Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Deodatus Philip Mwanyika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Njombe Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa nafasi ya kuchangia katika hoja iliyo mbele yetu. Awali ya yote, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme, kwamba sisi Wananjombe Mjini tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, tumekuwa na miradi mingi kwa mara ya kwanza. Njombe haikuwa na miradi mikubwa ya maji, lakini katika kipindi cha miaka mitano tumepata takriban shilingi 58,000,000,000 kwa miradi mikubwa mitatu ya maji kwa ajili ya Mji wa Njombe unaokua kwa haraka sana. Kwa hiyo tunaishukuru sana Wizara kwa utekelezaji mzuri, tunawashukuru sana NJUWASA ambao wamefanya kazi nzuri wakiongozwa na viongozi wa NJUWASA pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo yote Njombe Mjini bado haijaeleweka kwa Wizara ya Maji. Njombe Mjini ni halmashauri ambayo ina mji na vijiji. Tuna vijiji 44; lakini katika vijiji hivyo 44 tuna tatizo kubwa sana la maji. Nimelisema hapa, nimelirudia na kulirudia kila mwaka. Niombe Mheshimiwa Waziri atuangalie sana Njombe Mjini, kwa maana ya Njombe Vijijini. Katika miaka mitatu iliyopita yote hatujawa na mradi wowote uliotekelezwa katika maeneo ya vijiji. Mwaka jana nilisema hapa kwamba tumeondolewa mpango mzima wa P4R kwa sababu tunaonekana tupo mjini lakini tuna vijiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru mwaka jana tukapewa Mradi wa Kifanya, tukaingia kwenye makaratasi. Mradi huo ukafanyiwa usanifu, tenda zikatayarishwa, mikataba ikawa tayari kusainiwa, lakini ikasimamishwa; hata huo nao haukuendelea. Nimwombe sana Mheshimiwa Aweso sana, ninaomba atumie kila uwezo alionao angalau tuwe na mradi Njombe Vijijini katika kipindi hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatambua kwamba tuna Mradi mwingine mkubwa wa Igongwi. Nimeongea kwa muda mrefu sana na Mheshimiwa Aweso anaufahamu huo mradi. Mradi wa Igongwi ni mradi mdogo wa bilioni 4.7; cha kusikitisha ni kwamba mradi huu una miaka 10 haujakamilika. Mradi una lot nne, lot ya kwanza imekamilika, lot ya pili imekamilika, lakini tuna lot ya tatu na ya nne, ndiyo juzi, juzi. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri baada ya kumlilia akam-authorise Katibu Mkuu atupatie angalau fedha kidogo, tunashukuru kwa hilo limesukuma. Hata hivyo tunaomba huu Mradi wa Igongwi upewe kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafahamu kuwa upo kwenye mpango; lakini kuwekwa kwenye mpango ni jambo moja na kupata fedha za utekelezaji ni jambo lingine. Niombe sana upewe kipaumbele. Haiwezekani mradi wa 4.7 billion ukakaa miaka 10. Niombe sana wananchi wa vijiji vinavyohusiana na mradi huu wapate hiyo haki yao ambayo kweli wanastahili kwa maana ni wa muda mrefu. Tuna Vijiji vya Kitulila, Madobole, Luponde, Buwemba, Njomlole, Magoda na Ikisa. Vijiji vyote hivi havina maji; na Kijiji cha Uwemba ndicho ninachotoka mimi, hakina maji. Nimwombe sana Mheshimiwa Aweso atusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Kifanya ambao umeondolewa kwa sababu za kitaalam pengine, mimi sizijui; lakini niseme mradi huu ni mradi ambao Mheshimiwa Rais marehemu Magufuli alipita eneo la Kifanya akiwa na Waziri wa Maji Mheshimiwa Mnyaa Mbarawa, wakawaahidi wananchi, wakawaambia kwamba utatekelezwa ndani ya miaka miwili, lakini hadi leo mradi huu haujatekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika usanifu wananchi wamehusishwa, kwa hiyo wanaufahamu vizuri, wanauongelea lakini hawajaona huo mradi. Niombe sana, mradi wa Kifanya ninajua hajauweka kwenye bajeti kwa sababu anasema ni mradi mpya; lakini in fairness mradi huu ulitakiwa uwepo, kwa sababu hatujapata mradi vijijini katika miaka mitatu; hata huu uliowekwa umetolewa. Kwa hiyo nimwombe sana atuangalie kwa jicho la pekee sana watu wa Halmashauri ya Njombe Mjini na maeneo ya vijijini ambayo yanahitaji jicho la kipekee ili yaweze kuangaliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru tuna mradi wa majitaka; mradi huu unakwenda vizuri lakini unahitaji kukamilishwa. Njombe imefikia mahali ambapo inatakiwa iwe manispaa, haiwezi kuwa kama hakuna mradi wa majitaka. Tuombe sana mradi huu wa maji taka nao ukamilishwe kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa tuna mradi mdogo sana ambao niliomba nao uangaliwe. Tuna jengo la ofisi pale mjini la NJUWASA, tuombe sana nao uangaliwe kwa sababu pale Njombe tunatumia ofisi za mkoloni hadi leo. Tuombe kwamba angalau tuangaliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja. (Makofi)