Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkinga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TWAHA S. MWAKIOJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nitumie nafasi hii kukushukuru kwa nafasi hii. Pili, nitumie nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya na uhai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie tena nafsi hii kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa namna ambavyo anaendelea kuitendea mema na kuwatendea mema Watanzania. Mambo anayoyatenda yote, viashiria vyote vya kiuchumi na vya kijamii vinaonesha positive trend. Kwa hiyo, tuna kila sababu ya kumshukuru, kumpongeza na kumwombea Mungu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mtume wetu Muhammad (S.A.W) anasema kwamba mtu yeyote atakayewafanyia wema, basi tumlipe mithili ya wema anaotufanyia na kama itatokea kushindwa kumlipa kwa wema huo, basi tumwombee Mungu. Mimi binafsi na wananchi wenzangu wa Mkinga na Watanzania wengine tunaendelea kumwombea Mungu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa wema mwingi anaotutendea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue pia nafasi hii kumpongeza sana Waziri, kaka yangu Mheshimiwa Juma Aweso, Ndugu yangu huyu ni mtu rahimu sana, ni mtu mnyenyekevu sana, ni mchapakazi sana na kwa kweli ndani ya Wizara yake wanaishi kama familia. Ukimwangalia Engineer, dada yangu huyu wa Kinyamwezi ni mtu mwema sana, anatusaidia sana na Wizara hii ina mwenezi kwa namna wanafavyofanya kazi, ninawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichangie katika maeneo matano kwa haraka haraka. Eneo la kwanza, nizungumzie suala la Gridi ya Taifa. Kwa kweli suala hili Mheshimiwa Waziri ni muhimu sana, limekuja wakati sahihi, limekuja katika mazingira sahihi na mahitaji ya wakati wa sasa, tunahitaji hasa kuwa na gridi ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Wilaya yetu ya Mkinga haijajumuishwa katika mpango huu wa gridi ya Taifa, nimwombe Waziri kwa unyenyekevu mkubwa, wananchi wenzangu wa Wilaya ya Mkinga, hususan wa Tarafa ya Maramba, wanasumbuka sana na hali ya upatikanaji wa maji safi na salama, hususan kipindi cha kiangazi. Waziri atufikirie kama mradi huu unafika Muheza, mradi huu unafika Korogwe, mradi huu umefika Pangani na sisi watu wa Mkinga chonde chonde, ndugu zangu wa Maramba hawatanielewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshaliongea hili sana, ninaomba atakapokuja Mheshimiwa Waziri, kaka yangu sina maneno mengi ya kumwambia, lakini aniambie ni namna gani na Wilaya yetu ya Mkinga anakwenda kuijumuisha kwenye Gridi hii ya Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, nizungumzie suala la ukamilishaji wa miradi iliyoanza. Katika Wilaya yetu ya Mkinga tuna miradi mingi ambayo haijakamilika, mradi mkubwa ni Mradi wa Tanga – Mkinga, Tanga – Horohoro. Mradi huu kwa kweli mpaka sasa tunamshukuru Mheshimiwa Samia ametuwekea shilingi 35,000,000, huo umeshaanza kutoa maji katika Kata ya Mtimbwani, tumeambiwa mwezi Oktoba utakamilika, tarehe hizi, Mheshimiwa Waziri nimwombe zisibadilike. Wananchi wa Mkinga wana hamu sana na maji haya, wameyakosa muda mrefu, wanaendelea kumshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maji haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi mingine ambayo haijakamilika ni Mradi wa Mhinduro, Mradi wa Gombero, Mradi wa Mapatano, Mradi wa Daluni na Mradi wa Bwiti. Ninamwomba Mheshimiwa Waziri tukimpitishia bajeti hii, katika mwaka unaoanza Julai atukamilishie miradi hii ili na sisi watu wa Mkinga tuweze kufurahia mema ya Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu, nizungumzie suala la upotevu wa maji. Wamesema wengi...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MHE. TWAHA S. MWAKIOJA: Nimalizie kwa kusema, ninaona muda umenitupa mkono; nilitaka kuzungumzia suala hilo. Nizungumzie pre paid meter nalo ni muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kabisa, niiombe Wizara ya Fedha na Serikali kwa ujumla ihakikishe Wizara hii inapatiwa fedha kwa wakati ili iweze kuwasaidia wananchi. Ni Wizara pekee ambayo huduma yake haikwepeki hata kwa dakika moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha na ninaomba niunge mkono hoja. Ahsanteni sana. (Makofi)