Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Babati Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. EMMANUEL J. KHAMBAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Wizara yetu ya Maji, ambayo ni Wizara muhimu kwa nchi yetu. Ninatumia nafasi hii, kwanza kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Dhamira yake ya dhati kabisa ya kuhakikisha anamtua mwanamama ndoo kichwani ameitekeleza kwa vitendo katika maeneo mengi nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maendeleo ni mchakato. Tunajua kwamba, zipo changamoto, lakini kwa namna ambavyo bajeti hii ya zaidi ya shilingi trilioni moja tukiipitisha, sisi Wabunge wote leo, ni dhahiri fedha hizo zikisimamiwa kwa weledi zitakwenda kutatua changamoto ya maji katika maeneo mbalimbali nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda nitajikita kwenye mambo machache. Kwanza, ninaipongeza Wizara, kupitia Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kubuni Mpango mzima wa Gridi ya Taifa ya Maji. Ninaamini ukikamilika utakwenda kutatua changamoto ya maji katika maeneo mengi nchini, lakini pamoja na ubunifu huo, ninapenda kuishauri Wizara kujikita katika mfumo wa kutumia mita janja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mita janja itasaidia, kwanza Wizara yenyewe kupitia wasaidizi wenu, kuweza kusimamia upotevu wa maji nchini. Katika mitandao yetu yote ya maji nchini tukiweka mfumo huu utasaidia kudhibiti maji yasipotee na Serikali iweze kuendelea kupata fedha ambazo zitaendelea kusaidia miradi mingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala zima la mita janja litatusaidia hata katika maeneo mengine ambayo wananchi wamekuwa wakibambikiziwa bili za maji kwa sababu, mwananchi ataweza kununua maji kama anavyonunua vocha, kama anavyonunua umeme. Hivyo itakuwa ni pre-paid.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatumia nafasi hii, wanasema asiyeshukuru kwa yai hata akipewa kuku hatashukuru. Sisi watu wa Jimbo la Babati Mjini tunaishukuru Serikali, chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa miradi mbalimbali ambayo ipo katika Jimbo la Babati Mjini. Hapa karibuni tumepata miradi ya visima katika Kata ya Bonga, Kata ya Singe na Kata ya Nangara, ambayo tunatazamia gari hilo likitoka upande wa Babati Vijijini litaelekea Babati Mjini na kuendelea kuchimba visima katika maeneo hayo na wananchi waendelee kupata huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendelea kuipongeza Serikali kwa kutupa Mradi wa Mto Eri, Maisaka, Eneo la Sawe, ambapo tenki kuu litakwenda kujengwa na kuweza kuhudumia Eneo la Maisaka, Katani, ambako Mji wa Babati ndio unakoelekea. Ninamwomba Waziri wa Maji, zile shilingi 16,000,000,000 katika hii shilingi trilioni 1.2 ambayo tunakwenda kuidhinisha leo, fedha zitoke kwa sababu, utaratibu wa ujenzi au mchakato wa maji umeanza. Tunamwomba Waziri atupatie fedha hizo, ili mradi uweze kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatumia nafasi hii kuipongeza Wizara ya Maji, ndiyo Wizara pekee inayotumia mfumo wa Force Account na kuonesha performance ya hali ya juu nchini. Hivyo, ninawaomba katika miradi ambayo imesalia, Mradi wa Maji Taka wa Babati muweze kusaidia kuukamilisha. Tunashukuru wametoa shilingi 700,000,000 lakini mkandarasi anahitaji shilingi bilioni 1.9, ili aweze kurudi site.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba waweze kutupatia fedha hizo, ikiwezekana kabla ya Bajeti ya Mwaka Mpya wa Fedha wa Serikali kuja, ili mkandarasi aweze kurudi site na fedha ambazo Serikali imetoa ziweze kuonesha thamani, tuone best value for money na wananchi wa Jimbo la Babati Mjini waendelee kunufaika na huduma ya maji taka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda, ninaomba kuunga mkono hoja kwa kumpongeza Waziri, Naibu Waziri na Mkurugenzi wangu wa Maji, Iddi Msuya, pale Babati. Ninakushukuru sana. (Makofi)