Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon Abubakar Damian Asenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilombero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa nafasi hii ya kuchangia Wizara yetu ya Maji. Mheshimiwa Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Waziri na Watumishi wa Wizara wasihuzunike, sisi tunasema ni mambo makubwa ya kuomba miradi, kuomba maji, kuomba fedha na madhali wanafanya kazi kwa bidii, Mwenyezi Mungu atawasaidia. Sisi tunawaombea Mwenyezi Mungu awasaidie wapate fedha, watusaidie kwenye miradi hii mikubwa ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama hapa, kama kawaida yangu, kusema mambo mawili; kwanza kushukuru na kuomba tena, kama wananchi wa Kilombero walivyonituma. Leo nimepokea simu ya Mwalimu wangu wa Kiswahili, anaitwa Joram Mkumbi, Mzee wa Ulumbi, ameniambia nimeona video TikTok, Ifakara inafumuliwa mitaro. Wanataka kufanya nini Ifakara? Nikamwambia Mwalimu Joram Mkumbi, ile si mitaro. Yale ni mabomba makubwa ya Mradi wa Maji wa Kiburubutu wa shilingi bilioni 45 ambazo Halmashauri ya Mji wa Ifakara imepewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipoingia kwenye uchaguzi Mwaka 2020, tuliahidi jambo hili. Nina mambo makubwa ya lami na mradi huu wa maji, Wakati tunasema Chama Cha Mapinduzi tunaomba kura, wananchi waliona kama hadithi, pengine tunadanganya; leo matenki kule yamefika karibu 70% na Ifakara Mjini pale, kata zote tisa za Tarafa ya Ifakara, watu wanaona mji unafukuliwa mabomba ambamo binadamu anaweza akatembea, yanapita Ifakara Mjini kwenda kusambaza maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia kwa mradi huo mkubwa. Sasa Mwalimu wangu wa Kiswahili akasema, maneno ya Kiswahili yapo haba kwenye kushukuru, akasema ukienda pale, simama kwa turuhani na urua, mshukuru Waziri, mshukuru Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Injinia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwambia Mheshimiwa Waziri, miezi miwili iliyopita Injinia aliniazimia eskaveta tukaenda kuboresha tuta pale Ifakara. Kama si Katibu Mkuu wa Maji kunipa lile eskaveta, basi leo athari ya mafuriko ingekuwa kubwa sana katika Mji wa Ifakara. Ninamshukuru kwa kiasi kikubwa sana kwa hiyo, nimesimama hapa kutoa shukrani belebele, shukrani teletele na shukrani jazira kwa kazi kubwa, ambayo Mheshimiwa Waziri ameifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amekuja jimboni kwangu, nimemwambia kuhusu ule mto, amefika ametembea. Sijawahi kuona Waziri anatembea kwa mguu porini kwenye vichaka, karibu kilometa nzima, anaenda kuona sehemu ambako mto umezibwa. Waziri mwingine angebaki kwenye gari tu, lakini ametembea kwa mguu, amefika mtoni, ameona namna mto ule ulivyoziba. Nisimkushukuru kwa kweli, nitakuwa mchoyo wa fadhila. Sasa ninaomba nini Mheshimiwa Waziri, kwa sababu, dakika ni tano?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ni hilo la ule mto aliouona. Wizara ya Kilimo wanataka kujenga mabwawa na skimu za umwagiliaji. Ule mto, Wizara ya Nishati wanautaka kwa sababu, unamwaga maji katika Bwawa la Mwalimu Nyerere. Sisi tuna kilometa takribani tatu au nne kutoka Kibaoni mpaka Lipangalala. Mheshimiwa Waziri, ninavyozungumza naye kuna wananchi zaidi ya 100 wako Shule ya Msingi Lipangalala baada ya nyumba zao kujaa maji kwa sababu, mto ule umejaa uchafu, umejaa takataka. Maji kidogo tu, mvua kidogo, maji yanamwagwa kwa wananchi na lile tuta la zamani limeharibika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeongea na Mamlaka ya Bonde, nimeongea na Katibu Mkuu ameniambia atanisaidia na wewe nisaidie vifaa ama pesa kidogo zikakae pale zifukue mto ule, zirejeshe yale matuta, yale maji yakamwagwe Mto Kilombero yaende Bwawa la Mwalimu Nyerere. Ni maji muhimu sana kwa nchi yetu. Ninazungumza katika hali ambayo Waziri mwenyewe amefika na ameona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hilo ni jambo la msingi sana. Sitamani kwenda kushika shilingi yako Mheshimiwa Waziri kuhusu jambo hili. Wananchi wa Ifakara leo, wa Jimbo la Kilombero, wanaangalia Mbunge atasema nini kuhusu mafuriko tuliyoyapata au kazi yake ni kutuletea unga tu? Sasa haiwezi Wizara nzima, Mheshimiwa Waziri Juma Aweso na Mwenyekiti wa Mkoa, Msisimbi, wakakosa eskaveta na ma-tipper mawili kukaa pale kufukua mto ule? Mwenyezi Mungu ambariki atusaidie jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, ninaomba shilingi 60,000,000 tu, maji ya Kidatu Solar Station ni machache. Nimeongea na Meneja mzuri wa RUWASA, anaitwa Engineer Mlelwa, Kilombero akasema tukipata shilingi 60,000,000 tu pale Kata ya Kidatu, Msolwa Station wataongezewa maji. Ameniambia wamefanya upembuzi yakinifu kwa Mradi wa Iyanga na Lumemwe yote kupata maji, shilingi 680,000,000 zinatakiwa na tenki pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna matenki pale Mradi wa Barabara; wale Waisraeli wameacha matenki makubwa. Yale matenki yanataka mnara ili tuyatumie kuleta maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, siyo kwa umuhimu, ninaomba shilingi 67,000,000 za ukarabati wa Mradi wa Maji wa Mwaya, katika Kata ya Mwaya yenye watu wengi pia. Mwaya kuna watu 40,000 wanahudumiwa na mradi huo. Ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri anisaidie mambo hayo. Mungu ambariki sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja. (Makofi)