Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduru Kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ENG. FADHILI S. CHILOMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Nimechangia kwa maandishi kwa hiyo hapa nitafanya mambo mawili tu; nitatoa shukrani na kutoa ushauri kidogo. Shukrani zangu za dhati ninaomba zimfikie Rais kama wanavyosema wenzangu, kazi inafanyika na tunaiona. Kwa namna ya pekee kabisa na kwa unyenyekevu mkubwa, ninaomba niwashukuru Waziri wa Maji, Naibu Waziri pamoja na Katibu Mkuu, pamoja na wafanyakazi wote wa Wizara ya Maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini ninawashukuru kwa unyenyekevu? Wakati ninaingia kwenye Bunge hili kwenye Jimbo la Tunduru Kusini ninakotokea, kuna jumla ya miradi mitano imekwama kabisa. Miradi hii ni Tuwemacho, Msinji, Masugulu, Misechela na Mradi wa Igoma. Hii miradi ilikuwa imekwama kabisa kwa sababu ya changamoto ya fedha. Nilipokuja hapa nilimfuata Naibu Waziri, Waziri hakuwepo, watu hawa ni wasikivu sana, ninaungana na watu wote wanaowaombea kheri hawa watu. Waliniita tukaenda tukafanya mkutano kwenye ofisi zao pale pamoja na wafanyakazi wote wa Wizara, tunajadili issue ya Tunduru. Wametoa commitment yenye mwelekeo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyoongea leo hawa watu wametoa jumla ya shilingi 200,000,000 kwenda kuanza kukwamua Mradi wa Tuwemacho, zaidi ya yote tumewekeana utaratibu kwamba Bunge hili likiisha kazi ya kwanza inayoenda kufanyika ni kwenda kuzindua ule mradi, wameenda mbali zaidi wametoa na gari jipya kwa ajili ya Wilaya ya Tunduru. Hawa watu tunawashukuru mno.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizi ninaomba nitoe ushauri, watu wameongea sana hapa habari za vyanzo vya maji na mambo mengi yameongelewa, lakini kwenye chanzo hapo kuna kitu ninataka nishauri. Dunia hii watu wanaongezeka na ardhi haiongezeki, haya maji tunayoendelea kuyatumia ni yale yale, lakini kuna chanzo kimoja ninaona hakiongelewi sana. Serikali pamoja na jitihada zote inazozifanya za kuwekeza kwenye maji, ninashauri ianze kufanya sensitization ya kuwafanya watu waweze kuvuna maji ya mvua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kitu hakieleweki, unaweza ukaenda kwenye eneo mfano labda Mkoa wa Morogoro pale, kuna kipindi watu kila mwaka wanahangaika na mafuriko, sasa kinachoshangaza ni kwamba, wiki hii wanahangaika na mafuriko, mafuriko yakiisha, wiki ijayo wanasema sisi hatuna maji. Hivi vitu haviumani!
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukijenga nyumba kwa mfano, yenye upana wa mita tatu, urefu wa mita tisa, ukaezeka, lile bati kule juu linakuwa na upana wa square metre 38. Chukulia mfano hiyo nyumba umeijenga Dodoma, tafiti zinaonesha kwamba Dodoma ndiyo sehemu ambayo inapata maji kidogo, lakini kwenye tafiti pale inaonesha kwamba Dodoma average ya mvua inaonesha ni mililita 556.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu aliyejenga nyumba hiyo yenye urefu nilioutaja, mvua ikinyesha Dodoma, akiyavuna yale maji anapata lita zisizopungua 21,128, ambazo ukilinganisha na tafiti zinavyosema, kama ile nyumba imejengwa kijiijini na mtu akavuna maji maana yake ni kwamba, atakuwa na uwezo wa kupata maji ambayo anaweza kuyatumia siku 444, sawasawa na karibu mwaka mzima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo huo….
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. ENG. FADHILI S. CHILOMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)