Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Thomas Maganga Kampala

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Katavi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. THOMAS K. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kupata nafasi ya kuchangia hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Maji. Ninaomba ku-declare interest, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nichukue fursa hii kumpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya na kwa ongezeko kubwa la bajeti. Mwaka 2021 bajeti ilikuwa ni shilingi 697,000,000,000 leo tunavyoongea Mwaka wa Fedha 2026/2027 ni shilingi trilioni 1.1. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii ni kubwa sana. Ninampongeza sana Mheshimiwa Rais. Watanzania tunayo kasumba moja, huwa hatumpongezi mtu akiwa kwenye nafasi, huwa tunasubiri mpaka atoke. Mheshimiwa Rais huko aliko Mama akae kwa kutulia. Ninaamini baada ya kuondoka mwaka 2030 hawa hawa leo ambao hawazioni kazi zake, watampongeza wala asiwe na wasiwasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ninataka nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, yeye na timu yake wanafanya kazi nzuri sana. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri ameitoa Wizara hii mbali, miaka tisa kwenye wizara hii iliyokuwa na changamoto nyingi na ametoboa. Ndugu yangu ni kidume, afanye kazi na sisi Wabunge tuko nyuma yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu wa tatu wa kumpongeza kwenye wizara hii ni dada yangu Engineer, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, dada yangu, anafanya kazi kubwa sana ya kumsaidia Mheshimiwa Waziri. Ninataka nimwambie dada yangu huko aliko apokee maua yake na ninataka nimwambie; ninaamini kwa kazi kubwa anayowasaidia akina mama wa nchi hii, ana kiti chake mbinguni. Kama Mheshimiwa Katibu Mkuu huko aliko apokee maua yake, dhambi zake nipewe mimi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nichukue fursa hii pia kuwashukuru watendaji wote DG wa RUWASA anafanya kazi kubwa sana kaka yangu. Sisi tulioko vijijini ndiyo tunajua umuhimu wa RUWASA, DG anafanya kazi kubwa nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti iliyopita mimi ni Jimbo la Katavi nimepata shilingi 8,000,000,000. Kati ya shilingi 8,000,000,000 nilizopata shilingi 4,000,000,000 tayari zipo kwenye miradi na miradi inaendelea. Shilingi 8,000,000,000 niliyoipata inakwenda kutekeleza miradi ifuatayo:-

Mradi wa Nsenkwa, Inyonga shilingi bilioni 1.5, mradi wa ujenzi wa Kamsisi, Nsenkwa, Inyonga, Ilela shilingi bilioni 2.8, ujenzi wa mtandao wa maji vijiji nane, ujenzi wa utumiaji wa maji Ilunde shilingi milioni 700.3 na hivi ninavyoongea kuna mradi unaendelea kwenye Kata ya Kamsisi, Kijiji cha Imalauduki. Kazi yangu leo mimi ni moja tu kwa hizi raha anazonipa Mheshimiwa Waziri kwenye maji, kusukuma jahazi ili kazi kule ziendelee kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nimwambie Mheshimiwa Waziri, wakati Rais anapita kufanya kampeni 2025, tulimwambia sisi wananchi wa Jimbo la Katavi tutampigia kura kama tumechanganyikiwa na sababu mojawapo tuliyokuwa nayo ni hii kwenye huduma za maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nimwombe sana Waziri kwa unyenyekevu mkubwa sana atakapokuja ku-wind up ninaomba atueleze wana mpango gani na kusukuma mtandao wa maji, Gridi ya Taifa ya Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo kwa sababu raha zimenizidi, ninataka nimwambie Mheshimiwa Waziri ninamshukuru sana, Bwawa la Nzengo linakwenda kwa kasi sana na ajitahidi baada ya kukamilika aje alifungue.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo, ninasema ahsante sana, wamsalimie Mama Samia. (Makofi)