Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Agnesta Lambert Kaiza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili jioni ya leo niweze kuchangia kwa ufupi katika hii bajeti ya Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kwanza kabisa niungane pamoja na Wabunge wengine ambao wamempongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri na jitihada njema ambazo anazionesha kwa upande wa maji kwa maana ya kumtua mwanamke ndoo kichwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza kwa sababu ndani ya Jimbo langu la Segerea mpaka hivi ninavyoongea tayari tumepata tabasamu kutoka kwa Mheshimiwa Rais, kwani tumeweza kuchimbiwa visima vitatu ndani ya Kata tatu, Kata ambazo zilikuwa hazina maji kabisa, lakini hivi ninavyoongea, siku chache zijazo Kata ya Kimanga, Kata ya Kisukuru na Kata ya Segerea watakwenda kupata maji baada ya kuwa wameyakosa maji kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kumpongeza Mheshimiwa Rais, ninaomba kwa haraka sana niende kumpongeza Waziri Aweso pamoja na timu yake. Niseme ninaunga hoja bajeti hii ambayo Mheshimiwa Aweso ameiwasilisha kuanzia siku ya jana na ninaiunga mkono kwa sababu, imebeba ndoto za Mheshimiwa Rais za kumtua mwanamke ndoo kichwani, wakiwemo wanawake wa Mkoa wa Dar es Salaam, hususan wanawake wa Jimbo la Segerea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka pia niipongeze timu nzima ya DAWASA, Mkoa wa Dar es Salaam chini ya mtu bingwa kabisa Engineer Bwire kwa kazi nzuri wanayoifanya kuhakikisha wanawake wa Mkoa wa Dar es Salaam tunapata maji safi na salama. Kwa ajili ya muda ningeweza kuwapongeza hata mameneja wangu wa Jimbo la Segerea, lakini itoshe kusema kwamba kazi yao ni kubwa na ninawashukuru sana kwa ushirikiano mkubwa ambao wananipatia mpaka hivi sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Segerea lina Kata 13, Mitaa 61. nimekuwa nikisema ndani ya Bunge hili na uzuri Waziri amekuja ndani ya Jimbo la Segerea, amejionea kwa macho, tulitembea mguu kwa mguu aliona jinsi gani ambavyo wananchi wa Jimbo la Segerea wana uhaba mkubwa wa maji safi na salama. Kwa sababu hii Mheshimiwa Waziri, uhaba wa maji ndani ya Jimbo la Segerea una sababu nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ya kwanza, ukiangalia takwimu ya uzalishaji wa maji kwa sasa takwimu zinasema kwamba uzalishaji ni ujazo wa lita 534,000,000 kwa siku, wakati mahitaji ya Mkoa wa Dar es Salaam ni lita 750,000,000 na ukiangalia hapa ina maana kuna pungufu ya lita 216,000,000. Waziri ni wazi kabisa mapungufu haya, ndiyo yanayopelekea wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam na hususan Jimbo la Segerea tusipate maji safi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatambua upo mpango mkubwa kabisa wa Mheshimiwa Rais kutoka kwenye mradi mkubwa wa Kidunda. Ninaipongeza Serikali kwa sababu itakwenda kusaidia kwa sehemu kubwa kwa maana kipindi cha ukame, wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam wataweza kupata maji safi na salama. Kutokana na huo upungufu ambao nimeusema Mheshimiwa Waziri, ningeomba kwa haraka haraka ule Mradi wa Rufiji uwekewe kipaumbele Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafahamu wazi kabisa kwamba ni pesa nyingi inahitajika, lakini wengine wamesema kwamba pasipo maji hakuna uhai kwa sababu uhai ndiyo maisha. Hivyo Mheshimiwa Waziri hatuna budi kuwekeza katika uhai kwa kuwapatia wananchi maji safi na salama. Hivyo, niishauri Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan, Serikali ambayo ninajua kwamba ni sikivu kabisa iweze kuwekeza nguvu kubwa kwa ajili ya ule Mradi wa Rufiji, ili sasa wananchi wa Jimbo la Segerea na Mkoa wa Dar es Salaam kiujumla tuweze kupata maji safi na salama tofauti na jinsi ilivyo sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema zipo sababu nyingi zinazopelekea Mkoa wa Dar es Salaam tusipate maji safi na salama, nyingine ni ubovu wa miundombinu. Mheshimiwa Waziri anafahamu tumekwisha kuongea sana, Jimbo la Segerea miundombinu ni chakavu inahitaji kubadilishwa. Hata ukiangalia kwenye Kata zote kule, yale mabomba tu yaliyotandikwa kule chini ni vile vibomba vidogo kabisa ambavyo, hata ukiyafungulia maji, namna gani maji yanakuja kwa presha ndogo kwa sababu watu wamekuwa ni wengi, demand ni kubwa, viwanda ni vingi na kwa sababu hiyo nimwombe Mheshimiwa Waziri, chonde chonde tunaomba uboreshaji wa miundombinu ndani ya Jimbo la Segerea na Mkoa wa Dar es Salaam kiujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia ninaleta ombi kwako Mheshimiwa Aweso. Nimwombe wakati tunasubiria mradi huu mkubwa wa Kidunda pamoja na Rufiji na kwa sababu wananchi wa Jimbo la Segerea hatupati maji kabisa katika maeneo mengi, niko chini ya miguu yako Mheshimiwa Aweso, aende akatuchimbie visima kimoja katika kila Kata, ili wananchi wa Jimbo la Segerea, Mheshimiwa Waziri waweze kupata maji safi na salama huku wakisubiri mambo makubwa ambayo Serikali inayapanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ajili ya muda ninaomba nimalize kwa kusema, kaka yangu Mheshimiwa Aweso anaupiga mwingi, yeye na timu yake nzima. Jana wakati anahutubia aliona makofi mengi ndani ya hili Bunge siyo kwamba ni unafiki, mimi mwenyewe nilipiga makofi mpaka mikono ikaumia kabisa, ni kwa sababu yeye ni msikivu, lakini pia hapandishi mabega pale ambapo tunakwenda kwake kwa ajili ya kuhitaji huduma. Mheshimiwa Aweso Mwenyezi Mungu ambariki, lakini nitaomba wakati ana-wind up aniambie kaka yangu mpendwa je, visima atatuchimbia ndani ya Jimbo la Segerea?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)