoja na hayo maombi niliyomwomba kuna miradi mingi ambayo imesimama kwenye maeneo yetu: unakuta mipira imeenda site, lakini hakuna kinachokuwa kinaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wajitahidi kujipanga wanapotoa fedha watoe kwa kulingana kwamba hizi fedha zitahakikisha huu mradi unakwisha. Hiyo ninadhani sisi kama Taifa itatusaidia kuliko hapa saa hizi, sasa huyu anavuta, huyu anavuta, hakuna kinachoendelea. Kwa hiyo, hilo pia ninatamani wakae chini waangalie namna nzuri zaidi, wajipange vizuri zaidi ili kuhakikisha utoaji wa fedha wanavyokuwa wanaupeleka kwenye maeneo yetu uzingatie vigezo vya kuhakikisha miradi iwe on time. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hilo, niendelee kuomba suala la cost. Wanapokuwa wanajenga ile miradi ya maji kuna miradi ya vijijini na miradi ya mijini, kuwe angalau na uwiano wa pricing. Siyo kwingine wana-charge 300, kwingine wana-charge 500, kwingine wana-charge 700 na kwingine wana-charge 2000. Kwa hiyo, kama wanasema ni miji na kwenye miji tuta-charge kiasi Fulani, basi iwe flat rate kwenye miji yote. Kama ni vijijini wanasema vijijini tuta-charge 500, tujue basi hii ni flat rate kwa maeneo yote ya vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itasaidia hata wao kuwa na mpango mzuri wa namna ya kupata mapato. Kuna wakati nilikuwa ninasoma taarifa yao, hii Wizara ndiyo ninaona kama ni Wizara inayopokea fedha nyingi lakini hatuoni wao wanaingiza kitu gani. Kwa hiyo, ifikie hatua wanapokuwa wanapewa fedha wawe wanaoanisha na kiwango wanachokuja kuipatia Serikali yetu fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nisiseme mengi, niendelee kumsihi kaka yangu Mheshimiwa Aweso kwamba suala la Wizara hii anaiweza na anaimudu pamoja na timu yake nzima waangalie tu namna bora nzuri ya kufanya vizuri. Kuna kitu niliwahi ku-share naye, suala la Mto Rukwa. Yeye ndiye Waziri wa Maji, ndiye mmiliki wa maji ya Taifa lote hili kama maji yanatusumbua, basi na yeye anatakiwa awajibike kuhakikisha maji hayatusumbui. Sina maana ya kutusumbua kwa maana hayapatikani, lakini pia yanapokuwa yamezidi kwenye maeneo yetu waliangalie hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ziwa Rukwa linazidi kutanuka, waangalie namna ya ku-control maji ya Ziwa Rukwa, wananchi wanaendelea kupoteza maeneo yao na nini, wakati haya maji yanaweza yakatumika kwa namna iliyo bora zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga hoja mkono na ahsanteni sana. (Makofi)